Waziri asiye na Wizara Maalumu katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Mansour Yussuf Himid ametaka Zanzibar iwe Dola huru iliyokamilika na iwe na kiti chake Umoja wa Mataifa (UN) na kutambuliwa na taasisi za kimataifa.
Waziri huyo ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM na Katibu wa Idara ya Fedha ya Chama hicho Zanzibar, pia amepinga msimamo wa chama hicho tawala kuwa na Muungano wa Serikali mbili na kuudhihaki kuwa hauna manufaa wala tija kwa Wazanzibari.
Mansour alisema hayo jana wakati akichangia bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria katika kikao cha bajeti cha wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2012/13.
“Wananchi wetu wawe huru katika kutoa maoni ya mchakato wa Katiba...kama watu hawataki Muungano waseme, ikiwamo wanaotaka Muungano wa mkataba akina sisi … mfumo huu wa Serikali mbili kwangu mimi sebuu,” alisema Mansour akimaanisha anaukataa moja kwa moja.
Alisisitiza kuwa Muungano wa Serikali mbili kwa sasa hauna nafasi tena na hauwezi kuisaidia Zanzibar kwenda mbele na kupiga hatua kubwa ya kiuchumi kutokana na Zanzibar kukosa sifa ya kuwa Dola yenye kumiliki uchumi wake.
Alitoa mfano wa maeneo huru ya uchumi ambayo yalitangazwa na Rais mstaafu wa Zanzibar, Dk Salmin Amour mwaka 1992 Fumba yakiwa na eneo la hekta 900 za msitu zilizotengwa, lakini yameshindwa kuendelezwa na kubaki msitu wanaoishi wanyama aina ya komba na ngedere.
“Tusidanganyane hakuna mwekezaji anayeweza kuja kuwekeza katika maeneo huru ya uchumi yaliyo Fumba kwa sababu Zanzibar haina uwezo wa kuhimili uchumi wake na ndiyo maana maeneo hayo yamekuwa msitu wa kuishi komba na ngedere,” alisema Mansour. Hakuna wa kumtisha.
Alisema zama za kutishana zimepitwa na wakati na kufafanua kuwa kutofautiana katika mawazo isiwe chanzo cha kutukanana na kudharauliana na kusingiziana kiasi watu wengine kuonekana wahalifu wakifananishwa na wafuasi wa vyama vya kisiasa vilivyopita ikiwamo Hizbu na Jumuiya ya Mihadhara ya Kidini ya Uamsho.
Alitoa mfano wa viongozi walioongoza kwa vitisho na nguvu za kijeshi, kwamba kwa sasa hawapo tena madarakani kutokana na wananchi kuwapinga na kuwakataa moja kwa moja wakiwamo marais wa zamani wa Misri, Hosni Mubarak na wa Libya Kanali Muammar Gaddafi.
Chanzo: Habari Leo
No comments:
Post a Comment