SERIKALI ya Zanzibar imesema haijawahi kupokea fedha za aina yoyote kutoka mfuko wa mikopo unaosimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania.
Waziri wa Nchi Afisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf Mzee, aliyasema hayo jana wakati akijibu suala la Mwakilishi wa Jimbo la Kiwani, Hija Hassan Hija, aliyetaka kujua kama Zanzibar imeweza kupata mikopo hiyo.
Akijibu suala hilo Waziri huyo alisema ni kweli mikopo hiyo ilikuwapo lakini Zanzibar haijaweza kupatiwa na hakuna mtu aliyepatiwa.
Alisema kutokana na hali hiyo tayari Wizara hiyo hivi sasa imeshafanya mazungumzo na uongozi wa benki hiyo kuona Zanzibar nayo inapata mikopo hiyo.
Akijibu suala la msingi la Mwalishi la Jimbo la Mji Mkongwe, Ismail Jussa Ladhu, alietaka kujua kiasi cha mfumko wa bei uliopo, Waziri Omar alisema ulikuwa kwa kasi sana mwaka jana kwa kufikia asilimia 20.8 hadi kufikia mwezi Disemba 2011.
Alisema kupanda kwa mfumko huo wa bei uliweza kwenda sambamba na mfumko wa bei kwa Tanzania Bara, jambo lililoifanya Benki Kuu kupambana na mfumko huo kwa kupandisha kiwango cha riba ya Benki Kuu inayotozwa kwa mikopo iendayo taasisi za fedha nchini.
Hatua hiyo Waziri huyo alisema ilisaidia kupunguza ongezeko la ukwasi baina ya mabenki na husababisha kuleta uwiano kati ya fedha na mahitaji halisi ya shughuli za kiuchumi.
No comments:
Post a Comment