Habari za Punde

Watatu Wateuliwa kinyan'ganyiro cha Uwakilishi Jimbo la Bububu

 Na Juma Mohammed,MAELEZO Zanzibar 

Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi imejadili majina ya wanachama watatu wanaowania kuteuliwa na Chama hicho kwa ajili ya kinya’nganyiro cha Uchaguzi mdogo wa Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi Jimbo la Bububu.

 Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Ofisi ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, ilisema kwamba kikao hicho kimependekeza kwa Kamati Kuu ya CCM majina ya Husein Ibrahim Makungu (Bhaa), Omar Ibrahim Kilupi na Fatma Salim Said. 

 “Kikao kilipokea na kujadili majina ya wana CCM 3 walioongoza katika kura za maoni kwenye mkutano mkuu maalum wa Matawi ya Jimbo la Bububu na hatimaye kutoa mapendekezo yake kwa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, kwa hatua za mwisho” Ilisema taarifa hiyo ya CCM. 


 Katika hatua nyengine, Kamati Maalum imempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein, kwa kusimamia vizuri kazi ya uokoaji katika ajali ya kuzama kwa Meli ya Skagit, iliyozama Julai 18 karibu na Kisiwa cha Chumbe Kusini mwa Kisiwa cha Yasin. 

 Katika ajali hiyo, watu 150 waliokolewa wakiwa hai huku wengine zaidi ya mia moja wakipoteza maisha. Meli ya Mv. Skagit ilibeba abiria 290 ikitokea Bandari ya Dar es Salaam kuelekea Bandari ya Malindi Zanzibar,ilizama majira ya saa saba mchana. 

 Wajumbe wa Kamati Maalum pia wamempongeza Rais Dk. Shein, kwa hatua aliyochukua ya kuiangiza Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Fedha Uchumi na Mipango ya Maendeleo kuhakikisha inatafuta fedha haraka kwa ajili ya kuanunua meli ya abiria na mizigo.

 “Kikao pia kimempongeza Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein, kwa hatua aliyochukua ya kumuagiza Waziri wa Fedha wa Serikali (SMZ), kutafuta fedha haraka iwezokanavyo, kwa ajili ya ununuzi wa meli mpya ya kubebea abiria na hivyo kuwaondolea wananchi tatizo la usafiri wa majini lililodumu kwa muda mrefu sasa” Ilisema taarifa hiyo ya CCM Zanzíbar. 

 Aidha, Kamati Maalum imefarijika na hatua ya Rais Dk. Shein kuagiza ununuzi wa meli mpya ambayo itasaidia kuondoa tatizo la usafiri na usafirishaji kwa wananchi. “Kikao kimesema kauli hiyo ya Mhe. Rais wa Zanzibar ya kutafuta meli sio tu ni ya kijasiri, bali pia imetolewa wakati muafaka, ambapo Serikali imethubutu kupunguza kutoka Bajeti yake ya mwaka 2012/2013, jumla ya Tshs. Bilioni 17, ikiwa ni kianzio cha fedha za kununulia meli hiyo” Iliongeza taarifa hiyo ya CCM.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.