Na Salum Vuai, Maelezo
WAKATI mabingwa wa soka wa Tanzania Bara Simba wako Zanzibar kujifua kwa mechi dhidi ya watani wao Yanga, wapinzani wao hao wamejichimbia Bagamoyo dhamira kama hiyo.
Mahasimu hao wanatarajiwa kutiana mikononi Oktoba 3, mwaka huu katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, ikiwa miongoni mwa mechi za ligi kuu inayodhaminiwa na kampuni ya simu Vodacom.
Mmoja miongoni mwa waratibu wa ziara hiyo Abdul Mshangama, aliliambia gazeti hili kuwa, leo asubuhi, wekundu hao watafanya mazoezi katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Elimu, Chukwani, huku ikinuia kuomba kufanya mazoezi wakati wa usiku kwenye uwanaj wa Amaan.
Aidha, amesema, kunaangaliwa uwezekano wa kuitafutia timu hiyo mechi mbili za kujipima nguvu.
Siku ya Jumamosi. Simba itarejea mara moja Dar es Salaam kucheza na Prisons na baada ya hapo, watapanda boti kurudi tena hapa Zanzibar kuendelea na maandalizi yao.
Nayo Yanga, ilitarajiwa kuingia kambini wilayani Bagamoyo mkoani Pwani jana, kujiandaa na mchezo huo wa Oktoba 3, dhidi ya Simba.
Imeelezwa kuwa, timu hiyo itaingia uwanja wa Taifa kwa mchezo wa kesho dhidi ya African Lyon, ikitokea Bagamoyo na baada ya mechi itarejea huko kuendelea kujiandaa na pambano la watani.
Tangu wakati wa kampeni, miongoni mwa mambo ambayo wana Yanga wamekuwa wakiomba kutoka kwa Manji ni kulipiwa kisasi cha 5-0, ingawa kwa hali ya sasa ya timu hizo, ubora wao haupishani sana, hakuna hakika kama hilo litawezekana.
No comments:
Post a Comment