UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika,
kwa ruhusa yako naomba kutoa
hoja kwamba Baraza lako tukufu sasa
likae kama Kamati ya matumizi ili liweze kupokea, kuzingatia, kujadili,
kuchangia na hatimae liweze kuidhinisha
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kwa
mwaka wa Fedha 2012/2013.
2. Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda
kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukutana leo hii katika Baraza hili
tukufu, kwa lengo la kujadili masuala muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu.
3. Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya viongozi na
wafanyakazi wote wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, napenda kumpongeza Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dk. Ali Mohammed
Shein kwa kuwa mstari wa mbele katika
kuhakikisha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inafanya kazi ya kuwahudumia
wananchi. Utaratibu aliouanzisha wa kukutana na taasisi za Serikali na kupokea
taarifa za utekelezaji wa kila robo mwaka una madhumuni ya kukuza ufanisi
katika utendaji wa shughuli za Serikali ili kuweza kuwatumikia wananchi vizuri
zaidi.
4. Mheshimiwa Spika, vile vile sina budi kuwapongeza viongozi
wetu wa kitaifa Makamu wa Kwanza wa Rais Mheshimiwa Maalim Seif Sharif
Hamad na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi kwa jitihada zao za
kumsaidia Mheshimiwa Rais kuwatumikia wananchi wa Zanzibar. Mwaka mmoja wa
utekelezaji wa bajeti umeonesha dhahiri umahiri na umakini walionao viongozi
wetu hao.
5. Mheshimiwa Spika, napenda kutoa shukurani za pekee
kwa Mhe, Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad ambaye ndiye
msimamizi mkuu wa Ofisi hii, kwa ushauri wake na miongozo anayonipatia katika
utekelezaji wa majukumu yangu ya kila siku. Kwa hakika busara, hekima na uwezo
wake wa kusimamia majukumu yake, yananipa muongozo juu ya namna bora ya
kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika utekelezaji wa
majukumu yangu. Naendelea kumuhakikishia kuwa nitajitahidi kadri Mwenyezi Mungu
atakavyoniwezesha kusimamia vizuri majukumu yaliyo chini ya Ofisi ya Makamu wa
Kwanza wa Rais.
6. Mheshimiwa Spika, napenda pia uniruhusu kukupongeza
wewe binafsi na wasaidizi wako kwa kuliongoza Baraza hili tukufu kufuatana na
sheria na kanuni za Baraza zikichangiwa na hekima na uadilifu mulionao. Umahiri
wa utendaji kazi wenu unadhihirisha wazi pale inapotokea mijadala mizito na
ikafikia maamuzi muwafaka.
7. Mheshimiwa Spika, naomba kuchukua nafasi hii kuipongeza Kamati ya Kusimamia Ofisi za
Viongozi Wakuu wa Kitaifa inayoongozwa na Mheshimiwa Hamza Hassan Juma
Mwakilishi wa Wananchi wa Jimbo la Kwamtipura kwa kufanya nao kazi kwa
mashirikiano makubwa. Kwa hakika Ofisi yetu inathamini sana michango, ushauri
na maelekezo mbali mbali wanayotupa ambayo sio tu husaidia kutupatia mafanikio
katika utekelezaji wa majukumu ya ofisi yetu lakini pia hutuwezesha kukabiliana
na changamoto zinazotukabili.
8. Mheshimiwa Spika, pia napenda kuwashukuru wajumbe
wenzangu wa Baraza hili Tukufu la Wawakilishi, kwa kutoa ushirikiano wao wa
dhati kwangu mimi binafsi pamoja na watendaji wa Ofisi yetu tukiwa ndani ya
Baraza na hata katika majimbo yao.
9. Mheshimiwa Spika, napenda kuwapongeza Katibu Mkuu
na Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kwa mashirikiano
makubwa wanayonipa katika utekelezaji wa majukumu ya Ofisi yetu. Vilevile,
napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Wakurugenzi pamoja na wafanyakazi
wote wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kwa juhudi, bidii na ustahamilivu
katika kutekeleza majukumu yao ya kazi na kuleta ufanisi na tija kwa Taifa.
10. Mheshimiwa Spika, kwa namna
ya pekee napenda kuishukuru
familia yangu kwa ustahamilivu wao na msaada mkubwa wanaonipa katika kunijengea
utulivu ili niweze kutekeleza majukumu
yangu, nawaombea heri na baraka katika maisha yao.
11. Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Ofisi ya Makamu wa
Kwanza wa Rais napenda kutoa mkono wa
pole kwa ndugu na jamaa wa marehemu na kwa wale wote waliookolewa au kupoteza mali zao katika ajali ya meli ya
MV. Spice Islander iliyotokea tarehe 11/09/2011. Tutaendelea kuzikumbuka roho
za ndugu zetu waliotangulia mbele ya haki. Mwenyezi Mungu azilaze roho za Marehemu
mahala pema peponi Amin.
12. Mheshimiwa Spika, vile vile kwa niaba ya Ofisi ya
Makamu wa Kwanza wa Rais napenda kutoa mkono wa pole kwa familia pamoja na
wananchi wa Jimbo la Uzini na Bububu kwa kuwapoteza wawakilishi wao wapendwa,
marehemu Mussa Khamis Silima Mwakilishi wa Jimbo la Uzini na Salum Amour
Mtondoo Mwakilishi wa Jimbo la Bububu, tutawakumbuka kwa michango yao mikubwa
katika kuleta maendeleo ya nchi yetu. Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu
mahala pema peponi Amin.
MALENGO MAKUU YA OFISI YA MAKAMU WA KWANZA WA RAIS
13. Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa
Rais ina jukumu la kusimamia na kuratibu masuala ya mazingira, watu wenye
ulemavu, udhibiti wa dawa za kulevya na UKIMWI. Malengo makuu ya Ofisi ya
Makamu wa Kwanza wa Rais ni :
1.
Kuimarisha
na kutetea uzingatiaji wa haki za binaadamu na fursa sawa kwa watu wenye
ulemavu katika jamii.
2.
Kuongoza,
kuratibu, kufuatilia na kutathmini muitiko wa kitaifa wa kupambana na UKIMWI.
3.
Kuimarisha
usimamizi wa mazingira na matumizi endelevu ya maliasili.
4.
Kuratibu
na kudhibiti usafirishaji na biashara haramu ya dawa za kulevya.
UTEKELEZAJI WA MALENGO YA OFISI YA MAKAMU WA KWANZA
WA RAIS KWA MWAKA 2011/12 NA MALENGO 2012/13
14. Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa
Rais imejipangia kutekeleza majukumu yake kupitia Idara na Tume zifuatazo.
1.
Ofisi
ya Faragha
2.
Idara
ya Mipango Sera na Utafiti
3.
Idara
ya Uendeshaji na Utumishi
4.
Idara
ya Mazingira
5.
Idara
ya Watu Wenye Ulemavu
6.
Tume
ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya
7.
Tume
ya UKIMWI
8.
Ofisi
ya Makamu wa Kwanza wa Rais Pemba
UTEKELEZAJI WA MALENGO KWA MWAKA 2011/2012
OFISI YA FARAGHA
15. Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Faragha ina majukumu
ya kusimamia na kuratibu shughuli zote zinazofanywa na Makamu wa Kwanza wa
Rais.
16. Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Faragha kwa mwaka wa
fedha 2011/2012 ilijipangia malengo yafuatayo:-
- Kusimamia na kuratibu shughuli zote za Makamu wa Kwanza wa Rais.
- Kukuza na kuimarisha mawasiliano ya habari za Makamu wa Kwanza wa Rais.
- Kuimarisha huduma na mazingira mazuri ya utendaji kazi ofisini na nyumbani kwa Makamu wa Kwanza wa Rais.
17. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Aprili 2011/2012
Ofisi ya Faragha imeweza kutekeleza yafuatayo katika malengo iliyojipangia:-
18. Mheshimiwa Spika, katika kuratibu shughuli za
Makamu wa Kwanza wa Rais, mambo mbalimbali yametekelezwa yakiwemo; kufanya
ziara za kikazi ndani na nje ya nchi na kuandaliwa ripoti ambazo zimewasilishwa
Serikalini. Aidha, vikao teule 19 vilivyojadili mada mbalimbali zikiwemo
masuala ya kilimo, uvuvi, dawa za kulevya n.k. vimefanyika.
19. Mheshimiwa Spika, Miongoni mwa ziara za ndani ni
pamoja na kutembelea Wizara ya Kilimo na Maliasili, Wizara ya Habari,
Utamaduni, Utalii na Michezo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Miundombinu
na Mawasiliano pamoja na Idara na Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Makamu wa
Kwanza wa Rais. Pia ziara ya kufanya ukaguzi wa baadhi ya maeneo yaliyoharibiwa
kimazingira kama vile, maeneo ya Uwanja wa Amani, njia kuu zinazopita umeme
katika eneo la Kwarara, Uwandani, Kiwani, Wingwi n.k.
Aidha Mheshimiwa Makamu wa Kwanza wa
Rais amefanya ziara katika Mikoa mitatu ya Tanzania Bara ikiwemo Tabora, Lindi
na Dar es Salam ambapo alipata fursa ya kushiriki katika shughuli mbali mbali
za kijamii, kuzindua na kuweka mawe ya msingi katika miradi mbali mbali ya
kimaendeleo.
20. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2011/2012
Mheshimiwa Makamu wa Kwanza wa Rais alifanya ziara moja ya kikazi nchini India.
Katika ziara hiyo, Mheshimiwa Makamu wa Kwanza alipata fursa ya kutembelea
majimbo ya Hyderabad, Karnataka (Bangalore) na Kerala. Mheshimiwa Makamu wa
Kwanza na ujumbe wake walipata fursa ya kukutana na Viongzi wa Serikali na
taasisi mbali mbali pamoja na wawekezaji katika majimbo hayo matatu.
21. Mheshimiwa Spika,
Zanzibar inatarajiwa kufaidika na ziara hii katika Nyanja mbali mbali zikiwemo,
teknolojia ya habari na mawasiliano, elimu, kilimo, biashara na uwekezaji.
Ufuatiliaji wa mafanikio ya ziara hii kwa pande zote mbili unaendelea vizuri.
