Habari za Punde

Balozi Seif kuinua michezo Kitope

Na Othman Khamis, OMPR
UONGOZI wa Jimbo la Kitope, unakusudia kuimarisha sekta ya michezo kwa lengo la kuwawezesha vijana wa jimbo hilo kuwa pamoja katika harakati za kimichezo na kijamii.
Mbunge wa Jimbo hilo Balozi Seif Ali Iddi amesema hayo mara baada ya kusikiliza matatizo na ushauri wa wanamichezo wa timu nne zilizomo jimboni humo, katika kikao chao kilichofanyika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Tawi la CCM Kitope A.

Balozi Seif aliwaeleza wawakilishi wa timu hizo ambazo ni Kitope United, African Boys, Home Boys na Kombora, kuwa uamuzi wao wa kufikiria kuanzisha timu moja imara ya jimbo ni faraja  kwa viongozi, na kwamba utarahisisha  upatikanaji wa vifaa na misaada kwa wepesi zaidi.

Aliahidi, kwa kuwa yeye ni kiongozi wao wa jimbo, atahakikisha sekta ya michezo inapata nguvu zaidi kutokana na umuhimu wake  uliojichomoza hivi karibuni wa kutoa ajira endapo vijana hao watajituma vilivyo.
Aidha aliahidi kuzungumza  na wafadhili mbalimbali wa michezo, ili kuona namna gani wanaweza kusaidia uimarishaji wa uwanja wa uhakika na wa kisasa ndani ya jimbo hilo.

Alisema suala hilo litakwenda sambamba na  upatikanaji wa vifaa vya michezo ikiwemo mipira, nyavu, magoli na jezi ambazo alisema zimo ndani ya uwezo wake kulingana na utaratibu aliokwishauanzisha tokea alipoanza kuliongoza jimbo hilo.
Aliwataka kuanza maandalizi ya msingi kwa ajili ya ujenzi wa jingo la klabu, na kusema  atahakikisha anasaidia nguvu za unyanyuaji jengo kwa hatua ya matofali na kuangalia mbinu za kuendeleza ujenzi huo.

Mapema wanamichezo hao walimueleza Balozi Seif  matatizo yanayowakabili katika katika harakati zao za kuendeleza michezo ambayo yamekuwa yakipunguza kasi yao ya ufanisi, ikiwa ni pamoja na uhaba wa vifaa vya michezo, ujenzi wa jengo la klabu pamoja na uanzishwaji wa mashindano ya Kombe la Mbunge.
Katika kikao hicho, Balozi Seif Ali Iddi alikabidhi seti ya jezi na fedha taslimu kwa timu ya soka ya Kitope United  inayojiandaa na usajili kwa ajili ya mashindano yajayo.

 

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.