Habari za Punde

’Sikupewa shindikizo kujiuzulu’.

Waziri Aboud abainisha changamoto
Cuf yaupongeza ujasiri wa Hamad


Na Husna Mohammed

ALIYEKUWA waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, Hamad Masoud Hamad amesema amechukua hatua ya kujiuzulu sio kwa hiyari yake na sio shindikizo la mtu yeyote.

Waziri huyo wa zamani aliyerudi kwenye viti vya ‘backbenchers’ ndani ya ukumbi wa Baraza la Wawakilishi, alieleza hayo jana katika ukumbi wa Baraza hilo alipopata nafasi ya kueleze machache na kuuliza suali kufuatia kuwasilishwa taarifa ya serikali.

Hamad Masoud ambaye ni Mwakilishi wa jimbo la Ole (CUF), alisema uamuzi aliouchukua umetoka katika nafasi yake baada ya kupima na kufikiri na si maamuzi yaliyotokana na shindikizo la mtu.

"Nimejiuzulu kujenga heshma yangu, wananchi wa jimbo langu la Ole na sio shinikizo la mtu yoyote", alisema.


Alisema pamoja na kuwepo kwa shinikizo kutoka kwa watu mbalimbali la kutakiwa kujiuzulu, lakini hakushawishika kwa hayo ambapo baada ya kupata ushauri kutoka kwa uongozi wa juu wa chama chake aliamua kujiuzulu nafasi hiyo.

"Nilizungumza na Rais wa Zanzibar pamoja na kumpelekea barua ili kujiuzulu nafasi hii, tuliweza kuzungumza mambo kadhaa lakini sitaki kuyataja hapa", alisema.

Julai 20 mwaka huu waziri huyo aliandika barua ya kujiuzulu kufuatia kuzama kwa meli ya MV Skagit ambayo hadi jana imethibitika kupoteza maisha ya watu 78.

Katika hatua nyengine serikali imesema tukio la kuzama kwa meli ya MV. Skagit limetoa funzo kwa serikali, hasa uhaba wa vifaa katika vya kisasa vya uokozi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed alieleza hayo jana katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi alipokuwa akiwasilisha taarifa rasmi ya serikali juu ya tukio la kuzama kwa meli ya MV. Skagit.

Aliyataja mambo mengine kuwa ni kukosekana kwa taarifa na uwezo wa ndani wa kukabiliana na maafa ikiwemo uwezo wa vifaa na wataalamu pamoja na udogo wa sehemu ya kuhifadhia maiti.

Changamoto nyengine ni maamuzi sahihi na ya haraka yaliyochukuliwa na viongozi wetu yameweza kuleta ufanisi mkubwa katika operesheni ya uokozi.

Aidha Waziri Aboud, alisema shilingi milioni 320 zimepokelewa na kuingizwa katika akaunti ya Mfuko wa Maafa Zanzibar kutoka kwa watu mbalimbali.

Hata hivyo, alisema shilingi milioni 20 hadi kufikia tarehe 22 zimetumika kwa ajili ya mambo mbalimbali kwenye ajali hiyo.

Wakati huo huo, Chama cha CUF kimesema uamuzi wa kujiuzulu uliochukuliwa na aliyekuwa waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, Hamad Masoud Hamad ni sahihi.

Mkurugenzi wa Haki za Binaadamu, Habari na Uenezi na Mawasiliano na Umma, Salim Bimani alieleza hayo jana kupitia taarifa ya chama hicho iliyotolewa kwa vyombo vya habari.

Mkurugenzi Bimani alisema CUF inaamini kuwa uamuzi wa waziri huyo kujiuzulu ni hatua sahihi katika uwajibikaji na kwamba amechukua ujasiri mkubwa hali ambayo itakuwa mfano wa kuigwa katika zama za demokrasia na utawala bora, ndani na nje ya nchi.

“Kila mkweli na mwenye upeo wa kuona mbali ataelewa kwamba Hamad, pamoja na chama chake, wamejipambanua, kuwa tafauti, katika utendaji, na huo ni mfano bora wa kuigwa katika kutumikia umma na ujenzi wa demokrasia ya kweli“, alisema Bimani.

Alifahamisha kuwa Chama kimebaini kuwa Hamad Massoud, hana kosa wala hakutenda uzembe wa namna yoyote, bali amechukua hatua hiyo kwa ajili ya kubeba dhamana ya kisiasa.

Mkurugenzi huyo alisema waziri huyo amejizulu kutokana na kuguswa na tukio la kuzama kwa meli ya MV. Skagit, jambo ambalo limewagusa wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

“Kila mmoja anayo haki ya kuwajibika na kuchukua maamuzi sahihi yenye hikma na busara pale inapobidi na hasa ambapo yaliyojiri yanagusa nchi, taifa, na maslahi ya umma, na hiyo ni daraja ya juu ya uungwana“, alisema Bimani.









No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.