Na Rose Chapewa, MOROGORO
WAZIRI wa Uchukuzi Dk. Harison Mwakyembe amefanya ziara ya kushitukiza katika kituo cha mabasi cha msamvu Manispaa ya Morogoro na kufanya ukaguzi wa mabasi ya abiria yaendayo mikoani.
Katika operesheni hiyo mabasi matatu aliyaamrisha yalipe faini ya shilingi 250,000 kila moja kutokana na makosa mbalimbali ikiwemo la kutokuwa na dereva wa akiba.
Ziara hiyo aliifanya mapema wiki hii majira ya asubuhi kwa kushirikiana na maofisa wa Mamlaka ya udhibiti wa usafiri wa nchi kavu na majini (SUMATRA), ambapo lengo lake ni kuangalia mabasi yanayofanya safari za mikoani na nje ya nchi na kuona kama yanakidhi vigezo vya SUMATRA katika shughuli ya kusafirisha abiria.
Katika Ziara hiyo Dk. Mwakyembe alifika katika kituo hicho cha mabasi na kuegesha gari mbali kidogo kisha kuelekea kwenye mabasi huku akijifanya kama abiria na kuingia ndani ya mabasi hayo kisha kuanza kukagua leseni za madereva na vitambulisho vya kampuni za mabasi wanavyotumia madereva.
Ukaguzi mwingine alioufanya ni ratiba za safari pamoja na usalama wa mabasi na baadaye aliamrisha madereva walioonekana kuwa na makosa kulipa faini SUMATRA.
Mabasi yaliyolipishwa faini ni pamoja na Royal Coach linalofanya safari zake kutoka Dar es Salaam kuelekea Bukoba ambapo dereva wake hakuwa na kitambulisho cha kampuni, basi la Super Najimunisa na Muro Investment yanayofanya safari zake Dar es Salaam kuelekea Mwanza ambapo mabasi hayo yalikuwa na kosa la kutokuwa na dereva wa akiba.
Baada ya kubaini makosa hayo waziri Mwakyembe aliwataka madereva ambao walionekana kuwa na makosa kulipa faini ya papo hapo kwa SUMATRA, vinginevyo aliwataka SUMATRA kuwafikisha mahakamani hata hivyo madereva hao walikubali kulipa faini hiyo baada ya waliwasiliana na wamiliki wa mabasi wanayofanyia kazi.
Akizungumza na maofisa wa SUMATRA pamoja na madereva Dk. Mwakyemba alisema kuwa makosa kama hayo yanaweza kusababisha ajali za barabara na hivyo kupoteza maisha ya watu, vilema vya kudumu na uhalibifu wa mali na kwamba ataendelea kufanya ziara za namna hiyo mara kwa mara ili kubaini makosa mengine.
Aidha aliwataka SUMATRA pamoja na kikosi cha usalama barabarani kusimamia sheria za usalama barabarani na kutowaonea aibu madereva watakaonekana kuwa na makosa kwani kwa kufanya hivyo kutasaidi kupunguza ajali ambazo zimekuwa ni tishio hapa nchini.
Kwa upande wake mkuu wa usalama barabarani mkoani hapa Leonard Gyindo alisema kuwa kikosi cha usalama barabarani kimejipanga katika kudhibiti ajali za barabarani kwa kufanya ukaguzi kabla ya gari halijaondoka katika kituo hicho na kwa madereva wenye makosa wamekuwa wakilipishwa faini ya papo hapo na wengine kufikishwa mahakamani.
No comments:
Post a Comment