22. Mheshimiwa Spika, zaidi ya wananchi 250 walifika
ofisini kwa Makamu wa Kwanza wa Rais kwa ajili ya kuwasilisha malalamiko yao
pamoja na kupatiwa ushauri na maelekezo katika kuyapatia ufumbuzi mambo
yanayowakabili. Aidha mabalozi 12 wanaoziwakilisha nchi zao pamoja na
wawakilishi wa mashirika tisa ya kimataifa
na ya kikanda walifika kwa Makamu kwa ajili ya kujitambulisha na kuzungumzia
mambo mbali mbali ya kimaendeleo pamoja na kuimarisha mashirikiano.
23. Mheshimiwa Spika, kuanzishwa kwa kitengo cha
habari katika Ofisi ya Faragha, kumepelekea kurahisisha upatikanaji wa taarifa
na matukio mbalimbali ambayo Makamu wa Kwanza wa Rais anayafanya. Kitengo
kimeweza kuanzisha mtandao wake wa kijamii “weblog” ambao unaojulikana kwa jina
la “Zanzibar ni njema” yenye anuani http://mkr1znz.wordpress.com.
Mtandao huo wa kijamii hurusha hewani habari na taarifa mbalimbali za
Mheshimiwa Makamu wa Kwanza wa Rais.
24. Mheshimiwa Spika, Kitengo cha habari katika Ofisi
ya Faragha pia kina mashirikiano na mawasiliano mazuri na vyombo vyengine mbali
mbali vikiwemo vile vinavyotumia mtandao ambavyo pia huchapisha habari na
matukio ya Mheshimiwa Makamu wa Kwanza wa Rais.
25. Mheshimiwa Spika, Jumla ya vipindi vitano
vimetayarishwa na kurushwa hewani kupitia TV na radio za Serikali na zile za
binafsi. Zaidi ya makala 15, zimeandikwa na kuchapishwa katika magazeti mbali
mbali na mitandao ya kijamii. Mikutano miwili na waandishi wa habari “Press
conference” imefanyika. (Tafadhali angalia kiambatanisho Nam. 1).
26. Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha mazingira
mazuri ya utendaji kazi ofisini na upatikanaji wa huduma nyumbani kwa Makamu wa
Kwanza wa Rais, samani na vitendea kazi mbalimbali vimenunuliwa.
27. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2011/2012
hadi kufikia Mei 2012 Ofisi ya Faragha imekwishatumia jumla ya Shilingi 99,100,000 kwa kuendeshea kazi.
MALENGO KWA MWAKA WA FEDHA 2012/2013
28. Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Faragha kwa mwaka wa
fedha 2012/13 imejipangia kutekeleza malengo yafuatayo:-
1.
Kusimamia
na kuratibu shughuli zote za Makamu wa Kwanza wa Rais.
2.
Kukuza
na kuimarisha mawasiliano ya habari za Makamu wa Kwanza wa Rais.
3.
Kuimarisha
mazingira ya kazi katika kuleta ufanisi.
4.
Kuimarisha
huduma za Makamu wa Kwanza wa Rais.
29. Mheshimiwa Spika, ili kutekeleza malengo
iliyojipangia, Ofisi ya Faragha kwa
mwaka fedha 2012/2013 inahitaji jumla ya Shilingi 511,324,000 kwa kazi za kawaida. Kati ya hizo T.Shs.
300,000,000 kwa kuendeshea kazi na T.Shs. 211,324,000 ni kwa ajili ya
mishahara.
IDARA YA MIPANGO SERA NA UTAFITI
30. Mheshimiwa Spika, Idara ya Mipango, Sera na Utafiti
ina majukumu ya kuandaa na kusimamia utekelezaji wa sera na mipango ya
maendeleo ya Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, kukusanya, kutunza takwimu,
ufuatiliaji na tathmini pamoja na kuratibu shughuli za utafiti kwa Idara zote zilizo chini ya Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais.
31. Mheshimiwa Spika, Idara ya Mipango, Sera na
Utafiti kwa mwaka wa fedha 2011/2012 ilijipangia malengo yafuatayo:-
1.
Kusimamia
na kuratibu shughuli zote za mipango, sera na utafiti katika Ofisi ya Makamu wa
Kwanza wa Rais.
2.
Kuweka
utaratibu utakaowezesha upatikanaji wa taarifa sahihi za shughuli za Ofisi ya
Makamu wa Kwanza wa Rais ndani na nje ya nchi kwa wepesi.
3.
Kuratibu
na kusimamia miradi ya maendeleo ya taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Makamu wa
Kwanza wa Rais kwa kushirikiana na Washirika wa Maendeleo.
4.
Kutafuta
rasilimali ambazo zitasaidia katika utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Makamu
wa Kwanza wa Rais.
32. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Mei 2012 Idara ya
Mipango, Sera na Utafiti imeweza kutekeleza yafuatayo katika malengo
iliyojipangia:-
33. Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza kazi zake za kawaida za kuratibu, Idara hii imeandaa
mipango ya utekelezaji, bajeti, pamoja na kuiwakilisha Ofisi katika
kamati za kitaalamu na vikao mbali mbali ili kuhakikisha masuala yaliyo
chini ya Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais yanazingatiwa katika mipango yote ya
maendeleo.
34. Mheshimiwa Spika, Idara ya Mipango imekamilisha
uandaaji wa tovuti ya Ofisi ya Makamu wa
Kwanza wa Rais kwa lengo la kutoa taarifa kiurahisi ndani na nje ya nchi,
tovuti hii inatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika kurahisisha mawasiliano
baina ya Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais na wadau wake (www.fvpo.go.tz).
35. Mheshimiwa Spika, Idara imeendelea kuratibu na
kusimamia utekelezaji wa miradi mitatu ya maendeleo ikiwemo mradi wa kuangamiza
kunguru weusi, mradi wa usimamizi wa maji machafu Msingini - Kichungwani Pemba
pamoja na mradi wa kuimarisha majengo ya viongozi.
36. Mheshimiwa Spika, Mradi wa Kuangamiza Kunguru
Weusi umeanza rasmi mwezi wa Machi 2012.
Lengo Kuu la Mradi huu ni kuua kunguru weusi waliopo hapa Zanzibar kwa
kutumia mitego na sumu. Aidha lengo la
mradi la mwaka 2011/2012 ni kuua kunguru 408,000. Mradi huu unatekelezwa kwa
pamoja kati ya Idara ya Mazingira na Idara ya Misitu na Maliasili
Zisizorejesheka. Fedha za utekelezaji wa
mradi huu zinatoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Finland
kupitia Jumuiya isiyokuwa ya Kiserikali ya Uhifadhi wa Wanyama pori ya Tanzania
(Wildlife Conservation Society – WCS).
37. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa mchango wa
Serikali, jumla ya Shillingi 50,000,000 zilipangwa kutumika na hadi kufikia
mwezi wa Mei 2012 Shillingi 35,000,000 sawa na asilimia 70 zimetolewa. Mambo yaliyofanyika kwa fedha hizo ni pamoja
na kutengeneza mitego 30 na kusambazwa maeneo mbalimbali (tafadhali angalia
kiambatanisho nam. 2), kununua sumu ya kuulia kunguru kilo mbili kutoka New
Zealand, kununua vifaa mbalimbali vikiwemo mabesini, ndoo, sinia, vijiko,
glavu, mapanga na majembe pamoja na kununua chambo cha kutumika kwenye sumu na
mitego.
38. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi wa Mei 2012
jumla ya kunguru 11,596 wameshauliwa. Idadi hiyo ni ndogo kwa mujibu wa kiwango
cha mwaka kilichowekwa, hii imetokana na kuchelewa kupatikana kwa fedha na muda
mkubwa ulitumika kutengeneza mitego pamoja na kuagizishia sumu kutoka nje ya
nchi.
39. Mheshimiwa Spika, mradi wa ujenzi wa mtaro wa
maji machafu Msingini na Kichungwani ulizinduliwa rasmi Julai 2009. Mradi
unatekelezwa kwa pamoja kati ya Serikali kupitia Idara ya Mazingira na wananchi
wa Shehia za Msingini na Kichungwani zilizopo katika Wilaya ya Chake Chake,
Mkoa wa Kusini Pemba kupitia mradi wa TASAF. Lengo kuu la mradi huu ni kulinda
na kusimamia mazingira ya baharini na ukanda wa pwani wa magharibi ya bahari ya
hindi kutokana na shughuli mbali mbali zinazofanywa kutoka nchi kavu ambazo zinasababisha
uchafuzi wa mazingira. Jumla ya shilingi 440,000,000 zilitolewa na UNEP pamoja
na Aqua- 4 All kwa ajili ya vifaa na kazi za mradi huu. Aidha jamii kupitia
TASAF ilichangia jumla ya shillingi 69,000,000.
40. Mheshimiwa Spika, Shughuli kubwa za mradi huu
ambazo zimefanyika ni pamoja na ujenzi na ukarabati wa mtaro wa maji ya mvua
wenye urefu wa mita 1,610, ulazaji wa mabomba ya kupitishia maji machafu na
ujenzi wa mabwawa matatu ya kukusanyia na kusafishia maji machafu. Kazi kubwa
zilizobakia kukamilisha mradi huu ni uwekaji wa kokoto kwenye mabwawa hayo na
matengenezo ya mtaro wa zamani wa maji ya mvua. Mkandarasi wa kutoa huduma za
usambazaji wa kokoto, mchanga na saruji kwa ajili ya kumalizia kazi hizo
ameshapatikana na anatarajiwa kuanza kazi hivi karibuni.
41. Mheshimiwa Spika, mradi huu ulitarajiwa
kukamilika tarehe 31 Machi 2011, lakini kutokana na ucheleweshwaji wa
upatikanaji wa fedha kutoka UNEP, pamoja na ugumu uliojitokeza wakati wa mvua
wa kufikisha vifaa vya kazi katika eneo lililochimbwa mabwawa umesababisha
mradi huu kutomalizika kwa wakati uliopangwa.
42. Mheshimiwa Spika, katika utekelezaji wa mradi wa
kuimarisha nyumba za viongozi wa kitaifa, ununuzi wa vifaa na marekebisho ya
makaazi mapya ya Makamu wa Kwanza wa Rais yamefanyika.
43. Mheshimiwa Spika, Idara ya Mipango iliendelea na juhudi zake za
kutafuta rasilimali za kusaidia katika
utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya
Makamu wa Kwanza wa Rais, kwa kuandika pendekezo la mradi wa kujenga uwezo kwa
Ofisi na kuiwasilisha UNDP hali ambayo imepelekea kufanikiwa kuingizwa katika
mradi wa miaka minne wa UNDAP. Aidha pendekezo jengine la mradi wa kujenga
uwezo limeandikwa na kuwasilishwa Benki ya Dunia.
