Habari za Punde

Pingamizi za wachezaji zaikaba TFF

Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
KAMATI ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), juzi ilishindwa kuamua mustakbali wa wachezaji waliowekewa pingamizi katika usajili wao kwa ajili ya kucheza ligi kuu ya soka Tanzania Bara msimu ujao.
Kamati hiyo iliyokuwa chini ya Mwenyekiti wake Alex Mgongolwa, sasa imeamua leo saa 6:00 mchana kukutana na viongozi wa klabu zilizoweka na kuwekewa pingamizi tu katika ofisi za TFF jijini Dar es Salaam.
Habari za ndani kutoka TFF, zimesema, kufuatia mkutano wa juzi kutwa hadi usiku,  kumalizika bila kupata suluhisho la pingamizi hizo, sasa shirikisho hilo limeamua kutumia busara ya kuzikutanisha pande zinazopingana kujaribu kupata suluhu.
Katika pingamizi hizo, Azam inapinga usajili wa Ramadhan Chombo ‘Redondo’ kwenda Simba, huku ikidai dola za Kimarekani 50,000 ingawa Simba wamefika dola 20,000 ambazo pia wameomba kulipa kwa awamu.
Habari zaidi zinasema kwamba, Simba nayo inataka dola 60,000 kutoka kwa Yanga, ili wawauzie beki Kevin Yondan, ikipinga usajili wake Yanga kwa maelezo kuwa ina mkataba naye uliosainiwa Desemba 23 mwaka jana.
Vilevile Simba imewasilisha malalamiko ya mchezo usio wa kiungwana katika usajili wa Mbuyu Twite aliyeko Yanga kwa maelezo alisaini mkataba na klabu yao Agosti Mosi mwaka huu mbele yao, viongozi wa Shirikisho la Soka Rwanda (FERWAFA) na APR na kulipwa jumla ya dola 32,000.
Nayo Yanga inapinga Simba kuwaacha wachezaji Dan Mrwanda, Haruna Shamte, Kanu Mbiyavanga na Lino Masombo kwa maelezo walishapatiwa leseni za kucheza Ligi ya Tanzania walizozitumia kwenye mashindano ya Kombe la Kagame.

Mbali na malalamiko hayo na mengine mengi, mabingwa wa Zanzibar timu ya

Super Falcon, inapinga wachezaji wake wanne; Edward Christopher Shija, Samir Said Luhava (Simba), Robert Joseph Mkhotya (African Lyon) na Sultan Juma Shija (Coastal Union) kusajiliwa katika timu hizo kwa maelezo taratibu halali za uhamisho hazikufuatwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.