Na Kijakazi Abdalla, ZJMMC
WAKATI mwezi wa mfungo mtukufu wa Ramadhani ukikaribia bei za bidhaa mbalimbali zinaonekana kupanda zaidi ikilinganishwa na miezi ya nyuma.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti, baadhi ya wafanyabiashara wa soko la Mwanakwerekwe la mjini hapa, wamesema kuwa bei za bidhaa muhimu kwa mwezi huu zimepanda bei.
Walisema kuwa bei ambazo ni muhimu kwa mwezi mtukufu hasa nazi zinapatikana kwa bei ya shilingi 550 hadi 600 kwa jumla kwa nazi moja, mkungu wa ndizi ni shilingi 20,000 ambapo kwa chana moja ni shilingi 2,000 hadi 1,500 ndizi mkono wa tembo dole moja inauzwa kwa bei ya shilingi 1,500 hadi 1,600 muhogo polo shilingi 12,000 hadi 14,000.
Kwa upande wa bidhaa za nafaka kama maharage kilo moja ni shilingi 1,600, njugu mawe kilo moja ni shilingi 1,900 kunde kilomoja shilingi 1,400 ambapo mtama kwa kilo unauzwa shilingi 900.
Aidha wafanyabiashara hao walisema kwa upande wa bidhaa za matunda kama mananasi linauzwa kwa bei ya shilingi 2,500 hadi 4,000, ambapo embe boribo kwa tenga moja zinauzwa shilingi 18,000 hadi 20,000.
Tikiti moja katika soko hilo linauzwa kati ya shilingi 1,500 na 2,000 hata hivyo inategemea kwa ukubwa wa tunda lenyewe, matunda ya pesheni kwa kilo linauzwa shilingi 2,000 hadi 1,500.
Akizungumza na Gazeti hili, Kaimu Meneja mkuu wa soko hilo, Said Omar Talib, alikiri kuwepo na upandaji wa bidhaa hizo, ambapo alisema inatokana na baadhi ya bidhaa hizo kutoka Tanzania Bara.
Aidha aliwataka wafanyabiashara kutowakomoa wananchi kwa kuwauzia bidhaa hizo kwa bei ya juu, jambo ambalo litawashinda kumudu bei hizo hasa katika mwezi huo wa Ramadhan ambapo mahitaji yanaongezeka.
“Tunawaomba wakulima wasivune mazao machanga kwa ajili ya kufanya biashara, kwani kufanya hivyo ni hasara kwa pande zote mbili kati ya muuzaji na mnunuzi,” alisema.
No comments:
Post a Comment