44. Mheshimiwa Spika, Idara ya Mipango,Sera na
Utafiti kwa mwaka wa fedha 2011/2012
ilikadiriwa kutumia Shilingi 170,010,000
kati ya hizo Shilingi 15,000,000 kwa
kuendeshea kazi na Shilingi 155,000,000
kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Hadi kufikia Mei 2012 Idara
ilikwisha ingiziwa shilingi 15,000,000
sawa na asilimia100 kwa kazi za
kawaida na Shilingi 140,000,000 sawa na asilimia 90 kwa kazi za maendeleo.
MALENGO KWA
MWAKA WA FEDHA 2012/2013
45. Mheshimiwa Spika, Idara ya Mipango, Sera na Utafiti
kwa mwaka wa fedha 2012/13 imejipangia kutekeleza malengo yafuatayo:-
- Kusimamia, kuratibu na kuandaa, shughuli zote za mipango, sera, utafiti pamoja na ufuatiliaji na tathmini kwa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais.
- Kuratibu na kusimamia utekelezaji wa shughuli mtambuka (UKIMWI, dawa za kulevya, jinsia, mazingira, watu wenye ulemavu, utawala bora na idadi ya watu)
- Kuimarisha mazingira ya kazi na kujenga uwezo wa watendaji
46. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Miradi ya
Maendeleo Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais inatarajia kutekeleza miradi mitano
(5) kwa kupitia fedha za Serikali na mradi mmoja kwa fedha za wahisani. Miradi
yenyewe ni:-
a)
Mradi
wa kuendeleza elimu ya mazingira
b)
Mradi
wa majaribio wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi
c)
Mradi
wa kuangamiza kunguru weusi
d)
Mradi
wa kuingiza masuala ya watu wenye ulemavu katika mipango ya maendeleo
e)
Mradi
wa kujenga kituo cha Tiba na
Marekebisho ya Tabia kwa watumiaji wa dawa za kulevya huko Tunguu
(Construction of Treatment and Rehabilitation Center)
f)
Na
mradi wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi ambao utatumia fedha za wahisani.
47. Mheshimiwa Spika, ili kutekeleza malengo
iliyojipangia Idara ya Mipango, Sera na Utafiti kwa mwaka wa fedha 2012/2013
inatarajia kutumia jumla ya Shilingi 176,251,000 kwa kazi za kawaida. ambapo
T.Shs. 115,000,000 kwa ajili ya kuendeshea kazi na T.Shs. 61,251,000 kwa ajili ya mishahara. Idara pia
inatarajia kutumia jumla ya Shilingi 255,000,000 kwa kazi za maendeleo ikiwa ni
mchango wa serikali. Aidha Idara inatarajia kutumia jumla ya Shilingi
705,600,000 kutoka kwa wahisani. Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais inaendelea
kuwasiliana na Washirika wa Maendeleo kuhusu ongezeko la Fedha hizi za Mchango
wa Wahisani katika Miradi ya Kimaendeleo.
IDARA YA UENDESHAJI NA UTUMISHI
48. Mheshimiwa Spika, Idara hii ina majukumu ya
kusimamia rasilimali watu pamoja na undeshaji wa kazi za kila siku za Ofisi ya
Makamu wa Kwanza wa Rais. Katika kutekeleza majukumu hayo inasimamia utawala,
ajira, maslahi na maendeleo ya watumishi pamoja na sheria, kanuni na taratibu
za utumishi. Pia inasimamia masuala ya nidhamu, uwajibikaji, mafunzo na mafao
ya wafanyakazi wanaostaafu.
49. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2011/2012
Idara ilijipangia malengo yafuatayo:
1.
Kuimarisha
mazingira mazuri ya utendaji kazi.
2.
Kukuza
uwezo wa wafanyakazi na viongozi na kuwapatia maslahi
3.
Kukuza
na kuimarisha mawasiliano ya habari.
4.
Kuimarisha
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais.
5.
Kuimarisha
huduma za usafiri katika Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais.
6.
Kuratibu
safari za kikazi nje na ndani ya nchi.
50. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Mei, 2012 Idara ya
Uendeshaji na Utumishi imeweza kutekeleza majukumu yafuatayo:
51. Mheshimiwa Spika, Idara imeendelea na jitihada zake
katika kuhakikisha kuwepo kwa mazingira mazuri ya kazi kwa kuwapatia
wafanyakazi vifaa mbali mbali vikiwemo samani za Ofisi na vitendea kazi. Hatua hiyo imetoa mwelekeo mzuri wa ufanisi
hasa katika utekelezaji wa majukumu ya kazi.
52. Mheshimiwa Spika, Idara ya Uendeshaji na
Utumishi imeweza kuwapatia maposho
wafanyakazi wanaostahiki na kufanya malipo ya fedha za likizo kwa wafanyakazi
18 waliokwenda likizo.
53. Mheshimiwa Spika, Idara imeendelea kuwapatia
mafunzo wafanyakazi ili kuleta ufanisi katika utendaji. Mfanyakazi mmoja
anaendelea na mafunzo ya muda mrefu, watatu wamepatiwa mafunzo ya muda mfupi na
wafanyakazi wawili wameweza kusaidiwa baadhi ya gharama za mafunzo kama vile
usafiri na vifaa vya kuandikia. (Tafadhali angalia kiambatanisho Nam. 3)
54. Mheshimiwa Spika, Idara kupitia Kitengo cha Habari
na Mawasiliano kwa kushirikiana na taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Makamu wa
Kwanza wa Rais imeendelea kushajihisha wananchi na kutoa elimu ya mazingira,
dawa za kulevya, UKIMWI na masuala ya watu wenye ulemavu kupitia Televisheni,
Radio na Magazeti. (Tafadhali angalia kiambatanisho Nam. 4)
55. Mheshimiwa Spika, Idara imefanya matengenezo
makubwa ya jengo la Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais ili liweze kuwa na hadhi
inayolingana na Ofisi hii. Miongoni mwa matengenezo hayo ni pamoja na
kubadilisha mfumo wa maji machafu na safi, kubadilisha sehemu za mikingo ya
vigae vya paa, kupaka rangi na kujenga sehemu ya kupokelea wageni.
56. Mheshimiwa Spika, Idara imeweza kuhudumia
safari sita za nje na kumi na saba za
ndani kwa viongozi na watendaji katika kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, safari hizo zimewawezesha kuhudhuria
shughuli mbali mbali za kazi na mikutano ambayo imepelekea kuimarisha utendaji
kazi, mahusiano na kubadilishana uzoefu.
57. Mheshimiwa Spika, Idara ya Uendeshaji na Utumishi
kwa mwaka wa Fedha 2011/2012 imekadiria kutumia jumla ya shilingi 704,204,000
kwa kazi za kawaida. Kati ya hizo T.Shs. 388,770,000 kwa ajili ya kuendeshea
kazi na T.Shs. 315,434,000 kwa ajili ya mishahara. Hadi kufikia Mei, 2012
ilikwisha kuingiziwa kiasi cha Shilingi 745,545,197 sawa na Asilimia 106. kati ya hizo shilingi 299,725,000 sawa na
asilimia 77 kwa ajili ya kuendeshea kazi Shilingi 445,820,197 sawa na asilimia
141 kwa ajili ya mishahara. (Ongezeko hili limetokana na kuongezeka kwa
mishahara)
MALENGO KWA MWAKA WA FEDHA 2012/2013
58. Mheshimiwa Spika, Idara ya Uendeshaji na
Utumishi imepanga kutekeleza malengo yafuatayo:-
- Kusimamia majukumu na utendaji wa wafanyakazi.
- Kuimarisha mazingira ya utendaji kazi.
- Kuwajengea uwezo wafanyakazi na kuwapatia maslahi.
- Kukuza na kuimarisha mawasiliano ya habari
- Kusimamia utaratibu wa udhibiti wa matumizi ya fedha.
59. Mheshimiwa Spika, Idara ya Uendeshaji na Utumishi
ili iweze kutekeleza malengo iliyojipangia kwa mwaka wa fedha 2012/2013
inatarajia kutumia jumla ya Shilingi 616,444,000 kwa kazi za kawaida. Kati ya
hizo T.Shs.254,749,00 kwa kuendeshea
kazi na T.Shs. 361,695,000 kwa ajili ya
mishahara.
IDARA YA MAZINGIRA
60. Mheshimiwa Spika, majukumu makuu ya Idara ya
Mazingira kwa mujibu wa Sera ya Mazingira ni kukusanya na kuhifadhi taarifa za
kimazingira, kutoa taarifa za kimazingira ili ziweze kusaidia katika
kutayarisha na kutekeleza mipango na miradi ya kimaendeleo, kufuatilia mwenendo
wa hali ya kimazingira, kukabiliana na matatizo ya kimazingira, kuhamasisha
wadau kuchukua hatua za kuhifadhi mazingira pamoja na kutoa elimu ya mazingira
kwa jamii.
61. Mheshimiwa Spika, Idara ya Mazingira kwa mwaka wa
fedha 2011/2012 ilikuwa na malengo yafuatayo:-
1.
Kuongeza uelewa wa elimu ya mazingira kwa jamii na
wadau wengine.
2.
Kuhakikisha
kwamba miradi ya maendeleo inazingatia vigezo vya utunzaji wa mazingira.
3.
Kudhibiti
uingizaji wa bidhaa chakavu zinazoharibu na kuchafua mazingira.
4.
Kuendelea
kuzuia uingizwaji na matumizi ya mifuko ya plasitiki.
5.
Kuandaa Mpango
Mkakati wa utekelezaji wa Sera mpya ya Mazingira.
6.
Kutekeleza
mradi wa kuangamiza kunguru weusi hapa Zanzibar.
7.
Kuandaa
mkakati wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi (climate change strategy).
8.
Kuweka
utaratibu mzuri wa uvunaji wa maliasili zisizorejesheka.
62. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Mei 2012 Idara ya
Mazingira imeweza kutekeleza yafuatayo
katika malengo iliyojipangia:-
63. Mheshimiwa Spika, Idara imeweza kutoa matangazo juu
ya marufuku ya mifuko ya plastiki kwa siku za sikukuu kupitia Redio za ZBC, Hit
FM na Zenji FM, pamoja na Televisheni za ZBC na Zanzibar Cable. Vipindi 9 vya redio na vipindi 3 vya TV
vinavyohusu usimamizi wa mazingira vimerushwa hewani (Tafadhali rejea
kiambatanisho Nam. 4). Filamu fundishi (documentaries) tatu kuhusu athari za
mifuko ya plastiki, uchimbaji holela wa mchanga, na bidhaa chakavu za umeme na
elektroniki ziliandaliwa. Semina kumi
juu ya athari na udhibiti wa mifuko ya plastiki na uchafuzi wa mazingira
zimefanywa skuli zote za msingi za Unguja na Pemba ambazo zina vilabu vya
mazingira. Jumla ya skuli 146 (90 Unguja 56 Pemba) na wanafunzi 292 (180 Unguja
112 Pemba) walishiriki semina hizo. Mkakati wa mawasiliano kwa ajili ya elimu
ya mazingira umetayarishwa. Aidha, Idara
ilifanya mikutano mitano ya jamii huko Pemba katika maeneo ya Uwandani,
Kangagani na Muwambe na kuwahusisha wanajamii 157 (wanawake 30, wanaume 127). Mikutano hiyo imepelekea kuundwa kwa kamati
za jamii za usimamizi wenye uwiano wa ukanda wa pwani (Integrated Coastal Zone
Management Committees – ICZM).
64. Mheshimiwa Spika, Idara ya Mazingira imefanya
semina ya siku tatu kwa Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako tukufu na wewe
mwenyewe Mheshimiwa Spika ulitupa heshima ya kuiongoza semina hiyo. Semina hiyo
iliyohusu masuala mbalimbali ya mabadiliko ya tabianchi ilikuwa na lengo la
kuwapa uelewa wa mabadiliko ya tabianchi na mwelekeo wa Zanzibar katika
kusimamia suala hilo. Sambamba na hayo
wafanyakazi 12 waliwezeshwa kufanya ziara ya kimasomo mjini Moshi na Arusha
kujifunza na kupata uzoefu juu ya usimamizi wa taka, wafanyakazi hao ni kutoka
Idara ya Mazingira, Manispaa, Halmashauri ya Wilaya ya Magharibi, Mabaraza ya
Miji ya Chake Chake, Wete na Mkoani, Jumuiya ya Wakulima, Wafanyabiashara na
Wenye Viwanda pamoja na jumuiya zisizokuwa za kiserikali ambazo zimewakilishwa
na jumuiya ya CODECOZ.Aidha viongozi 10 wa Kamati ya machimbo ya Uwandani
walishiriki ziara ya kimasomo Mjini Mombasa nchini Kenya kwa lengo la kujifunza
namna bora ya shughuli za uchimbaji na urejeshwaji wa maeneo yaliyochimbwa.
65. Mheshimiwa
Spika,
katika kujenga uwezo wa kiutendaji Idara
ya Mazingira ili kuweza kutekeleza majukumu ya kutoa elimu ya mazingira na
kufanya tathmini ya athari za kimazingira, jumla ya wafanyakazi sita wamepatiwa
mafunzo ya muda mfupi kuhusu uandishi wa habari na tathmini ya athari za
kimazingira. Aidha, wafanyakazi wawili
wamepatiwa mafunzo ya muda mrefu katika fani ya Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano
( ICT) na
Uandishi wa habari. Wafanyakazi watatu wamelipiwa gharama za masomo kwa ngazi
ya cheti katika fani za kilimo,
usimamizi wa kumbukumbu na Usimamizi rasilimali watu. .
66. Mheshimiwa Spika, Idara imefanyia mapitio ripoti
12 za Tathmini za Athari za Kimazingira na Kijamii na kutoa vyeti vya mazingira
kwa taasisi husika kwa hatua za utekelezaji. (Tafadhali angalia kiambatanisho
Nam. 5). Jumla ya miradi ya hoteli 110 (80 Unguja na
30 Pemba) imefanyiwa ufuatiliaji katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar ili
kuona namna inavyozingatia masuala ya kimazingira katika uendeshaji wa shughuli
zao (Tafadhali angalia kiambatanisho Nam. 6). Katika ufuatiliaji huo, miradi
iliyoonekana na kasoro za kimazingira ilitakiwa kuondoa kasoro hizo ikiwa ni
pamoja na kufanya ukaguzi wa kimazingira. (Environmental audit).
67. Mheshimiwa Spika, miradi ambayo imejenga ndani ya
mita 30 kuanzia alama inayofikiwa na maji ya bahari yanapojaa (high water mark)
imetakiwa kubomoa sehemu ambayo imejengwa ndani ya eneo hilo. Hadi sasa ni mradi mmoja tu wa Zanzibar Ocean
View ndio umeripoti kutekeleza amri hiyo.
Kwa miradi ambayo imekaidi amri hiyo majina ya miradi hiyo
yamewasilishwa Idara ya Mipango Miji na Vijiji kwa hatua za kisheria kwa mujibu
wa Kanuni ya kudhibiti matumizi ya ardhi kwa ajili ya uekezaji ya mwaka 2006
(Tafadhali angalia kiambatanisho Nam. 7). Sambamba na utekelezaji huo, Kanuni ya kufanya tathmini ya athari za
kimazingira (Environemntal Impact and Social Assessment – EISA Regulations)
imefanyiwa mapitio.
68. Mheshimiwa
Spika, rasimu ya kanuni ya kupiga marufuku uingizwaji wa
bidhaa chakavu za umeme na elektroniki (e-waste) nchini imeandaliwa kwa
kuwashirikisha wadau husika. Hata hivyo, baada ya kanuni hiyo kupitiwa na Kamati
ya Uongozi ya Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais na wadau wengine imeonekana ipo haja ya kuandaa viwango vya
bidhaa zitakazoruhusiwa kuingizwa nchini badala ya kupiga marufuku ya moja kwa
moja kuingiza bidhaa hizo. Idara inaendelea kushauriana na Wizara ya Biashara,
Viwanda na Masoko ili kuweka viwango vinavyohitajika vya bidhaa hizo chakavu.
69. Mheshimiwa
Spika, kanuni ya kusimamia marufuku ya mifuko ya plastiki imefanyiwa
marekebisho yaliyohitajika. Kufuatia
marekebisho hayo, matangazo kwa njia ya gari yametolewa kwa mikoa mitano ya
Zanzibar. Aidha, operesheni za kila siku
zimefanyika ambazo zinasimamiwa na mkuu wa operesheni wa Jeshi la Polisi
Zanzibar. Kwenye operesheni hizo hadi kufikia mwezi wa Mei 2012 jumla ya watu 192 (5 wanawake na 187 wanaume)
wamekamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria na kutozwa faini jumla ya
shilingi 7,650,000 (shilingi 6,350,000.Unguja na 1,300,000 Pemba). Fedha zote
hizo zimeingizwa kwenye mfuko mkuu wa Serikali kupitia Mahakama husika. Aidha
mafanikio makubwa yaliyopatikana kwenye operesheni hizo ni kupungua kwa kiwango
kikubwa cha matumizi ya mifuko ya plastiki pamoja na kupungua kuzagaa kwa
mifuko hiyo kwenye maeneo mbali mbali ya Zanzibar.
70. Mheshimiwa
Spika, rasimu ya Mpango Mkakati wa utekelezaji wa Sera mpya
ya Mazingira imeandaliwa. Hata hivyo,
kukamilika kwa uandaaji wa Mpango Mkakati huo unategemea kukamilika kwa Sera
mpya ya Mazingira ambayo itajadiliwa katika kikao cha Makatibu wakuu hivi
karibuni. Sera hiyo imechelewa kukamilika kutokana na umuhimu wa kuingiza mambo
mengine mapya ya kimazingira yakiwemo ya mabadiliko ya tabianchi ambayo utafiti
wake ulikuwa haujakamilika.
71. Mheshimiwa Spika, katika hatua za kuandaa mkakati
wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, utafiti juu ya athari za kiuchumi
zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi umefanyika na ripoti yake imewasilishwa
Serikalini baada ya kujadiliwa na wadau.
Kufuatia kupatikana kwa taarifa hizo, tayari hatua za kumpata mshauri
mwelekezi wa kuandaa Mkakati huo zimeshaanza.
Katika hatua nyengine, maeneo 148 yanayoingia maji ya chumvi Unguja na
Pemba yameorodheshwa, kati ya hayo 25 yapo Unguja na 123 yapo Pemba (Tafadhali angalia kiambatanisho Nam. 8). Aidha kamati za uongozi na kitaalamu
za kusimamia masuala ya mabadiliko ya tabianchi kwa Zanzibar zimeanzishwa.
Kamati ya uongozi ina wajumbe 10 ambao ni Makatibu wakuu na kamati ya kitaalamu
ina wajumbe 23 katika ngazi ya Wakurugenzi na Viongozi wa taasisi zisizo za
kiserikali.
72. Mheshimiwa
Spika, rasimu ya kanuni juu ya uchukuaji wa maliasili
zisizorejesheka imeandaliwa na kujadiliwa na wadau mbalimbali. Hivi sasa Ofisi
ya Makamu wa Kwanza wa Rais inaendelea
kuyafanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali kabla ya kuchapishwa na kuanza utekelezaji. Sambamba na kanuni hiyo, Ofisi ya Makamu wa
Kwanza wa Rais pia inaendelea na taratibu za kuandaa kanuni ya usimamizi wenye
uwiano wa ukanda wa pwani (Integrated Coastal Zone Management {ICZM}
Regulations).
73. Mheshimiwa Spika, kutokana na kuwepo athari za
mabadiliko ya tabianchi, Idara ya Mazingira ilibahatika kupata fedha za
wahisani za kutekeleza mradi wa majaribio wa kukabiliana na mabadiliko ya
tabianchi kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano
wa Tanzania. Kupitia mradi huu, Idara ya
Mazingira ilipata jumla ya Shilingi 539,414,800 ili kutekeleza kazi mbalimbali
za mradi huo wenye lengo la kufanikisha upatikanaji wa maji yasiyokuwa na
chumvi kwa Wananchi wa Shehia ya Nungwi, Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa
Kaskazini Unguja.
