Habari za Punde

Msaada kutoka Canada kwa watoto Nairat na dada yake

IMG_4563
Wazanzibari wanaoishi Canada ambao wanajumuika pamoja chini ya Jumuia yao ijulikanayo kama ZACADIA (Zanzibar-Canadian Diaspora Association) wameshitushwa na kusikitishwa na hali ya kiafya ya mtoto Nairat na dada yake pamoja na familia yao nzima kwa ujumla - kama walivyosoma huko nyuma kwenye ukumbi huu MZALENDO<http://www.mzalendo.net/matangazo/nawaombeni-msaada-na-mola-atawalipa>.
Kutokana na hali hiyo mbaya ya kiafya ya watoto hao, ZACADIAkatika kusaidia matibabu ya Nairat na dada yake inatoa mchango wake wa TShs 750,014.04.

ZACADIAinatoa shukrani za dhati kwa wale wote walioitikia wito wa kumchangia mototo wetu Nairat na dada yake. Misaada yenu inawasubiri siku ya hesabu ili kuwasaidia na nyinyi. Jumla ya dola 490.03 zimepatikana kwa upande wa Toronto na GTA yote kwa jumla.

Pesa hizo zimepelekwa Zanzibar tarehe 21 September, 2012 kutoka Canada kwa njia ya MONEYGRAM, kupitia kwa Bi. Salma Said ambaye ni mdhamini wa hawa watoto kwa hivi sasa.
Kwa niaba ya Wana-Zacadia wote waishio Canada tunamtakia mtoto Nairat pamoja na dada yake Bishambe, shifaa ya haraka na kwa wakati huo huo tunaitakia Zanzibar kila mafanikio katika wakati huu mgumu wa kiuchumi kwa Ulimwengu mzima.

Kila la kheri.

Hassan Othman
Katibu / ZACADIA
(Toronto, Canada).

Asalamu Alaykum.

Kwanza sina budi kumshukuru Mwenyeenzi Mungu Mtukufu kwa kunijaali hali ya uzima mimi na watoto wangu Nairat na Bisambe kuwa hawajambo na wapo katika hali ya afya njema na wakiendelea na matibabu yao kama kawaida huko Jijini Dar es Salaam.

Pili napenda sana kutoa shukrani zangu za dhati kabisa kwa uongozi mzima wa Wazanzibari tunaoishi Canada chini ya Jumuia ya Zanzibar-Canadian Diaspora Association (ZACADIA) kwa kutoa fedha za mchango wa shilingi750,014.04 ambazo zimekuja kwa njia ya m/ gram na tayari nimeshakwenda kuzichukua.

Kwa niaba yangu niaba ya Sheikh Hassan Mussa wa UK na kwa niaba ya mama wa Nairat na Bisambe ambaye ni Bi Khadija Mohammed tunasema tunatoa shukrani kubwa sana kwa nyinyi kuonesha mfano huu katika kutoa fedha kwa ajili ya matibabu ya watoto hawa Shukran na malipo ya kheri hii yatatoka kwake mwenyewe Mwenyeenzi Mungu (s.w) ambaye tunamtegemea sote katika kila jambo.


Shukrani zetu sio kutoa mchango tu bali hata kuonesha uzalendo mkubwa ni jambo muhimu sana kwetu kwani kitendo mlichofanya ZACADIA cha kushirikiana na kutoa michango hii ni cha kuigwa na wengine katika nchi zinazofuata, Sote tunakumbuka alipokuwa hai Marehemu Dk Yussuf Salim wa Denmark alivyokuwa akichukua uamuzi wa haraka haraka wakati mwengine bila ya kuwashauri wenzake na hilo hakuwa akilifanya kwa kujionesha bali alikuwa akifanya kwa kuonesha uzalendo na mapenzi ya jamii ya nchi yake. Ni jambo zuri ambalo linapaswa kuigwa na nchi nyengine na wazanzibari wengine.

