Habari za Punde

SMZ haiwezi kurejesha ‘kick boxing’. Huko ni kupuuza fikra za mzee Karume

Na Mwantanga Ame
SERIKALI ya Zanzibar, imesema itaendelea kupiga marufuku mchezo wa kick boxing, kwani kuruhusu uchezwe humu visiwani, ni kukiuka mawazo ya Rais wa kwanza wa Zanzibar, marehemu Abeid Amani Karume.

Akijibu hoja za wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wakati wakichangia bajeti ya wizara hiyo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Said Ali Mbarouk, alisema wizara yake haiwezi kwenda kinyume na amri ya muasisi wa nchi ya Zanzibar kwa kuruhusu vijana wake kucheza mchezo huo au ule wa masumbwi (boxing).

“Wananchi wa Zanzibar waliahidi kulinda na kutekeleza fikra za mzee Karume. Kuwaachia wacheze kick boxing, itakuwa kuzipinga fikra za muasisi huyo”.

Alifafanua kuwa, kiapo cha Chama cha Afro Shirazi (ASP) baada ya kifo cha mzee Karume, ni kwa wananchi kulinda na kutekeleza fikra, busara na maazimio yake, hivyo si busara kuwaletea mchezo huo”, alisisitiza.

“Tukiamua kuurejesha mchezo huu hatutakuwa tunamtendea haki mzee Karume huko aliko. Akifufuka na kukuta tunapigana hatatuelewa, tuzienzi fikra zake kama kiapo cha chetu kinavyosema”, alieleza Waziri huyo.

Kwa upande mwengine, alikiri kuwa uwanja wa Amaan uko katika hali mbaya kutokana na kukauka majani katika eneo la kuchezea (pitch), lakini akasema wizara yake inajiandaa kutafuta njia za kuufanyia matengenezo.

Amesema katika hatua ya kwanza ambayo tayari imechukuliwa, ni kufanya mazungumzo na mwakilishi wa Shirikisho Soka Duniani (FIFA) aliyekuwepo Zanzibar hivi karibuni, kuona vipi watalifanyia kazi tatizo hilo, kwa kushirikiana na Chama cha Soka Zanzibar, (ZFA).

Hata hivyo, alisema tatizo kubwa linalukabili uwnaja huo kwa sasa, ni ukosefu wa maji, kwani kisima cha awali kilichochimbwa uwanjani hapo, hakikuwa na maji, na sasa sa wanatafuta njia nyengine ya kuweza kupatikana kwa maji katika kiwanja hicho.

Akizungumzia juu ya hoja zinazohusu utamaduni Waziri huyo alisema wizara hiyo kupitia taasisi husika itaendelea kuona inasimamia utamaduni wa Zanzibar pamoja na sanaa ikiwa pamoja na kusimamia maadili ya Mzanzibari.

Nae Waziri wa Nchi Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed, akizungumzia juu ya umuhimu wa kuwepo kwa viwanja vya kufurahishia watoto alisema tayari hivi sasa imo katika hatua ya kulifanyia kazi suala hilo kwa kukijenga kiwanja cha kufurahishia watoto kariakoo baada ya kukabidhiwa chini ya mikono ya ZSSF.

2 comments:

  1. Sawa sawa Mheshimiwa Waziri, kwani michezo yote iliyopo ulimwenguni ya kucheza ni lazima tutiane mangumi!; Wazanzibari ni watu wastaarabu bwanaa na Karume Senior aliliona hilo. No, kwa michezo ya kutoana sura...

    ReplyDelete
  2. Tuache utumwa wa historia!...tusimuelewe vibaya yule mzee, tuangalia lengo lake la kukataa mchezo huo lilikua nini.

    Kuelewa vibaya baadhi ya hekma za mzee Karume kumetuletea maafa makubwa visiwani, mpaka leo watu hawataki kulipia baadhi ya huduma kama vile maji , elimu nk..sababu mzee karume alisema itakuwa bure ..tuache hizooo!!!

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.