74. Mheshimiwa Spika, kazi ambazo kwa sasa zimetekelezwa ni pamoja na kuchimba kisima katika
eneo la Shehia Kilimani chenye uwezo wa kuzalisha maji lita 30,000 kwa saa,
kuchimba msingi wa Kilomita 7.5 kutoka eneo la kisima hadi Nungwi, kununua
mabomba na kuyalaza katika msingi uliochimbwa, kujenga kibanda cha pampu ya
maji, kununua na kufunga pampu ya maji.
Aidha, kazi zinazoendelea ni kufunga tangi jipya lililonunuliwa kutoka
Uingereza lenye uwezo wa kuhifadhi lita 150,000, kununua na kufunga transfoma pamoja na kuunga
umeme kwenye kibanda cha pampu ya maji.
Hivi sasa mradi huu uko katika hatua za mwisho za kukamilika.
75. Mheshimiwa Spika, Idara ya Mazingira kwa mwaka wa
fedha 2011/2012 ilikadiriwa kutumia Shilingi 239,158,000 kwa kazi za kawaida, hadi kufikia Mei 2012 ilikwisha ingiziwa shilingi 261,426,046 sawa na asilimia 109.3 kati ya hizo shilingi 66,680,000 sawa na
asilimia 66 kwa ajili ya kuendeshea kazi na Shilingi 194,746,046 sawa na
asilimia 144 kwa ajili ya mishahara. Aidha katika kufanikisha kazi
zilizotekelezwa jumla ya shilingi 118,105,066 zilitumika kutoka mradi wa MACEMP
na SMOLE.
76. Mheshimiwa
spika, Idara ya Mazingira kwa mwaka wa fedha 2011/2012,
ilipangiwa kukusanya jumla ya shillingi 9,000,000. Aidha makusanyo hayo
yamegawika katika sehemu mbili ikiwa ni
pamoja na ada ya hifadhi ya mazingira ambayo ilipangiwa jumla ya shilingi
4,000,000 na ada ya ukaguzi wa mazingira yenye jumla ya shilingi 5,000,000. Kwa
mwaka huu, Idara ya Mazingira ilihusika na ukusanyaji wa ada ya hifadhi ya
mazingira pekee kwa kuwa ada ya ukaguzi wa mazingira imehamishiwa kamisheni ya
Utalii. Ada hii imehamishiwa kwenye taasisi hiyo kwa kuwa ilihusika na fomu za
maombi ya leseni za biashara za Utalii ambazo hupitia kwenye taasisi mbali
mbali kuridhia utoaji wa leseni hizo. Kwenye kifungu cha ada ya hifadhi ya
mazingira hadi kufikia mwezi wa Mei 2012, Idara ya Mazingira imeweza kukusanya Shilingi 5,978,000 sawa na
asilimia 149 ya kifungu hicho.
MALENGO KWA MWAKA 2012/2013
77. Mheshimiwa Spika, Idara ya Mazingira kwa mwaka wa
fedha 2012/13 imejipangia kutekeleza malengo yafuatayo:-
1.
Kudhibiti
uchafuzi wa mazingira.
2.
Kusimamia
uingizwaji wa masuala ya mazingira katika miradi ya maendeleo.
3.
Kuongeza
uwezo na kuimarisha muundo wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
4.
Kuimarisha
usimamizi endelevu wa maliasili.
5.
Kuongeza
uelewa wa elimu ya mazingira kwa jamii na wadau wengine.
6.
Kuimarisha
utekelezaji wa Sera, Sheria na Kanuni za mazingira.
7.
Kuimarisha
mazingira ya kazi na kuwajengea uwezo wafanyakazi.
78. Mheshimiwa Spika, ili kutekeleza malengo
iliyojipangia Idara ya Mazingira kwa mwaka wa fedha 2012/2013 inatarajia
kutumia jumla ya Shillingi 369,369,000 kwa kazi za kawaida. Kati ya hizo
shilingi 112,373,000 ni kwaajili ya kuendeshea kazi na shilingi 257,296,000 ni
kwaajili ya mishahara
79. Mheshimiwa
Spika, Idara ya Mazingira kwa mwaka wa fedha 2012/2013,
imepangiwa kukusanya jumla ya shillingi 10,800,000.00 ambazo zitatokana na ada
ya hifadhi ya mazingira ikwa ni pamoja na vyeti vya Mazingira.
IDARA YA WATU WENYE ULEMAVU
80. Mheshimiwa Spika, Idara ya Watu Wenye Ulemavu ina
majukumu ya kuratibu masuala mbali mbali ya watu wenye ulemavu, pia inafanya
kazi na Baraza la Taifa la Watu wenye Ulemavu ambalo linaishauri Serikali
kuhusu maendeleo ya watu wenye ulemavu kwa mujibu wa Sheria No. 9 ya mwaka
2006.
81. Mheshimiwa Spika, Idara ya Watu Wenye Ulemavu kwa
mwaka wa fedha 2011/2012 ilijipangia malengo yafuatayo:-
- Kuendeleza usajili wa Watu wenye Ulemavu kwa kupata taarifa zinazohitajika juu ya watu wenye ulemavu.
- Kuongeza uelewa wa jamii juu ya Sera, Sheria na Mikataba ya Kimataifa ya haki za watu wenye ulemavu.
- Kujenga uwezo wa Idara, Baraza la Taifa la Watu wenye Ulemavu Zanzibar na Jumuiya za Watu wenye Ulemavu.
- Kuratibu Shughuli za Baraza la Taifa la Watu wenye Ulemavu Zanzibar.
82. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Mei 2012 Idara ya
Watu Wenye Ulemavu imeweza kutekeleza yafuatayo katika malengo iliyojipangia:-
83. Mheshimiwa Spika, katika kuendeleza usajili wa Watu
Wenye Ulemavu, Idara imeweza kusajili watu wenye ulemavu katika mikoa yote
miwili ya Pemba. Jumla ya watu 6,445 wenye ulemavu tofauti wamesajiliwa. Kati
ya hao wanaume 3,556 na wanawake 2,878. (Tafadhali angalia kiambatanisho Nam.
9). Kabla ya kufanya usajili, mafunzo yalitolewa kwa masheha 121, wakusanyaji
taarifa 25 na wasimamizi wa usajili 4. Kwa ajili ya kushajihisha na kuwafichuwa
watu wenye ulemavu.
84. Mheshimiwa Spika, katika kuongeza uelewa wa jamii
juu ya Sera, Sheria na Mikataba ya Kimatafa ya Haki za Watu wenye Ulemavu,
Idara inaendelea kuifanyia mapitio Sheria ya Watu wenye Ulemavu. Vikao vitano
vya awali vimefanyika vya kupitia Sheria No. 9
ya mwaka 2006 ya watu wenye ulemavu
ambavyo viliwashirikisha wadau mbali mbali wa Unguja na Pemba.
85. Mheshimiwa Spika, katika kuhamasisha mambo mbali
mbali ya Watu wenye Ulemavu na kwenda sambamba na utekelezaji wa Mikataba ya
Kimataifa ya Watu Wenye Ulemavu, Idara imefanikiwa kuadhimisha siku ya
Kimataifa ya Watu wenye Ulemavu, tarehe 3/12/2011 katika kiwanja cha Mahonda
Wilaya ya Kaskazini “B”, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
86. Mheshimiwa
Spika, Idara
imefanikiwa kushawishi uanzishwaji wa maafisa waratibu wa masuala ya watu wenye
ulemavu ili kusaidia taasisi husika kuingiza masuala ya Watu wenye Ulemavu
katika mipango ya taasisi za Serikali. Jumla ya maafisa waratibu 16 tayari wapo
katika wizara zetu. Vile vile Idara ilitoa mafunzo juu ya uingizwaji wa masuala
ya watu wenye ulemavu kwa maafisa hao. Aidha Idara kwa kushirikiana na “Save
the Children” imetoa mafunzo juu ya haki na uhifadhi wa mtoto kwa watu 80
wakiwemo wazazi, walezi na watoto wenye ulemavu katika mikoa miwili ya Pemba.
Idara imeweza kuandaa vipindi 15 vya Radio na viwili vya TV kupitia Shirika la
Utangazaji la Zanzibar (ZBC), Zenji FM na Radio Istiqama Pemba. (Tafadhali
rejea kiambatanisho Nam. 4)
87. Mheshimiwa Spika, katika kujenga uwezo wa Idara na
Baraza la Taifa la Watu wenye Ulemavu, Idara imeweza kununua vifaa vya ofisini
kama vile samani za Ofisi na vifaa vya utendaji kwa wafanyakazi wake. Aidha
Idara imemlipia mafunzo mfanyakazi mmoja katika ngazi ya Diploma ya kompyuta.
88. Mheshimiwa Spika, kwa kutambua mchango wa Jumuiya
za Watu wenye Ulemavu katika suala zima la kutetea haki na kuhakikisha Jumuiya
za Watu wenye Ulemavu zinakuwa na nguvu kiutendaji na kiuwezo, Idara imeweza
kutoa ruzuku kwa Jumuiya tisa (9) za Watu wenye Ulemavu pamoja na kuwapatia visaidizi (viti vyenye
magurudumu mawili) watu 31 Unguja na
Pemba. (Tafadhali angalia kiambatanisho
Nam.10a na b)
89. Mheshimiwa Spika, katika kuratibu shughuli za
Baraza la Taifa la Watu wenye Ulemavu, Idara imefanya vikao vinne vya Baraza la
Taifa la Watu Wenye Ulemavu na kujadili mambo mbali mbali yanayohusu maendeleo
ya Watu wenye Ulemavu hapa Zanzibar.
90. Mheshimiwa Spika, Idara ya Watu Wenye Ulemavu kwa
mwaka wa fedha 2011/2012 ilikadiriwa kutumia Shilingi 177,995,000 kwa kazi za kawaida hadi kufikia Mei 2012 ilikwisha
ingiziwa shilingi 139,424,888 sawa
na asilimia 78.3 kati ya hizo shilingi 85,258,000 sawa na
asilimia 62 kwa ajili ya kuendeshea kazi Shilingi 54,166,888 sawa na asilimia
127 kwa ajili ya mishahara.
MALENGO KWA MWAKA WA FEDHA 2012/2013
91. Mheshimiwa Spika, Idara ya Watu Wenye Ulemavu kwa
mwaka wa fedha 2012/13 imejipangia kutekeleza malengo yafuatayo:-
- Kuratibu shughuli za Baraza la Taifa la Watu wenye Ulemavu.