ZACADIA mlichofanya ni kitu muhimu sana cha kujikusanya na kuona umuhimu wa kuisadia jamii yenu mlioiwacha nyumbani, na bila ya shaka jambo hili litatoa matunda mazuri kwani kuonesha umoja peke yake ni jambo kubwa na hivyo hatua hii itachangia wengine kuiga mfano huu mzuri lakini pia serikali ambayo ina jukumu hili la kuhakikishia afya njema wananchi wake inaweza kupata moyo inapoona wananchi wake wanachukua majukumu kama haya na kuyasimamia hadi kufikia kikomo kwani tukumbuke kwamba serikali haiwezi kufanya kila kitu lakini ikiwa sisi wananchi tutasaidia jamii yetu basi sio kuipa somo tu serikali bali tutakuwa tunaikumbusha kwamba kuna hiki na kile kimekosekana katika jamii na kinahitajika kwa maana hiyo basi tutakuwa tumeisaidia serikali katika kutekeleza majukumu yake.


Hakuna jambo muhimu kama umoja na tukiwa mahodari wa kuwa wamoja na kusaidiana basi tutakapofikwa na jambo zito na kubwa inakuwa rakhisi sana kutatua kwa haraka kwani kwa kuwa tuna umoja, khasa kwa kuzingatia umoja ni nguvu hivyo basi napenda nitoe wito wangu kwa wengine kwamba suala la kujitolea tulione kama ni jukumu letu sote na sio taasisi moja au mtu mmoja, kila mmoja wetu achukulie jukumu hili kwamba linamkhusu na kwa kuzingatia kwamba kazi kama hizo za kujitolea zinahitaji ustahamilivu na busara kubwa na za hali ya juu na hivyo basi ikiwa wengine hawana fedha basi wachangie kwa kutoa ushauri mzuri wa mawazo au ushauri wa kimatibabu na hata ushauri wa lugha ya upole pia inasaidia sana kutoa faraja kwa wagonjwa na hata wale wenye kushughulikia wagonjwa.

Kwa mara nyengine tena nisema ahsanteni sana kwa kuliona hili na kujikusanya kwa kuhamasishana na kutoa mchango huu wa fedha kwa ajili ya matibabu ya watoto wetu hawa Nairat na Bisambe ambao wote kwa sasa bado wapo Dar es Salaam wakimaliziwa kupata matibabu.

Na inashaallah tunatarajia wiki hii kuwa watarejea Zanzibar baada ya kupata matibabu ya awali ambapo wanatakiwa kutumia dawa kwa muda wa miezi mitatu na kisha kurudi tena hospitali kwa uchunguzi mwengine. tunawataki kheri na mafanikio katika hilo inshallah.

Inshaallah tutakuwa tunajulishana katika kila hatua na kuhusu matumizi ya fedha kwa wale ambao watapenda kutazama orodha ya fedha nilitangulia kuelezea huko katika email zilizotangulia na nilichapisha baadhi ya vyeti na risiti za matumizi na idadi ya fedha nilizotumia kwa ajili ya kuweka uwazi katika matumizi ya fedha ambazo mimi ndio dhamana. Fedha zote zilizotolewa kwa ajili ya matibabu ya Nairat na Bisambe jumla ni shilingi millioni nne na nusu na tayari baadhi yake zimeshatumika lakini hesabu zote zipo pamoja na risiti zake.

Hapa naomba kusisitiza kwamba kutoa hesabu ya fedha tulizopokea au tulizotumia sio kwa ajili ya kujionesha bali ni kwa kuweka uwazi wa matumizi kwa wale waliotoa michango yao. Na nikiwa kama msimamizi mkuu wa suala hili naahidi kusimamia vyema matumizi ya matibabu ya hawa watoto na kamwe haitatumika hata shilingi kwa ajili ya matumizi mengine ambayo sio lengo la fedha hizi.

Inshaallah kama nilivyolibeba hili jukumu naamini nitaendelea nalo kwa salama hadi mwisho na bila ya shaka ujira wa haya yote upo kwake mwenyewe Subhanna sisi ni watumwa tu.

Namalizia kwa kusema kwamba nakupongezeni sana ZACADIA kwa uzalendo wenu mliouonesha na inshallah tutuzidi kuimarisha zaidi umoja huu na mshikamano wetu kwa masuala yote ambayo yanayotokea hapa nyumbani.

Napenda niahidi tena kwenu kwamba hii kazi ni kwa ajili ya jamii yetu lakini tunamuweka mbele Mwenyeenzi Mungu awe ndio mlinzi wa haya yote tunayoyafanya na kwa maana hiyo tuzidi kumuomba ili atunusuru katika fitna yoyote inayotokana na fedha hizi kwani tunafahamu fedha ni miongoni mwa fitna kubwa hapa ulimwenguni.



Shukran sana

Salma Said

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.