Na Fatma Omar, WKUU
ASILIMIA 97 ya nyumba zote katika kijiji cha Matemwe Mbuyu tende, Mkoa wa Kaskazini Unguja, hazina vyoo, ambapo wakaazi wake wamekuwa wakijisaidia maporini haja kubwa na ndogo.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi, baadhi ya wanakijiji wa hapo, walisema kijiji chao kinakabiliwa na matatizo makubwa ya kimaendeleo na hivyo kuwa na shida kubwa ya kimaisha.
Waliyataja matatizo yanayowakabili kuwa ni pamoja na elimu duni ya mambo mbalimbali ikiwemo afya, elimu, ukosefu wa vyoo, maji safi na salama, umeme na miundombinu ya barabara jambo ambalo limekuwa likisababisha kuwa nyuma kimaendeleo ukilinganisha na vijiji vyengine vya mkoa huo.
Aidha uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi umebaini kuweko kwa matatizo hayo yote hasa la ukosefu wa vyoo, jambo ambalo linahatarisha afya za wakaazi wa kijiji hicho hasa mripuko wa maradhi ya matumbo katika msimu huu wa mvua za masika.
Ofisa kutoka Idara ya Uwezeshaji iliyo chini ya Wizara ya Kazi, Uwezeshaji wananchi kiuchumi na Ushirika, Zeana Ahmed, na maafisa wengine ambao walifika katika kijiji hicho kwa ajili ya uhakiki wa kujua huduma za kimaendeleo katika kijiji hicho ulibaini kujua hali hiyo.
Katika taarifa yake hiyo, ofisa huyo alisema mara baada ya kukamilika ukusanyaji wa taarifa, ulibaini ukosefu mkubwa wa huduma za vyoo kijijini hapo, jambo ambalo limechangiwa na umasikini mkubwa wa kipato cha wanakiji wa hapo.
Sambamba na hilo, lakini Ofisa huyo, alisema uelewa mdogo wa huduma ya utumiaji wa vyoo kwa wanakijiji hao umechangiwa kwa kiasi kikubwa kuwa na mwamko wa uchimbaji wa vyoo pamoja na matumizi yake.
"Bado inaonekana ukosefu wa umuhimu wa elimu ya afya ni ndogo katika kjiji hicho na kupelekea hofu ya ueneaji wa maradhi ya mripuko," alisema.
Alisema bado suala la maendeleo ya wanawake liko nyuma hali inayosababisha kufikiria masuala ya familia zaidi pekee bila ya kujali elimu ya afya ambapo pia inaonekana idadi kubwa ya wanawake katika kijiji hicho hawana elimu ya juu ya lazima.
Aidha ukusanyaji huo wa taarifa ulibaini wanawake wengi wa kijiji hicho kujishughulisha na kilimo duni cha tungule, mahindi, choroko, pamoja na viazi vikuu ambapo wanaume wamekuwa wakijishughulisha na uvuvi.
"Utaalamu wa kisasa wa mambo ya uvuvi na uanzishaji shughuli za kiuchumi zinakwenda sambamba na mabadiliko ya mahitaji ya watu pamoja na kutokuwa na vifaa vya kisasa vya kufanya shughuli hizo," alisema.
Kuhusu suala la ufugaji bado liko chini ya asilimia 5 ambapo wengi wao hawafugi kwa biashara bali hufuga kwa ajili ya chakula.
Kwa upande wa huduma za upatikanaji wa maji safi na salama katika kijiji hicho, imekuwa ya tabu sana ambapo wanakijiji hao hutumia visima chakavu vilivyochimbwa miaka 30 iliyopita na kukosa huduma ya utiaji wa dawa kutoka mamlaka husika ya maji.
Idara ya Uwezeshaji ilifika kijijini hapo hivi karibuni kwa ajili ya kukusanya taarifa mbalimbali za kimaendeleo na matatizo ya wakaazi wa kijiji hicho.
Bado tuko katika karne ya saba, wakati wenzetu wameshakua katika karne ya 21, lakini yote kwa yote Serikali bado inapaswa kulaumiwa kushindwa kutoa elimu stahiki pamoja na kutafuta namna ya kuboresha hali za wananchi wake ili waweze kuondokana na hali hio.
ReplyDelete