- Kuwapatia visaidizi na kuimarisha juhudi za taasisi zinazoshughulikia masuala ya watu wenye ulemavu.
- Kuanzisha mfumo wa taarifa za Watu wenye Ulemavu.
- Kuandaa na kusimamia utekelezaji wa sera, sheria na kanuni za Watu wenye Ulemavu.
- Kuimarisha mazingira mazuri ya kazi na kujenga uwezo wa wafanyakazi katika kuleta ufanisi.
92. Mheshimiwa Spika, ili kutekeleza malengo
iliyojipangia Idara ya Watu Wenye Ulemavu kwa mwaka fedha 2012/2013 inatarajia
kutumia jumla ya Shilingi 532,562,000 kwa kazi za kawaida. kati ya hizo
96,992,000 ni mishahara na 435,570,000 ni matumizi ya kuendeshea kazi.
TUME
YA KURATIBU NA UDHIBITI WA DAWA ZA KULEVYA
93. Mheshimiwa Spika, Tume ya Kuratibu na Udhibiti wa
Dawa za Kulevya ina jukumu la kuratibu
mapambano dhidi ya matumizi, biashara na usafirishaji wa dawa za kulevya kwa kushirikiana na wadau mbali mbali, kutoa
taaluma kwa jamii juu ya athari ya dawa za kulevya na kutoa huduma za tiba
na ushauri nasaha kwa watumiaji wa dawa
za kulevya.
94. Mheshimiwa Spika, Kwa mwaka wa Fedha 2011/2012
Tume ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya ilijipangia malengo yafuatayo:-
1.
Kuwasilisha
mswaada wa marekebisho ya Sheria ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya Zanzibar katika
ngazi zinazo husika.
2.
Kuwajengea
uwezo watendaji wa Sekta ya Dawa za Kulevya.
3.
Kuendeleza
upigaji vita vya dawa za kulevya.
4.
Kuandaa
Sera ya Dawa za Kulevya.
5.
Kupunguza
maambukizi ya Virusi vya UKIMWI kwa watumiaji wa dawa za kulevya.
6.
Kuziendeleza
juhudi za Taasisi zisizo za kiserikali (NGOs) zinazotoa huduma za makaazi na
marekebisho kwa vijana wanaoacha matumizi ya dawa za kulevya (Sober Houses).
95. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Mei 2012 Tume ya
Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za kulevya imeweza kutekeleza yafuatayo katika
malengo iliyojipangia:-
96. Mheshimiwa Spika, Tume imeweza kufanya mapitio ya
Sheria Nam.9 ya mwaka 2009 ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya Zanzibar. Rasimu ya
Mswada wa Marekebisho ya Sheria hiyo ilipitiwa na wadau wa ngazi mbalimbali
kabla ya kupitishwa na Baraza lako tukufu.
97. Mheshimiwa Spika, ili kufanikisha shughuli za uhamasishaji na ufuatiliaji wa mambo
mbalimbali ya kikazi, jumla ya vespa nne (4) zimenunuliwa. Na kwa upande wa
kujenga uwezo wa watendaji, wafanyakazi watatu wameweza kupata mafunzo ya muda
mrefu juu ya dawa za kulevya ndani na nje ya nchi kwa ufadhili wa taasisi ya
“Center for Disease Control” ya Marekani, Serikali ya Australia na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar.
98. Mheshimiwa Spika, Tume iliweza kuandaa programu na
ziara za uhamasishaji upigaji vita dawa za kuleva kupitia vyombo vya habari na
kuzitembelea shehia mbalimbali za Unguja na Pemba. Jumla ya vipindi 41
vilirushwa hewani, vipindi 24 katika radio na 17 katika televisheni. Jumla ya
shehia 17 zilifanyiwa ziara za uhamasishaji na taaluma juu ya athari ya dawa za
kulevya, kati ya hizo tisa Unguja na nane Pemba zenye wastani wa watu 783.
Aidha wanafunzi 5,422 katika Skuli 28 walipatiwa taaluma hiyo. Kati yao
wasichana ni 2991 na wavulana 2431, wengi wao ni wenye umri kati ya miaka 12
hadi 18. Pia walimu 97 walifaidika na taaluma hiyo.
99. Mheshimiwa Spika, Tume kwa kushirikiana na taasisi
ya Umoja wa Mataifa ya Dawa za Kulevya na Uhalifu kanda ya Afrika Mashariki ( United Nations
Office on Drugs and Crime Regional
Office for Eastern Africa- UNODC-ROEA)
ilifanya semina maalum ya siku moja ya uhamasishaji upigaji vita
biashara na matumizi ya dawa za kulevya kwa wajumbe wa Baraza lako Tukufu. Pia kwa kutambua umuhimu wa taasisi za
kidini katika jamii, Tume kwa kushirikiana na taasisi ya “American
International Health Alliance” (AIHA) iliandaa semina juu ya dawa za kulevya
kwa mtandao wa taasisi za dini mbali mbali unaoratibiwa na Ofisi ya Mufti Unguja na Pemba. Jumla ya washiriki 84
walinufaika na mafunzo hayo. Lengo hasa ni kuwapa mwamko zaidi na kusaidia
kuendelea na juhudi zao za kila siku za kuwaasa vijana, waumini na jamii kwa
jumla juu ya athari ya dawa za kulevya.
100. Mheshimiwa Spika, Uandaaji wa Sera ya Dawa za
Kulevya haukuweza kukamilika kama ilivyotarajiwa kutokana na kuchelewa kupata
fedha zilizoahidiwa na wafadhili. Hata hivyo shughuli hiyo imeshaanza na imo
katika hatua za awali za ukusanyaji wa maoni ya wadau.
101. Mheshimiwa Spika, Tume kupitia kituo chake cha
ushauri nasaha kilichopo mtaa wa Sogea kiliweza kutoa huduma kwa jamii na
watumiaji wa dawa za kulevya wapatao 984 wakiwemo wanawake 510, na wanaume 474.
Kati ya hao 97 walikuwa ni watumiaji wa dawa za kulevya (wanaume 82 na wanawake
15). Aidha, watu tisa (9) kati yao waligundulika na virusi vya UKIMWI, (w/ke 4,
w/me 5). Kupitia huduma za kuwafikia wateja (outreach programme) katika maeneo
yao (maskani), jumla ya wateja 125 (wanawake 20, wanaume 105) waliweza kufikiwa
katika maeneo mbali mbali (Tafadhali angalia kiambatanisho Nam. 11).
102. Mheshimiwa Spika, Kwa kutambua mchango wa taasisi
zisizo za kiserikali katika suala zima la mapambano dhidi ya dawa za kulevya
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kupitia Tume ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa
za Kulevya ilizipatia jumla ya shillingi 9,900,000 nyumba tisa (9) za makaazi
ya vijana wanaoacha matumizi ya dawa za kulevya (Sober Houses) pamoja na seti
ya Televisheni na Radio Unguja na Pemba. Jumla ya vijana 501 walipata huduma
katika makaazi hayo. (Tafadhali angalia kiambatanisho Nam.12a, b na c)
103. Mheshimiwa Spika, Tume kwa kushirikiana na taasisi
ya AIHA iliweza kutoa mafunzo ya uongozi na uwekaji wa kumbukumbu za kifedha
kwa taasisi zinazotoa huduma za makaazi ya vijana wanaoacha matumizi ya dawa za
kulevya (Sober Houses) Unguja na Pemba. Jumla vijana 45 (wanawake 6, wanaume
39) walifaidika na mafunzo hayo. Aidha mafunzo ya programu ya upataji nafuu
(Recovery Oriented System of Care –ROSC) yalitolewa kwa wadau mbali mbali,
wakiwemo watendaji wa Mahakama, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Chuo
cha Mafunzo, jumla ya washiriki 75 kutoka Unguja na Pemba walifaidika na
mafunzo hayo.
104. Mheshimiwa Spika, Tume imekamilisha rasimu ya
muongozo wa nyumba za marekebisho za makaazi ya vijana wanaoacha matumizi ya
dawa za kulevya. Aidha, Tume iliweza kuandaa mkutano wa mapitio ya Katiba ya
Jumuiya ya vijana walioacha matumizi ya dawa za kulevya (Drug Free Zanzibar) na
kusimamia uchaguzi wa taasisi hiyo. Tume kupitia
programu yake ya Family Therapy imekuwa
ikikutana na wazee, familia na jamaa ili kubadilishana mawazo, kuwapa ushauri
na kuzungumzia mafanikio na changamoto mbali mbali. Mikutano minne na
wanafamilia iliyokuwa na wastani wa watu wapatao 3,022 ilifanyika.
105. Mheshimiwa Spika, Tume ya Kuratibu na Udhibiti wa
Dawa za Kulevya kwa mwaka wa fedha 2011/2012 ilikadiriwa kutumia shilingi 142,527,000 kwa kazi za kawaida, hadi
kufikia Mei 2012 ilikwisha ingiziwa shilingi 138,965,297 sawa na asilimia 97.5 kati ya hizo shilingi 62,200,000 sawa na asilimia 73 kwa ajili ya
kuendeshea kazi Shilingi 76,765,297 sawa na asilimia 134 kwa ajili ya
mishahara.
MALENGO KWA MWAKA WA FEDHA 2012/2013
106. Mheshimiwa Spika, Tume ya Kuratibu na Udhibiti wa
Dawa za Kulevya kwa mwaka wa fedha 2012/13 imejipangia kutekeleza malengo
yafuatayo;
1.
Kuratibu
na kuendeleza mapambano dhidi ya uingizaji na usafirishaji wa dawa za kulevya.
2.
Kuongeza
mwamko wa jamii juu ya athari na udhibiti wa dawa za kulevya.
3.
Kuimarisha
utoaji wa huduma za tiba kwa watumiaji wa dawa za kulevya.
4.
Kuanzisha
mfumo wa taarifa za dawa za kulevya.
5.
Kuratibu
na kuimarisha juhudi za taasisi katika kushughulikia mapambano dhidi ya dawa za
kulevya.
6.
Kuimarisha mazingira mazuri ya kazi katika
kuleta ufanisi.
107. Mheshimiwa Spika, Ili kutekeleza malengo
iliyojipangia Tume ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya inatarajia
kutumia jumla ya Shilingi 247,091,000
kwa kazi za kawaida. Kati ya hizo Shilingi 146,607,000 ni kwa ajili ya matumizi
ya kuendeshea kazi na Shilingi 100,684,000
ni kwa ajili ya mishahara.
