Joseph Ngilisho, ARUSHA
KITUO kidogo cha Polisi kilichopo Gereza kuu la Kisongo jijini hapa, kimenusurika kuchomwa moto na kundi la Morani wanaofikia 700 wa jamii ya kifugaji walioandamana wakiwa na silaha mbalimbali za jadi wakituhumu kituo hicho kuwaachilia watuhumiwa wa ujambazi pindi wanapowafikisha.
Wananchi hao wakiwa na matawi ya miti walijikusanya kutoka vijiji vitatu vya Mateves, Kisongo na Ngorbobo na kuelekea katika kituo hicho cha polisi na kuzua hofu kubwa kwa watu wanaosafiri wakiwemo watalii waliokuwa wakirandaranda eneo hilo ambao walionekana wakitimua mbio.
Wakati wakijaribu kuingia kwenye uzio wa uwanja wa ndege wa Kisongo ili kushika barabara ya kuelekea katika kituo hicho cha polisi, askari wenye silaha za moto na mabomu wakiwa kwenye magari matatu ya kutuliza ghasia walifanikiwa kuwazuia.
Kwa mujibu wa wananchi hao wakiongozwa na viongozi wao wa vijiji na vitongoji wanakituhumu kituo hicho kushirikiana na wahalifu, wakisisitiza kuwa pindi wanapowakamata wahalifu bila kujichukulia sheria mkononi wamekuwa wakiwafikisha kituoni, lakini katika hali isiyofahamika wanashangaa kuwaona mitaani tena.
Mmoja wa wananchi hao aliyejitambulisha kwa jina la Shangwe mkazi wa Kisongo alidai kuwa uhalifu katika eneo hilo la Kisongo umezidi kuongezeka kwani matukio ya ujambazi wa kutumia silaha yamekuwa yakijirudia huku polisi wakishindwa kudhibiti.
Alisema hivi karibuni alivamiwa na majambazi hao nyumbani kwake na kumpora kiasi cha shilingi milioni 7 na zaidi ya hapo majambazi hao walisikika wakisema lazima wamuue hali ambayo imemtia hofu na kumfanya aache kulala nyumbani kwake na kulala katika hospitali ya Mount Meru kutokana na hofu ya kuuawa.
Aidha, aliongeza kuwa hali ya usalama kwa wakazi wa maeneo hayo ni ndogo kutokana na matukio ya ujambazi yanayotokea mfululizo, kwani alisema tukio la uporaji wa shilingi milioni 7 lilienda sambamba na uvamizi wa maduka kadhaa ya bidhaa za rejereja na jumla pamoja na tukio la kuporwa kwa silaha aina ya bunduki ya mkazi mmoja wa eneo la kisongo.
Akizungumza muda mfupi baada ya kufanikiwa kuwatuliza wananchi hao, mkuu wa upelelezi wa polisi mkoa(RCO), Camilius Wambura mrakibu mwandamizi wa polisi SSP,alisema pamoja na kuwashukuru wananchi hao kwa kukubali mazungumzo na jeshi la polisi aliwataka wasijichukulie sheria mkononi.
Alisema kuwa jeshi la polisi halina mamlaka ya kuaachia watuhumiwa bila sababu za msingi isipokuwa mahakama ndio yenye mamlaka ya kufanya hivyo pale inapojiridhisha kuwa mshtakiwa hakutenda kosa.
Hata hivyo wananchi hao walimwambia RCO Wambura kuwa madai yao ni kutaka kujengewa kituo cha polisi eneo la kisongo tofauti na kile kilichopo ambacho kipo mbali na makazi yao, kuwepo kwa gari la doria kwa muda wote wa usiku.
Kwa upande wa kamanda wa polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas pamoja na kuthibitisha tukio la wananchi hao, alidai ya kuwa hajapata taarifa za matukio ya uhalifu katika eneo la kisongo.
Sabas aliwasihi wananchi hao kutokuwa wepesi wa kujichukulia hatua sisizofaa badala yake wanapowafikisha kituoni watuhumiwa waendelee kufuatilia watuhumiwa wao na kutoa ushahidi mahakamani ili mahakama iwatie hatiani na kuwahukumu kwenda jela.
No comments:
Post a Comment