Habari za Punde

Tanzania yaalikwa kutunga wimbo wa ACP

 DAR ES SALAAM
WASANII wa Tanzania, wamealikwa kushiriki shindano la kutunga wimbo utakaokuwa unatumiwa kama wimbo rasmi wa mataifa ya Afrika, Karibiani na Pasifiki (ACP), ambao mshindi wake atazawadiwa euro elfu tano.

Taarifa hizi ni kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Ghonche Materego.

Materego amesema mwaliko huo umekuja kupitia BASATA kwa mwamvuli wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Tanzania.

Alieleza kuwa, shindano hilo litakalohusisha mataifa 79 wanachama wa umoja huo, limeandaliwa na Sekretarieti ya ACP kwa lengo la kupata wimbo ambao utabeba dhana ya mataifa wanachama ACP.

Amefahamisha kuwa, shindano hilo litahusu msanii mmoja mmoja au kikundi cha wasanii ambao watapaswa kutunga wimbo huo kwa kuzingatia lengo kuu la umoja huo ambalo ni ‘maendeleo endelevu na upunguzaji umaskini sambamba na ushawishi mkubwa kwenye uchumi wa dunia.

Aidha, wimbo huo utatakiwa uwe wenye kujenga moyo, fikra na kutangaza malengo ya kundi hilo la mataifa ya Afrika, Pasifiki na Karibiani.

BASATA imewahimiza wasanii wa Tanzania kujitokeza kwa wingi kushiriki shindano hilo ikisema hiyo ni heshima na fursa pekee ambayo taifa limepewa, kuonesha vipaji na uwezo wa wasanii wake kimataifa katika eneo la utunzi wa nyimbo, na pia kuitangaza sanaa ya muziki wa Tanzania nje ya mipaka yake.

Vigezo mbalimbali vimeainishwa wakati wa kutunga wimbo huo, ikiwa ni pamoja na kutakiwa utumie moja kati ya lugha rasmi za ACP, ambazo ni Kingereza, Kifaransa, Kihispaniola na Kireno, na mwisho wa kuzituma ACP ni Agosti 31, 2012.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.