OFISI KUU PEMBA
108. Mheshimiwa Spika, Ofisi Kuu Pemba
ina jukumu la kuratibu, kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa shughuli zote za
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kwa upande wa Pemba.
109. Mheshimiwa Spika, Ofisi Kuu Pemba kwa mwaka wa
fedha 2011/2012 ilijipangia malengo yafuatayo:-
- Kuratibu na Kusimamia utekelezaji wa shughuli zote za Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Pemba.
- Kuimarisha mazingira ya Utendaji kazi.
- Kujenga uwezo wa wafanyakazi.
110. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Mei
2012 Ofisi Kuu Pemba imeweza kutekeleza yafuatayo katika malengo iliyojipangia:-
111. Mheshimiwa Spika, Ofisi Kuu Pemba imeweza kuratibu
ziara mbali mbali za Viongozi zikiwemo ziara za Makamu wa Kwanza wa Rais, ziara
za Kamati ya Baraza la Wawakilishi ya kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa
Kitaifa na ziara za Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais. Pia Ofisi
Kuu Pemba iliratibu ziara ya Mwakilishi wa Idara ya Maendeleo ya Kimataifa ya
Uingereza (UK-Department for International Development -DFID) katika maeneo
yanayoendeleza juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Aidha, Ofisi
ilisimamia utekelezaji wa msaada uliotolewa kwa ajili ya kuendeleza huduma kwa
vijana wanaoendelea kupata nafuu
ya kujikinga na matumizi ya dawa
za kulevya katika nyumba za
kurekebisha tabia (Sober Houses). Mikutano ya operesheni ‘Mifuko ya Plastiki’
kwa Mikoa ya Kusini na Kaskazini Pemba nayo pia iliratibiwa.
112.
Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kuimarisha mazingira ya utendaji
kazi, Ofisi Kuu Pemba iliweza kununua
vifaa mbali mbali kwa ajili ya matumizi ya Ofisi vikiwemo kompyuta na samani
pamoja na kuunganisha mitandao ya mawasilisano. Pia Ofisi Kuu Pemba imeweza
kuimarisha Ofisi ya Idara ya Watu Wenye Ulemavu kwa kuwapatia Ofisi yenye
mazingira rafiki wanayoweza kuitumia bila usumbufu.
113.
Mheshimiwa Spika, Ofisi Kuu Pemba kwa mwaka wa Fedha 2011/2012
ilikadiria kutumia jumla ya shilingi 214,115,000 kwa kazi za kawaida. Kati ya
hizo Shilingi 135,875,000 kwa ajili ya kuendeshea kazi na Shilingi 78,240,000 kwa ajili ya mishahara Hadi
kufikia Mei, 2012 ilikwisha kuingiziwa kiasi cha Shilingi 218,472,625 sawa na Asilimia 102 kati ya
hizo shilingi 95,242,000 sawa na asilimia 70 kwa ajili ya kuendeshea kazi
Shilingi 123,230,625 sawa na asilimia 158 kwa ajili ya mishahara.
MALENGO KWA MWAKA WA FEDHA 2012/2013
114. Mheshimiwa Spika, Ofisi Kuu Pemba kwa mwaka wa fedha 2012/13 imejipangia
kutekeleza malengo yafuatayo:-
- Kuratibu na Kusimamia utekelezaji wa shughuli zote za Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Pemba.
- Kuimarisha mazingira ya kazi na kuwajengea uwezo wafanyakazi.
- Kukuza na kuimarisha mawasiliano ya habari.
- Kusimamia na kuratibu udhibiti wa matumizi ya fedha.
115. Mheshimiwa Spika, ili kutekeleza malengo
iliyojipangia Ofisi Kuu Pemba kwa mwaka fedha 2012/2013 inatarajia kutumia
jumla ya Shillingi 316,659,000 kwa kazi
za kawaida. Kati ya hizo Shilingi 157,774,000 kwa ajili ya kuendeshea
kazi na shilingi 158,596,000 kwa
ajili ya mishahara.
TUME YA UKIMWI
116. Mheshimiwa Spika, majukumu makuu
ya Tume ya UKIMWI ni kuhakikisha kwamba sera na mikakati ya taifa ya kupiga
vita UKIMWI zinaundwa na kutekelezwa, kutafuta rasilimali zitakazotumika katika
utekelezaji wa muitiko wa kitaifa wa kupambana na UKIMWI, kuimarisha uwezo wa
wadau katika kufanyia kazi programu za UKIMWI na kuratibu shughuli zao, kushajihisha utoaji wa huduma za tiba na
matunzo kwa watu walioathirika na kuathiriwa, kufuatilia na kutathmini umakini
na ufanisi wa utekelezaji wa mikakati, sera na muitiko wa kitaifa na kutoa taarifa zote zinazohusiana
na UKIMWI.
117. Mheshimiwa Spika, Tume ya UKIMWI kwa mwaka wa
fedha 2011/2012 ilijipangia malengo yafuatayo:-
- Kutekeleza Mkakati wa Pili wa kitaifa wa kupambana na UKIMWI, kwa kuzishirikisha sekta za serikali, sekta binafsi na Asasi za kiraia katika ngazi zote.
- Kuimarisha utekelezaji wa programu za habari, utetezi na mawasiliano kwa ajili ya kuleta mabadiliko ya tabia kwa makundi yaliyo katika hatari zaidi ya kuambukizwa na jamii kwa ujumla.
- Kuimarisha mipango ya ufuatiliaji, tathmini na utafiti inayohusiana na shughuli za UKIMWI na maeneo yanayohusiana nayo.
- Kuongeza uwezo wa Tume na wadau katika kuratibu na kutekeleza shughuli za UKIMWI kwa mfuatano huo.
118. Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Mei
2012 Tume ya UKIMWI imeweza kutekeleza yafuatayo katika malengo iliyojipangia:-
119. Mheshimiwa Spika, Tume imeweza kuzindua Mkakati wa Pili wa kitaifa wa UKIMWI Siku ya UKIMWI
Duniani tarehe 1 Disemba 2011, baada ya uzinduzi, Mkakati huo ulisambazwa kwa wadau mbali mbali kwa kuanza
kuufanyia kazi. Aidha Tume imetayarisha
Mpango wa Utekelezaji wa Mkakati wa kitaifa wa UKIMWI wa mwaka 2012/13
hadi 2013/14. Pamoja na uzinduzi huo wa mkakati Tume imezinduwa Tovuti yake
www.zac.or.tz
120. Mheshimiwa
Spika, Tume imeweza
kuzisaidia Shehia 71 katika kuandaa
mipango ya Shehia dhidi ya udhalilishaji wa jinsia na UKIMWI (Tafadhali angalia kiambatanisho Nam. 13). Pia Tume
imewapatia mafunzo juu ya usimamizi wa masuala ya
UKIMWI Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ili kuwawezesha kuongeza usimamizi wa
uwajibikaji wa sekta za Serikali kwenye masuala ya UKIMWI.
121. Mheshimiwa Spika, Tume ya UKIMWI imeweza kuimarisha utekelezaji wa programu za habari,
utetezi na mawasiliano kwa ajili ya kuleta mabadiliko ya tabia kwa makundi
maalum na jamii kwa ujumla kwa kuufanyia mapitio Mkakati wa Taifa wa
Mawasiliano na Utetezi ambao unaendana na Mkakati wa Pili wa kitaifa wa UKIMWI.
Mkakati huo kwa sasa uko tayari
kusambazwa kwa wadau kwa matumizi .
122. Mheshimiwa Spika, ili mapambano ya UKIMWI yaimarike ushiriki na ushirikishwaji wa Watu
Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI ni jambo la lazima. Kwa kulitambua hilo, mkutano
wa kitaifa uliowashirikisha viongozi katika ngazi za maamuzi kutoka sekta
mbalimbali ulifanyika. Mkutano huo ulilenga kuhamasisha umuhimu wa
kuwashirikisha Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI katika mipango mbalimbali ya
maendeleo. Jumla ya washiriki 55 (wanaume 35, wanawake 20) walihudhuria
wakiwemo Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI. Aidha jumla ya shilingi milioni
15 walipatiwa ZAPHA+ kwa ajili ya
kutekeleza shughuli zao mbali mbali zinazolenga utekelezaji wa Mkakati wa Pili wa UKIMWI. Ni
matumaini ya Tume kwamba jitihada zao zitasaidia kupunguza unyanyapaa wa Watu
Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI na hatimae
maambukizi ya VVU.
123. Mheshimiwa Spika, Taasisi za Kidini zina mchango
mkubwa katika kupiga vita suala la UKIMWI. Semina mbili za mafunzo ya viongozi wa dini zimefanyika Unguja
na Pemba. Jumla ya viongozi 58 (wanaume 34, wanawake 24) wamefikiwa. Aidha,
kupitia Mtandao wa Taasisi za Dini Katika Mapambano Dhidi ya UKIMWI, miongozo
mbali mbali ya UKIMWI imechapishwa.
Nakala 350 za miongozo ya afya ya uzazi
na jinsia zimetolewa kwa waumini wa kiislamu na kikristo.
124. Mheshimiwa Spika, Tume ya UKIMWI pia imeweza kuandaa mikutano ya utetezi wa makundi maalum
pamoja na watu wenye ulemavu Unguja na Pemba kwa kuhamasisha taasisi mbalimbali
kuzingatia mahitaji ya makundi hayo katika programu mbalimbali za UKIMWI na
afya kwa ujumla.
125. Mheshimiwa Spika, Tume imeendelea kuchapisha jarida la Jihadhari. Hadi kufikia Januari,
toleo nambari 15 limetoka kwa kuchapishwa nakala 5,000 ambazo zimesambazwa
sehemu mbalimbali. Aidha, vipeperushi 3,000 kwa ajili ya makundi maalum
vimetayarishwa na kuchapishwa.
126. Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na tatizo la UKIMWI
Tume ya UKIMWI imeweza kuyafikia
makundi maalum (wanaume wanaofanya
mapenzi na wanaume wenzao, wanawake wanaojiuza na watu wanaotumia dawa za
kulevya kwa njia ya kujidunga sindano)
kwa kuwapatia huduma mbalimbali za kujikinga na UKIMWI. Makundi haya yameweza kufikiwa
kwa kuwatumia waelimishaji rika ambao
wanafanya kazi katika maeneo ambayo
makundi haya yanapatikana zaidi. (Tafadhali angalia kiambatanisho Nam.
