Habari za Punde

Zanzibar ina mengi ya kujifunza kutoka Indonesia - Dk Shein

Na Rajab Mkasaba, Ikulu

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, ameeleza kuwa Zanzibar ina mengi ya kujifunza kutoka Indonesia ikiwa ni pamoja na kuimarisha mashirikiano ya muda mrefu katika sekta ya biashara hasa katika zao la karafuu. 

Dk. Shein aliyasema hayo wakati alipokuwa na mazungumzo na Balozia wa Indonesia nchini Tanzania Mhe. Yudhistiranto Sungadi, aliyefika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya kumuaga Rais baada ya kumaliza muda wake wa kazi nchini Tanzania. 

 Katika maelezo yake,Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa Zanzibar ina historia ya muda mrefu ya mahusiano na mashirikiano mazuri kati yake na Indonesia katika kushirikiana kwenye sekta za maendeleo ikiwemo sekta ya biashara hasa ya zao la karafuu. 

 Dk. Shein alisema kuwa ipo haja ya kuimarisha zaidi uhusiano na aushirikiano huo katika sekta hiyo pamoja na sekta nyengine kwa manufaa ya pande zote mbili. Dk. Shein alisema kuwa licha ya kuzidisha mashirikiano katika biashara ya zao la karafuu pia kuna haja ya mashirikiano ya pamoja katika bidhaa nyenginezo hasa zitokanazo na zao hilo kutokana na Indonesia kupiga hatua katika uzalishaji wa bidhaa kadhaa zitokanazo na karafuu. 


 Pamoja na hayo, Dk. Shein alimueleza balozi huyo kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imo katika mikakati maalum katika kuimarisha sekta ya kilimo hasa kilimo cha umwagiliaji maji kutokana na umuhimu wa kilimo hicho hasa kwa wakati huu uliopo. 

 Mbali ya hayo, Dk. Shein pia, aligusia umuhimu wa kuwepo mashirikiano katika kilimo hicho cha karafuu na namna ya kuzitayarisha kwa lengo la kuzalisha bidhaa nyengine pamoja na kuendeleza kilimocha mazao mbali mbali ya chakula na matunda Dk. Shein alieleza kuwa miongoni mwa juhudi hizo zinazochukuliwa na serikali ni pamoja na kuimarisha utafiti katika sekta hiyo ya kilimo na kueleza kuwa ipo haja kwa Indonesia ikashirikiana na Zanzibar katika suala zima la utafiti. 

 Pamoja na hayo, Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa mbali ya mashirikiano katika tafiti pia, ipo haja ya katika kuendeleza mashirikiano katika mafunzo hasa kwenye sekta hiyo ya kilimo na sekta nyenginezo. 

Akizungumzia kuhusu mashirikiano kwenye sekta ya elimu, Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar tayari imo katika mikakati madhubuti ya kuimarisha sekta ya elimu hasa elimu ya juu ambapo hivi sasa kumekuwepo vyuo vikuu kadhaa kikiwemo Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), ambapo alisema kuwa iwapo kutakuwa na mashirikiano mazuri na Taasisi za elimu ya juu za nchi hiyo mafanikio makubwa yanaweza kupatikana. 

 Pia, Dk. Shein alieleza juhudi zilizochukuwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuimarisha na kuendeleza vyuo vya amali Unguja na Pemba huku akisisitiza haja ya kuongezwa ili viwe vingi zaidi na kuweza kutoa elimu ya amali kwa vijana kwa lengo la kupanua soko la ajira. 

 Pamoja na hayo, Dk. Shein alimueleza balozi huyo juhudi zinazochukuliwa na serikali anayoiongoza katika kuimarisha sekta za utalii, na ile ya uvuvi na mikakati iliyowekwa katika kuendeleza uvuvi hasa wa bahari kuu huku akiwakaribisha wawekezaji kutoka nchi hiyo kuja kuekeza Zanzibar pamoja na kuwepo mashirikiano ya pamoja katika kuimarisha sekta hizo. 

 Nae Balozi Sungadi alimueleza Dk. Shein kuwa Indonesia inajivunia uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu kati yake na Zanzibar ambao ni wa muda mferu na umeweza kuimarika hadi hivi sasa kwa lengo la kuimarisha sekta za maendeleo kwa pande zote mbili. 

 Balozi Sungadi alitoa shukurani kwa Dk. Shein kwa kuendelea kuiimarisha uhusiano na mashirikiano hayo kati ya Zanzibar na Indonehia huku akitoa pongezi kwa Dk. Shein kwa kuendeleza kusimia amani na utulivu hapa nchini. 

 Katika maelezo yake, Balozi hiyo wa Indonesia alisema kuwa licha ya yeye kumaliza muda wake lakini nchi yake itaendelea kushirikiana na Zanzibar pamoja na kuendelea kuiunga mkono katika kuimarisha sekta mbali mbali za maendeleo ikiwemo ushirikiano wa kibiashara, elimu, kilimo na nyengienezo. 

 Pia, Balozi huyo alielezea aushirikiano wa kimasomo ambapo nchi yake imewapatia vijana wa Zanzibar nafasi za masomo ya Degree ya kwanza na ya Pili katika sekta ya kilimo cha umwagiliaji pamoja na elimu ya Biashara. 

 Wakati huo huo, Rais Dk. Shein alifanya mazungumzo na Balozi wa Jumuiya ya Ulaya (EU) Mhe. Filiberto Seriani Sebregondi, huko Ikulu mjini Zanzibar. Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein alitoa shukurani kwa Jumuiya hiyo kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kumarisha sekta mbali mbali za maendeleo. 

Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa Zanzibar inathamini sana misaada ya Jumuiya hiyo ya Ulaya kwani imeweza kusaidia katika kuendeleza sekta kadhaa za maendeleo hapa nchini. 

 Nae Balozi Sebregondi alimueleza Dk. Shein kuwa EU, itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuendeleza na kuimarisha sekta zake za maendeleo kutokana na kuthamini juhudi kubwa zinazochukuliwa na viongozi pamoja na wananchi wa Zanzibar katika kujiletea maendeleo endelevu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.