Habari za Punde

Maximo apata ulaji Yanga. Anakuja wiki ijayo kuanza kibarua chake





Na Salum Vuai, Maelezo
KOCHA wa zamani wa timu ya Taifa ya Tanzania Marcio Maximo, anatarajiwa kuwasili nchini wakati wowote wiki ijayo kwa ajili ya kuanza kazi mpya ya kuifundisha klabu ya Yanga.

Mtihani wa kwanza kwa Mbrazili huyo utakuwa kuiandaa timu hiyo kwa ajili ya kutetea ubingwa wake wa michuano ya klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati Marcio Maximo‘Kagame Cup, iliyopangwa kufanyika jijini Dar es Salaam mwezi ujao.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu jana, Msemaji wa Yanga Louis Sendeu alithibitisha mpango wa timu yake kuingia mkataba na Maximo ingawa hakuwa tayari kufafanua utakuwa wa miaka mingapi na maslahi atakayopata.

“La msingi ni kwamba Yanga imezungumza na Maximo na tunatarajia atawasili wiki ijayo na atakapofika kila kitu kuhusu mkataba wake kitawekwa bayana”, alieleza Sendeu.

Hata hivyo, katika uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kutoka ndani ya klabu hiyo iliyoko mtaa wa Jangwani na Twiga, umebaini kuwa kocha huyo atakuja nchini pamoja na kocha msaidizi wa viungo.

Aidha, chanzo chetu kimeeleza kuwa, Maximo aliyeleta mapinduzi makubwa katika timu ya Taifa, ataambatana na mke wake kwa vile hatakuwa na mpango wa kurejea kwao hadi michuano ya Kagame itakapomalizika.

Mpasha habari wetu wa ndani ya klabu hiyo, pia amesema kuwa baada ya Maximo kukubaliana na Yanga kwa ajili ya kuinoa, ametoa mapendekezo kadhaa ya usajili wa wachezaji kwa ajili ya msimu ujao.

Mapendekezo hayo ni pamoja na usajili wa wachezaji kadhaa kwa ajili ya kikosi chake, na tayari klabu hiyo imekwishakamilisha kwa asilimia kubwa.

Miongoni mwa wanandinga hao ni golikipa Ali Mustapha ‘Barthez’ na beki wa kati wa Simba, Kelvin Yondani ambaye hata hivyo, usajili wake umeibua kasheshe na gumzo kubwa nchini.

Chanzo hicho kimesema kuwa tayari Barthez ameshasaini mkataba wa kukipiga na klabu hiyo, huku Yanga ikimtoa kwa mkopo mlinda mlango wake Shaaban Kado kurejea timu yake ya zamani ya Mtibwa Sugar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.