14).
127. Mheshimiwa Spika, katika masuala ya ufuatiliaji na tathmini, Tume ya UKIMWI imeweza kufanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa
program za UKIMWI. Jumla ya vikundi 24 vyenye miradi 36 ya kujiongezea mapato
vilifuatiliwa. Vile vile Tume iliweza kuandaa
ripoti ya mwaka ya ufuatiliaji na Tathmini kwa shughuli za UKIMWI na ripoti ya
mkutano mkuu maalum wa Umoja wa Mataifa ”United Nation General Assembly Special
Session” (UNGASS). Vile vile, Tume imeweza kukusanya, kuwasilisha, kuchambua na
kuhakiki taarifa za fomu zinazotumiwa na wadau mbali mbali katika kukusanya
taarifa za utekelezaji wa shughuli za UKIMWI (ZHAPMoS).
128. Mheshimiwa Spika, katika kuongeza uwezo wa wadau, Tume ya UKIMWI imeweza kutoa mafunzo kwa asasi za kiraia na
wadau wengine. Jumla ya asasi 55
zilipatiwa mafunzo ya uongozi, utetezi, ushawishi, ubia, utatuzi wa migogoro na
uandishi wa ripoti. Washiriki 15
(wanaune 9, wanawake 6) kutoka ZANGOC walipatiwa mafunzo ya jinsia na UKIMWI,
waandishi wa habari na wasanii 25 (wanaume 15, wanawake 10) walipatiwa mafunzo
juu ya ubunifu wa kazi za mawasiliano na
waelimishaji rika 40 (wanaume 22, wanawake18) kutoka katika makundi maalum
walipatiwa mafunzo ya namna ya kuyafikia
makundi maalum. Aidha Tume imeandaa warsha ya kuwahamasisha waheshimiwa wawakilishi na makatibu wa kamati
juu ya muitiko wa kitaifa wa kupambana
na UKIMWI ili kuongeza uelewa wao.
129. Mheshimiwa Spika, Tume ya UKIMWI imeimarisha mazingira
ya utendaji kazi kwa kufanya ukarabati wa jengo lake na kutoa mafunzo ya muda
mrefu na mfupi kwa wafanyakazi ili kuongeza ufanisi katika kutimiza majukumu yake. Katika kipindi cha mwaka wa
2011/12, jumla ya wafanyakazi 3 walipatiwa mafunzo ya muda mrefu na
wafanyakazi 6 wamepata mafunzo ya muda
mfupi. (Tafadhali
rejea kiambatanisho Nam. 3)
130. Mheshimiwa Spika, Tume ya UKIMWI
kwa mwaka wa fedha 2011/2012 ilikadiriwa kutumia Shilingi 472,000,000 kwa kazi
za kawaida hadi kufikia Mei 2012 ilikwisha ingiziwa shilingi 439,648,862 sawa
na asilimia 93. Aidha Tume
iliidhinishiwa Shilingi. 90,000,000 kwa kazi za maendeleo na hadi kufikia Mei
2012, ilikwisha ingiziwa Shilingi 90,000,000 sawa na asilimia 100. Kwa upande
wa fedha za wahisani walitarajiwa kuchangia Shilingi 1, 300,000,000 na hadi
kufikia Mei 2012, wamechangia Shilingi 705,550,000 sawa na asilimia 54.3.
MALENGO KWA MWAKA WA FEDHA 2012/2013
131. Mheshimiwa Spika, Tume ya UKIMWI
kwa mwaka wa fedha 2012/13 imejipangia kutekeleza malengo yafuatayo:-
- Kuimarisha uratibu na utekelezaji wa Sera, Sheria na Mkakati wa Pili wa kitaifa wa UKIMWI.
- Kuongeza uwezo wa programu za habari, utetezi na mawasiliano ili kuchochea mabadiliko ya tabia katika jamii na makundi maalum.
- Kuongeza utumiaji wa taarifa zinazotokana na ufuatiliaji, tathmini na utafiti katika programu za UKIMWI.
- Kuimarisha mazingira ya kazi ili kuleta ufanisi.
- Kusimamia utaratibu wa udhibiti wa matumizi ya fedha .
132. Mheshimiwa Spika, ili kutekeleza malengo
iliyojipangia Tume ya UKIMWI kwa mwaka fedha 2012/2013 inatarajia kutumia jumla
ya Shilingi 739,000,000 kwa kazi za kawaida, kati ya hizo shilingi 500,838,000
kwaajili ya kuendeshea kazi na shilingi 238,162,000 kwaajili ya mishahara Aidha
inatarajia kutumia Shilingi 50,000,000 kwa kazi za maendeleo na Shilingi
893,760,000 kutoka kwa wahisani.
SHUKURANI
133. Mheshimiwa Spika, kabla ya kumaliza hotuba yangu
naomba kuwashukuru wote waliofanikisha ukamilishaji wa kazi hii. Pia napenda
kuchukua fursa hii kukupongeza wewe Mheshimiwa Spika kwa Uongozi wako makini wa
kuliongoza Baraza hili tukufu katika awamu hii ya saba pamoja na Mheshimiwa
Naibu Spika na Wenyeviti wa Baraza. Aidha, bila ya kuwasahau naomba niwashukuru
kwa dhati kabisa Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako tukufu kwa kuwa wasikivu na
wastahamilivu wakati wote nilipokuwa nikiwasilisha hotuba yangu. Ni matumaini
yangu kwamba tutaendelea kushirikiana katika kutoa michango mbali mbali ambayo
itasaidia Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kutatua matatizo yanayoathiri
jamii. Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais inaahidi kuichukua michango yote
itakayotolewa na Wajumbe wa Baraza hili na kuifanyia kazi kwa maslahi ya Jamii
na Taifa kwa ujumla.
134. Mheshimiwa Spika, napenda kutoa shukrani zangu za
dhati kwa nchi marafiki, mashirika ya Kimataifa na watu binafsi kwa kuendelea
kutusaidia kuendeleza shughuli za Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais. Nchi hizo
ni pamoja na Marekani, Finland, Norway, Uingereza, Uholanzi, Australia, China,
Brazil, India na Falme za nchi za Kiarabu na Oman. Pia mashirika ya kimataifa
yakiwemo UNDP, UNICEF, UNFPA, UNAIDS, UNEP, UNODC, UNFCCC, WHO, World Bank,
AIHA, CDC, ICAP, Save the Children na nchi na mashirika mengine ambayo
sikuyataja, lakini kwa njia moja au nyengine yanatuunga mkono katika shughuli
zetu za maendeleo. Juhudi na michango yao tunaithamini sana.
135. Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako tena natoa
shukrani zangu kwa Viongozi wakuu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa na
Taasisi mbali mbali za Serikali
zikiwemo vyombo vya ulinzi na usalama
na taasisi zisizo za kiserikali zinazojishughulisha na masuala ya
UKIMWI, mapambano dhidi ya dawa za kulevya, utunzaji na uhifadhi wa mazingira
na kutetea haki na fursa za watu wenye ulemavu. Taasisi hizi zinatoa mchango
mkubwa na mashirikiano katika utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Makamu wa
Kwanza wa Rais, mashirikiano yao yanasaidia kuleta ufanisi katika utekelezaji wa
majukumu ya Ofisi yetu. Nawaomba waendelee kutupa mashirikiano hayo kwa
lengo la kuwatumikia wananchi
wa Zanzibar na kufikia lengo kuu la kukuza uchumi na kupambana na
umasikini.
136.Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa
Rais inatoa shukurani za dhati kwa vyombo vya habari vyote ambavyo tumekuwa
tukishirikana navyo kuielemisha jamii juu ya athari za uharibivu wa mazingira,
matumizi ya dawa za kulevya, namna ya kujikinga na VVU na UKIMWI na umuhimu wa
kuwahudumia watu wenye ulemavu. Ni matumaini yetu kuwa tutaendeleza
mashirikiano haya kwa faida ya jamii yetu sote.
137. Mheshimiwa Spika, shukurani za
pekee ziwaendee wote walioshiriki kwa njia moja au nyengine katika kufanikisha
utekelezaji wa kazi za Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais. Mwisho napenda
kuwashukuru wananchi wote kwa ujumla kwa kufanikisha kazi za maendeleo ya nchi
yetu.
HITIMISHO
138.Mheshimiwa Spika, kwa heshima nachukuwa nafasi hii
kuwaomba Wajumbe wa Baraza lako tukufu waipokee, waijadili, watushauri,
watuelekeze na hatimae kuidhinisha matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa
Rais ya jumla ya shilingi bilioni mbili
milioni mia saba na sabini (T.Shs. 2,770,000,000)
kwa mwaka wa fedha 2012/2013. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni moja milioni mia tano kumi na tano (T.Shs. 1,515,000,000) kwa ajili kuendeshea
kazi na shilingi bilioni moja milioni
mia mbili hamsini na tano (TShs.1,255,000,000)
kwa ajili ya mishahara. Aidha
tunaliomba Baraza lako Tukufu kuidhinisha jumla ya shilingi milioni mia mbili hamsini na tano (T.Shs. 255,000,000) kwa kazi za maendeleo ikiwa ni mchango wa Serikali na Shilingi milioni mia saba na tano na laki
sita (T.Shs 705,600,000) fedha
za wahisani (Tafadhali angalia kiambatanisho Nam. 15 a na b).
139. Mheshimiwa Spika, aidha, naliomba
Baraza lako tukufu liidhinishie Tume ya UKIMWI matumizi ya jumla ya shilingi milioni miasaba thelathini na tisa
(T.Shs. 739,000,000) kwa kazi za
kawaida, ambapo shilingi milioni mia
tano laki nane thelathini na nane elfu (T.Shs. 500,838,000) kwa ajili ya kuendeshea kazi na shilingi milioni mia mbili thelathini na nane laki
moja sitini na mbili elfu (TShs.238,162,000)
kwa ajili ya mishahara. Aidha
tunaliomba Baraza lako tukufu kuidhinisha jumla ya shilingi milioni hamsini (T.Shs. 50,000,000)
kwa kazi za maendeleo ikiwa ni mchango wa Serikali na shilingi milioni mia nane tisini na tatu lakisaba
sitini elfu (T.Shs 893,760,000) mchango
wa wahisani (Tafadhali angalia kiambatanisho Nam. 15 c na d).
140. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
No comments:
Post a Comment