Habari za Punde

Dk Shein afungua msikiti wa Ijumaa Kiboje Mwembeshauri

 Rais wa zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein,akisalimiana na Mufti wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi,pamoja na viongozi wengine alipowasili katika Msikiti wa Ijumaa Masjid Hudda wa Kiboje Mwembeshauri Wilaya ya Kati Unguja
 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein,(wa pili kulia) akikata utepe kama ishara ya kuufungua Msikiti wa Ijumaa Masjid Lhudda wa Kiboje Mwembeshauri,Wilaya ya Kati Unguja leo, (wa kwanza kulia) Mufti wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi,
 Rais wa zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein,akikaribishwa kwa Qasida wakati alipowasili katika Msikiti wa Ijumaa Masjid Hudda wa Kiboje Mwembeshauri Wilaya ya Kati Unguja.
 Rais wa zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein,akitoa nasaha zake mbele ya waumini wa Dini ya Kiislamu wakati wa sherehe ya ufunguzi wa Msikiti wa Ijumaa Masjid lhudda wa Kiboje Mwembeshauri Wilaya ya Kati Unguja jana.
Miongoni mwa Viongozi waliohudhuria katika hafla ya Ufunguzi wa Msikiti wa Ijumaa Masjid hudda,wa Kiboje Mwembeshauri,Wilaya ya Kati Unguja uliofunguliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein (Picha na Ramadhani Othman Ikulu )

Na Rajab Mkasaba

WAUMINI wa dini ya Kiislamu wametakiwa kuongeza jitihada zao katika ibada za sala za faradhi, sunna, sala za jamaa, kusoma sana Quran na kusaidiana katika mambo ya kheri yakiwemo kuwasaidia masikini na mayatima hasa katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhan.

 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein alimetoa wito huo leo huko Kiboje Mwembeshauri katika ufunguzi wa msikiti wa Ijumaa (Masjid Huddah), hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbali mbali wa dini, vyama vya siasa, serikali na wananchi.

 Alhaj Dk. Shein alisema kuwa Uislamu unafunza utukufu wa mwezi wa Ramadhan kupitia kitabu cha Quran Karim na sunna za Bwana Mtume (SAW), ambapo amali za waja wanaofanya ibada katika mwezi huu huwa ni bora zaidi kuliko miezi mengine.



 Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa Utamaduni wa Zanzibnar wakati wa mwezi wa Ramadhan ni kula pamoja na vile vile majirani kupelekeana chakula cha tunu miongoni mwa futari zao mambo ambayo huzidisha mapenzi na uhusiano mwema miongini mwao.

 “Bwana Mtume (SAW) alisisitiza umuhimu wa kuishi vyema na majirani katika hadithi iliyopokelewa na Al-Bukhaariy kwa kusema ‘ Mwenye Kumuamini Allah na siku ya mwisho, basi na amkirimu jirani yake”,alisema Alhaj Dk. Shein.

 Aidha, Alhaj Dk. Shein alisema kuwa ujenzi wa misikiti na madrasa ni namna moja ya kuimarisha dini ya Kiislamu ambapo jambo lililo muhimu zaidi ni kuimarisha matumizi ya majengo hayo.

 Alhaj Dk. Shein alisema kuwa misikiti ina matumizi mbali mbali katika jamii ya Kiislamu mbali na kusali pia, hutumika kwa kusomeshea darsa, kufanyia harusi, kusoma halili, kukaa itikafu, kufanyia majadala ya kidini na mambo mbali mbali ya kijamii yanayohitaji fatwa.

 Pamoja na hayo, Dk. Shein alitoa nasaha zake wa wananchi na Waislamu wa Kiboje wote kwa jumla kuimarisha matumizi ya misikiti kwa shughuli mbali mbali kwa mujibu wa mafundisho ya Bwana Mtume (SAW) na kuipa misikiti hadhi inayostahiki.

 Alhaj Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa shukurani zake kwa wananchi wa Kiboje na maeneo yote ya karibu kwa namna walivyojitahidi kuzitumia fursa zilizotolewa na serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuimarisha sekta ya kilimo.

 Alisema kuwa anaelewa changamoto zilizojitokeza na kwa zile ambazo ziko ndani ya uwezo wa Serikali, jitihada zitafanywa ili kuzipunguza kama sio kuziondoa kabisa. Aliwasihi wananchi wa Kiboje kuendelea na jitihada zao katika kilimo cha chakula sanjari na kutumia fursa za kupata miche ya miti ya matunda na ushauri kutoka kwa wataalamu wa kilimo na misitu.

 Sambamba na hayo, Alhaj Dk. Shein alisema kuwa anaelewa kuwa wizi wa mazao umeenea na unawavunja moyo wakulima na kutoa wito kwa Jeshi la Polisi, Masheha na vijanawa ulinzi shirikishi kwa pamoja washirikiane kukabiliana na wakorofi hawa wa wizi wa mazao.

 Alhaj Dk. Shein alisema kuwa anaelewa kuwa tatizo la kutowadhibiti kisheria linawaudhi sana wakulima na kwa hakika linawakatisha tamaa kwani wengi wao wanajulikana. Alisisitiza kwua kuna wajibu wa kuendelea kulima na kufanya kazi nyengine za halali na Serikali itaendelea kufanya bidii kuwasaidia wakulima katika suala hilo na kueleza kuwa wezi wa mazao wanakwenda kinyume na maelekezo ya Mwenyezi Mungu na hawana budi kurejea kwake.

 Dk. Shein pia, aliwakumbusha wamini na wananchi wa Kiboje kufahamu kuwa wana wajibu mkubwa wa kusimamia malezi na maadili mema ya watoto kwani malezi mema na maadili yanatokana na mafundisho ya dini ya Kiislamu yana mchango mkubwa katika kuwatayarisha watoto kuwa wacha Mungu na wenye misingi imara ya Uislamu.

 Nao wananchi na Waumini wa dini ya Kiislamu wa Kiboje walieleza kwua hatua hiyo ya ujenzi inatokana na jitihada mbali mbali za kuuimarisha msikiti huo kutoka kwa wananchi wenywe, viongozi mbali mbali na Waislamu wengine walioamua kusaidia.

 Waumini hao walieleza kuwa eneo lililojengwa msikiti huo ulikuwepo msikiti mdogo ambao ulijengwa zaidi ya miaka thamanini (80) iliyopita ambao ulitosha kusaliwa kwa wakati huo na kueleza kuwa ujenzi wa msikiti huo mpya ulianza mwaka 2009. Kwa maelezo ya risala hiyo ya Waumini hao gharama za ujenzi na zana za msikiti huo mpya uliofunguliwa leo ni shilingi milioni 41 na kuwashukuru wale wote waliochangia.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.