Habari za Punde

Wawakilishi wataka kufanyiwa marekebisho baadhi ya sheria

Na Mwashamba Juma
WAJUMBE wa Baraza la wawakilishi Zanzibar, walisema kuwa baadhi ya sheria za Tanzania zimekuwa zikikabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuingiliana na taratibu za kidini.

Wakichangia mada katika mafunzo ya sheria zinazoathiri maslahi ya mtoto, yaliofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Zanzibar Ocean View Kilimani mjini Unguja, walisema ingawa Baraza linaridhia na kupitisha sheria zinazohusia na Zanzibar, lakini walisema bado zinahitaji kurekebishwa ili ziendane na matukio halisi yanayotokea katika jamii.

Walifahamisha kuwa katika kuridhia sheria za kimataifa pamoja na matamko ya kimataifa sambamba na kuzitumia kama sheria mama, lakini katika mambo ya Muungano uwakilishi wa Zanzibar kimataifa wa kuridhia sheria za kimataifa unapitishwa bungeni.

"Maadili ya dini nyengine kwa kile kinachojuulikana kuwa utofauti wa dini kati ya Tanzania bara na visiwani katika uwakili wa mambo ya nje, hivyo suala la kuridhia baadhi ya sheria kunabana maadili ya upande mmoja hasa katika haki ya kuabudu kwa mtoto ambapo sheria za kimataifa zinampa fursa mtoto kuabudu dini anayotaka jambo ambalo haliendi sambamba na dini nyengine kama uislamu," walisema baadhi ya wawakilishi hao.

Walisema wakati umefika sasa wa kukubali sheria za kimataifa ambazo hazitokwenda kinyume na maadili na utamaduni wa nchi.

Hata hivyo, walikishukuru kituo cha huduma za sheria Zanzibar (ZLSC) kwa kuwaandalia mafunzo hayo na kusema kuwa sehemu walio ni kubwa kwani inahitaji uelewa mkubwa kisheria.

Akichangia katika mafunzo hayo, Mwakilishi wa Wawi, Saleh Nassor Juma, alisema ni lazima watoto wathaminiwe hasa ikizingatiwa kuwa ni viongozi wa baadae wa nchi hiyo hivyo hakuna haja ya kuwadharau.

"Baraza la Wawakilishi linawatetea watoto kwa sababu linaamini kwamba baada ya miaka michache watoto hao watakuwa na haki ya wapiga kura kwa maendeleo yao ya baadae, sambamba na kutegemewa wanasheria wa baadae pia kutayarishwa kwa jili ya kupata mainjinia na viongozi wa baadae kwa taifa letu, hivyo Baraza la Wawakilishi lina kila sababu ya kuwatetea na kuwajali watoto," alisema.

Alifafanua kuwa katika kuimarisha na kuboresha mazingoira mazuri ya mama na mtoto, baraza la Wawakilishi lazima lipitishe bajeti ambayo italenga kwenye masuala ya kuimarisha vituo vya afya sambamba na kuimarisha miundombinu kwa maslahi ya mama na mtoto.

Nae Mwakilishi wa Jimbo la Kwahani, Ali Salum Haji, wakati akichangia mada ya 'Sheria mbalimbali zinazoathiri maslahi ya mtoto' alisema suala la kuchelewesha kesi za watoto mahakamani kwa kisingizio cha kipimo cha DNA haliwatendei haki watoto wa kesi za unyanyasaji na udhalilishaji kijinsia bali ni kuwakosesha haki zao kisheria.

Nae Kaimu Mkurugenzi wa kituo cha huduma za sheria Zanzibar (ZLSC), Harusi Miraji Mpatani, alisema suala la kutoa msaada wa sheria kwa watoto ni njia moja ya kuwajali na kuwapatia haki zao za msingi kisheria, kwani wao hawawezi kusimamia wala kudai haki zao kisheria, pamoja na kutojua ama kuona wapi wananyanyaswa.

Mkurugenzi huyo alifahamisha kuwa, Kituo cha huduma za sheria Zanzibar ZLSC, kwa mashirikiano mazuri na Save the Children vimekuwa vikifanya kazi bega kwa bega katika kusaidia masuala ya watoto chini ya msaada wa Wizara ya Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto katika kusimamia masuala mazima ya kutetea maslahi ya mtoto.

Nae Mwakilishi kutoka Save the Children Mubbarak Maman, alisema taifa la Tanzania linahitaji kujipanga zaidi katika kuzungumzia masuala ya watoto, kwani matatizo yanayowakumba watoto ni mengi na yanahitaji kutumia juhudi na maarifa makubwa yenye kukubalika kisheria katika kupambana na masuala ya udhalilishaji watoto.

Alisema kwamba juhudi hizo hazitofanikiwa kama hakutokuwa na mikakati madhubuti pamoja na kujitolea kwa kutetea haki za watoto na kuangalia mambo yanayowakandamiza watoto kwa kuyachukulia sheria zinazofaa.

Mubbarak aliongeza kuwa Watanzania bara na visiwani wanahitaji kujipanga katika masuala mazima ya kumlinda mtoto kabla ya kuzungumzia masuala yanayowahusu watoto na badala yake kuyachukulia hatua za kisheria na kutoa mwamko kwa jamii ili kupambana nayo na kuyapinga kwa nguvu zote.

Mapema akiwasilisha mada katika mafunzo hayo, Mkufunzi kutoka Chuo Kikuu cha Tunguu, Ali Uki, akizitaja haki za watoto ni pamoja na kutopata mateso ya kimwili na akili, kutoumizwa, kutonyanyaswa, kutoharauliwa, kutofanyishwa kazi kwa maslahi ya mtu mwengine ikiwemo ngono.

Mafunzo hayo ya siku moja yaliwashirikisha wajumbe wa Baraza la wawakilishi ambapo mafunzo hayo yalifadhiliwa na kituo cha huduma za sheria na Save the Children.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.