Habari za Punde

Wachuuzi watakiwa kudumisha usafi


WACHUUZI katika madiko ya kuuzia samaki wametakiwa kudumisha usafi ikiwa ni hatua ya kuyafanya kuwa katika hali nzuri ya kimazingira.

Waziri wa Uvuvi na Mifugo, Abdilahi Jihad Hassan, aliyasema hayo jana wakati akijibu suala la Mwakilishi wa Jimbo la Wawi, Saleh Nassor Juma, aliyetaka kujua ni kwanini hivi sasa kuna madiko ambayo yameonekana kuwa ni machafu huku wachuuzi wakiweka biashara zao chini kunakosababishwa na madiko yaliopo kutokuwa na hadhi.

Akijibu suala hilo, Waziri huyo alisema suala la unadhifu wa masoko hayo yapo chini ya usimamizi wa wafanyabishara wenyewe na ni vyema wakafikiria namna ya kudumisha usafi katika sehemu zao za biashara.

Alisema mara nyingi Wizara hiyo imekuwa ikijenga madiko kwa ajili ya kuwapatia wananchi sehemu za kufanya biashara zao lakini matumizi huachiwa wao wenyewe pamoja na Wizara ya Afya.

Alisema kutokana na kuwapo kwa vitengo vya kusimamia hifadhi ya mazingira na huduma za afya ni vyema kwa taasisi husika kuiona hali hiyo na kuisimamia vyema ili kuyafanya madiko hayo kuwa sio sehemu zinazoweza kuleta madhara kwa binadamu.

Alisema wakuu wa madiko sio wanaokusanya mapato kutoka kwa wachuuzi wala wavuvi bali kazi hiyo hufanywa na Halmashauri.

Alisema madiko ambayo hukusanywa fedha za mapato ni zile zinazohusu wao wenyewe ambapo huamua kufanya hivyo kwa ajili ya maendeleo yao ya kijiji na hayana uhusiano na wakuu wa madiko.

Kuhusu suala la sehemu za hifadhi, Waziri huyo alisema wizara hiyo kupitia Idara ya Maendeleo ya Uvuvi inajenga madiko sehemu mbali mbali pale uwezo unaporuhusu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.