WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Amali imesema haina haja kutoa tamko la kuiondoa elimu ya juu ndani ya Mfumo wa Muungano kwa vile tayari kuna mchakato wa kupatikana kwa maoni ya kuweza kuandaliwa kwa katiba mpya.
Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Zahra Ali Hamad, aliyasema hayo jana wakati akijibu suala la Mwakilishi wa Mji Mkongwe, Ismail Jussa Ladhu aliyetaka kujua kama wizara ina mpango wa kuitoa elimu ya juu katika mambo ya Muungano.
Akijibu suala la msingi la Mwakilishi wa Mpendae, Mohammed Said Dimwa, aliyetaka kujua kujitoa kwa vyuo vikuu ya Zanzibar katika mfumo wa udahili kitaifa CAS kama ndio chanzo cha wanafunzi wa Zanzibar kukosa mikopo ya elimu ya juu, Zahra alisema alisema hilo halina ukweli kwani bado wanafunzi wa Zanzibar wamekuwa na haki ya kuweza kupata mikopo hiyo.
Alisema ni vyema kwa wanafunzii wa Zanzibar kuomba mikopo hiyo kwa vile tayari Wizara hiyo imeshafanya mazungumzo na taasisi hiyo kuona wanafunzi wa Zanzibar wanafaidika.
Alisema Wizara hivi sasa inakusudia kufuatilia mikopo hiyo kuona Zanzibar inaweza kupata nafasi hizo kama ni haki ya Wazanzibari.
Hata hivyo, Naibu Waziri huyo alisema hivi sasa Wizara,inajiandaa kufuatilia kwa undani kufahamu idadi ya watu waliofaidika na mikopo ya elimu ya juu.
Alisema mfumo wa kujiunga na CAS upo kwa mazingira ya hiari na ndio maana baadhi ya vyuo havijajiunga na mfumo huo.
Alisema Chuo Kikuu cha Zanzibar na Chuo Kikuu cha Ualimu Chukwani havijawahi kujiunga na mfumo huo na wanafunzi wake amekuwa wakipata mikopo ya elimu ya juu kupitia Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ya Serikali ya Muungano wa Tanzania.
No comments:
Post a Comment