Habari za Punde

Atelekeza Mke Aliyezaa Watoto Wenye Kufanana na Nyani



Na Jumbe Ismailly, SINGIDA

MWANAHARUSI Juma (34) mkazi wa kijiji cha Ndulungu, wilayani Iramba ametorokwa na mumewe kutokana na kujifungua watoto wawili wanaofanana na nyani.

Mwanamke huyo mwenye familia ya watoto wanne wenye baba wawili tofauti aliolewa na mume wa kwanza na kujifungua mtoto wa kwanza, Fadhila Juma (15) mwaka 2007 kabla ya kuolewa na Sadick Selemani ambaye alimtoroka baada ya kumpatia watoto wawili wanaofanana na nyani.


Akizungumza na gazeti hili, mama huyo licha ya kuwa watoto hao ni binadamu lakini wamekuwa na mfanano mkubwa na nyani.

Alibainisha pia mama mzazi wa watoto hao kuwa watoto wake hao wenye matatizo wamekuwa wakishindwa kutembea mwendo mrefu bila kupumzika na kibaya zaidi wamekuwa wakipumua kwa shida sana na matumbo yao ni makubwa.

“Matumbo ya watoto wangu wawili wenye matatizo ni makubwa,macho yao ni mekundu kama mnavyoyaona na hupumua kwa shida sana kiasi cha kuwafanya washindwe kutembea umbali mrefu bila kupumzika”alisisitiza Mwanaharusi.

Aliweka bayana mama wa watoto hao wenye matatizo kwamba watoto hao alijifungua wakiwa katika hali ya kawaida kabisa, lakini walianza kuugua mara kwa mara na kusababisha kutoweza kuzungumza.

Alifafanua pia kwamba baada ya mtoto wake wa kwanza mwenye matatizo kuanza kuugua mara kwa mara alimpeleka katika Hospitali ya Mkoa wa Singida kwa ajili ya uchunguzi zaidi,lakini kwa mujibu wa maelezo ya madaktari waliomhudumia ni kwamba hakuwa na ugonjwa wowote zaidi ya kupungukiwa damu na kasha kuongezewa na kuruhusiwa kurudi nyumbani.

“Lakini nimekuwa nikijaribu kumshauri mume wangu Bwaba Sadick kabla hajanikimbia juu ya kuwapeleka watoto wetu wakafanyiwe uchunguzi zaidi kwenye hospitali za rufaa, hakuonyesha utayari wa kufanya hivyo zaidi ya kusema hana fedha za kuwashughulikia watoto wetu hawa”alisisitiza mama huyo kwa masikitoko makubwa.

Mwanaharusi alisema ndoa yake ilikuwa ni ya wake wawili naye alikuwa mke mdogo na ndipo baada ya kuona anambana sana mumewe juu ya matibabu ya watoto hao,ndipo mwaka 2010 mumewe aliamua kuondoka nyumbani hapo na kuhamia kwa mke mkubwa ambaye hakumtaja jina.

Hivyo kutokana na hali hiyo inayowakabili watoto hao,mama huyo anayeishi kwa kutegemea misaada midogo midogo kutoka kwa wasamaria wema alitumia fursa hiyo kuomba mashirika,Taasisi na wadau wengine kumsaidia ili aweze kuwapeleka watoto hao kwenye matibabu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kijiji hicho, Idd Abubakari Nyauli alisema baada ya jitihada za serikali ya kijiji kumwita mume wa mama huyo kutozaa matunda, wanaandaa utaratibu wa kumfikisha kwenye vyombo vya sheria ili sheria ziweze kufuata mkondo wake.

1 comment:

  1. Ninaomba namba yake ya simu kama Tigo au Voda ili nasi tuweze kumsaidia kwa kadri Allah atakavyotuwezesha..Tunamtakia subra juu ya mtihani huu na mengine, kwani hujafa hujaumbika.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.