Habari za Punde

Bunduki za Arsenal zafyatukia Anfield

 Risasi mbili Liverpool chali
Lukas Podolski, right, celebrates his first Arsenal goal with Santi Cazorla, who also netted
Lucas Podolski akishangilia pamoja na Cazorla baada ya kufunga goli la kwanza dhidi ya Liverpool huko Anfield.

LONDON, Uingereza

BAADA ya kuanza ligi kuu ya Uingereza kwa mdudu wa sare, jana Arsenal ilizinduka kutoka usingizini na kuilaza Liverpool mabao 2-0 na kurudisha furaha ya mashabiki wake na kocha Arsen Wenger.
 
Ushindi huo, umempa matumaini mapya Mfaransa Arsen Wenger, ambaye mapema alikaririwa akiwaonya wale wanaokibeza kikosi chake, akisema timu hiyo itafufuka na kuzishangaza timu nyengine.
 
Timu zote ziliuanza mchezo taratibu huku kila moja ikifanya mashambulizi ya kushtukiza ambayo hata hivyo hayakuwa na hatari kubwa milangoni.
 
Baada ya kupita nusu saa, Arsenal ikaanza kucheka na nyavu kwa bao lililofungwa na Lucas Podolski mnamo dakika ya 31.

Mjerumani huyo alifunga kufuatia kazi nzuri ya Santi Cazorla aliyekatisha nusu ya uwanja upande wa Liverpool na kummegea Podolski pasi murua, na yeye kuaachia shuti la chinichini lililompita kilaini mlinda mlango Pepe Reina.
 
Bao hilo lilidumu hadi wakati wa mapumziko, ingawa wachezaji wa Liverpool walijaribu kutaka kulichomoa, lakini mashabulizi ya akina Steven Gerrard yalikumbana na ukuta mgumu wa washika bunduki hao.
 
Kipindi cha pili kilianza huku kila upande ukihaha kutafuta bao, Arsenal ikitaka kuongeza na Liverpool kusawazisha, hali iliyoiweka milango ya timu hizo katika wakati mgumu.
 
Mnamo dakika ya 68, Podoski naye alilipa fadhila, kwa kumtengenezea pasi nzuri Cazorla, na kiungo huyo akampiga tobo golikipa wa  Liverpool Pepe Reina, ambaye aligeuka akiushindikiza mpira kwa macho ukijaa nyavuni
 
Makosa hayo ya Reina, yalizidisha machungu wa mwanzo mbaya wa kocha mpya wa wekundu hao  Brendan Rodgers, ambaye bado hajaonja ushndi katika ligi akiwa na timu yake hiyo katika michezo mitatu iliyokwishacheza.
 
Meneja huyo inasemekana amevunjwa moyo kwa kuwapoteza nyota nguli Andy Carroll na Charlie Adam mwishoni mwa msimu wa uhamisho wa kiangazi bila timu hiyo kusajili wachezaji mbadala.
Katika mechi zilizotangulia, Liverpool ilifungwa mabao 3-0 na West Bromwich, kabla kulazimisha sare ya 2-2 dhidi ya mabingwa watetezi Manchester City.
 
Nayo Aresnal ilianza msimu kwa sare ya kutokufungana na Sunderland, na matokeo kama hayo yakajiri tena katika mechi yake ya pili dhidi ya Stoke City, na sasa imefikisha pointi tano katika msimamo wa ligi hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.