Habari za Punde

Vijana skauti Bububu watakiwa kuwa polisi jamii

Na Salum Jecha, ( ZJMMC).
VIJANA wa skauti wa Bububu,wametakiwa kuwa askari jamii kwa kutoa taarifa kwa jeshi la polisi na shehia kwa matukio yanayotokea katika jamii.

Akizungumza katika sherehe ya kutimiza miaka minne ya kuundwa kundi la skauti ya Bububu, Msaidizi mkuu wa kituo cha polisi Bububu, Abeid Mjaka, katika viwanja vya Skuli ya Bububu msingi, alisema ni vizuri vijana wa Skauti kuanza kazi ya kuhamasisha vijana kujiunga na skauti ili kuepukana na vishawishi vinavyoweza kujitokeza katika maisha yao.

Aidha aliwataka vijana hao kujiendeleza kielimu kwa kuwa elimu ni msingi wa maisha.
"Vijana muwe makini sana juu ya elimu kwani bila ya elimu hamtoweza kufanya lolote, msitoroke skuli na pia muwe wajumbe katika kutoa taarifa za wanafunzi watoro ambao wanazurura nyuma ya skuli lazima muwaripoti katika ofisi za walimu," alisema msaidizi mkuu wa Kituo.

Kwa upande wake Mkuu wa upelelezi Kituo cha polisi Bububu, Sajenti Ali Omar, alieleza kuwa milango iko wazi wakati wowote wa skauti kutafuta ushauri na msaada wa kisheria pindi wakihitaji kufanya hivyo.

Mkuu huyo wa upelelezi alisema kuwa kituo hicho kiko tayari kutoa mashirikiano ya kimafunzo kama watayahitaji.

"Sisi tuko tayari kukupeni mafunzo pindi mtakapokuwa tayari, tunakuombeni mjipange nasi tuko tayari kukupeni mashirikiano kwa kuwapa mafunzo hayo," alisema.

Nae mkuu wa skati Bububu, Saidi Salum Muhamed, alieleza kwamba kundi lao linakabiliwa na changamoto mbali mbali zikiwemo ukosefu wa mahema, usafiri, unifom, kisanduku cha huduma ya kwanza pamoja na ofisi, ambapo kwa sasa wanafanya kazi zao katika skuli ya msingi Bububu siku za mapumziko.

Kundi la skauti la Bububu limeundwa Julai 15, 2009,ambapo lilianza na vijana 100 ambapo kwa sasa kundi hilo lina vijana 170 wanawake na wanaume.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.