Uongozi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) umeamua kuwasimamisha kufanya mitihani wanafunzi wote wanaomaliza masomo yao mwaka huu ambao hawajakamilisha ada ya chuo hadi itakapofika tarehe 22 mwezi huu ambapo mitihani hiyo itaanza.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano wa pamoja kati ya uongozi wa chuo na uongozi wa wanafunzi kwenye Makao Makuu ya chuo hicho Vuga, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha SUZA Professa Idriss Ahmad Rai amesema wanafunzi wanaoendelea na masomo wa mwaka wa kwanza na wa pili hawatahusika na hatua hiyo na wameruhusiwa kufanya mitihani baada ya kujaza mkataba maalum.
Amesema mkataba huo utawalazimisha wanafunzi kulipa malimbikizo ya ada wanayodaiwa kabla ya kuanza muhula mpya wa masomo mwezi Oktoba na watakaoshindwa kulipa hawataruhusiwa kuendelea na masomo yao.
Hata hivyo amesema wanafunzi watakaoshindwa kuanza mitihani tarehe 22 watapewa nafasi ya kufanya mitihani wakati wa mitihani ya marejeo lakini kwa upande wao utakuwa ndio mtihani wa kawaida iwapo watalipa madeni yao.
Professa Rai amesema SUZA imefanya uwamuzi huo mzito kutokana na wanafunzi wengi kushindwa kulipa ada zao na hivi sasa wanawadai kiasi cha shilingi 270 milioni.
‘Zaidi ya wanafunzi 850 hawajalipa ada baadhi yao wamelipa nusu na wengine hawajalipa kabisa na uzoefu unaonyesha baada ya wanafunzi kumaliza mitihani ya mwisho wanakuwa wagumu kukamilisha malipo yao hivyo tumeamuwa kuwabana kabisa’ alisema Professa Rai.
Amesema lengo la chuo siyo kuwakomoa wanafunzi lakini ni njia ya kuhakikisha wanapata fedha ambazo ni muhimu katika kukiendeleza chuo hicho pamoja na ruzuku inayotolewa na Serikali.
Ameongeza kuwa wanaelewa ugumu wa maisha unaowakabili wanafunzi wengi hasa katika kipindi hiki cha mwezi wa Ramadhani na kuelekea siku
kuu wiki ijayo lakini hakuna njia ya mkato ya kupata mapato na amewataka wazazi kulielewa suala hilo na kuwapa ushirikiano mkubwa watoto wao katika maendeleo yao ya elimu.
Katika mkutano wa uongozi wa chuo na uongozi wa wanafunzi, wanafunzi waliomba waruhusiwe kufanya mitihani na wale ambao hawatalipa malimbikizo ya madeni yao wasipewe matokeo mpaka pale watakapo kamilisha ada zao.
IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR 15.08.2012
No comments:
Post a Comment