HOTUBA YA MAKAMU WA KWANZA WA RAIS WA ZANZIBAR, MHE. MAALIM SEIF SHARIF HAMAD
KATIKA MAADHIMISHO YA KUMI YA SIKU YA TIBA ASILI - AFRIKA, HUKO BUSTANI YA VICTORIA MJINI ZANZIBAR TAREHE 31 AGOSTI, 2012
Mheshimiwa Naibu Waziri wa Afya,
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi,
Waheshimiwa, wawakilishi wa mabalozi wadogo wa Jamhuri ya watu wa China na India.
Katibu Mkuu Wizara Afya,
Waheshimiwa Waganga wa Tiba Asili,
Waalikwa nyote, mabibi na mabwana
Asalaam Alaykum.
Kwanza kabisa sinabudi kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutujaalia uhai na uzima na kutuwezesha kukusanyika hapa kwa pamoja katika hafla ya kuadhimisha siku ya Tiba Asili Barani Afrika.
Vile vile, shukurani zangu za dhati kabisa nazielekeza kwenu waandaaji wa shughuli hii muhimu kwa ustawi na maendeleo ya afya za watu wetu, hao siwengine bali ni Wizara ya Afya Zanzibar pamoja na wadau mbali mbali wa Tiba Asilia, kwa maandalizi yenu mazuri.
Na zaidi kwa uamuzi wenu wa kunialika mimi kuja hapa kujumuika nanyi katika hafla hii. Nasema ahsanteni sana.
Waheshimiwa viongozi, wataalamu na waalikwa wenzangu
Siku ya leo tupo hapa kwa lengo maalum ambalo ni kusherehekea siku ya Tiba Asili – Barani mwetu Afrika, katika sherehe ambazo mwaka huu zimepewa kauli mbiu iliyo katika mfumo wa swali linalouliza “SHEREHE ZA KUADHIMISHA MIAKA KUMI YA TIBA ASILI BARANI AFRIKA, TUNAJIFUNZA NINI?
Lakini kabla ya kuanza kuitafakari kauli mbiu hiyo, nahisi si vibaya kwanza tukakumbushana kuwa Tiba Asilia ni fani kongwe kabisa ambayo imekuwa ikitumiwa na binaadamu wa mataifa mbali mbali katika kutibu na kupata unafuu wa maradhi na matatizo tafauti yanayowakabili katika maisha yao ya kila siku.
Taaluma hii kongwe inazidi kukuwa na hivi sasa inapata umaarufu mkubwa. Shirika la Afya Duniani (WHO) tayari limeanzisha Idara Maalum ya Tiba Asili, bila shaka hatua hiyo ni kwa sababu ya kutambua umuhimu wake mkubwa katika kuleta unafuu wa kiafya na kusaidia kuondoa matatizo na shida za kijamii.
Katika kuthibitisha hilo, shirika hilo la WHO linasema Barani Afrika kiasi cha asilimia 80 ya wakaazi wake wanatumia Tiba Asili, katika mahitaji yao ya kujitibu na maradhi tafauti.
Nayo Kamati ya WHO Barani Afrika katika azimio lake la mwaka 1984 limeyataka mataifa kuandaa taratibu na sheria muafaka za uendeshaji na utoaji wa Tiba Asili kwa wananchi na kuleta ufanisi uliokusudiwa.
Hapa nchini mwetu Zanzibar, sote tunaelewa mchango na nafasi ya Tiba hii, kwa miaka nenda miaka rudi. Wananchi wetu, pamoja na kuthamini sana na kutumia kikamilifu tiba za kisasa katika hospitali na vituo vyetu vya afya, mara kadhaa huhitaji kutibiwa na kupata ushauri kutoka kwa Waganga wanaojishughulisha na Tiba Asili.
Idadi ya watu wanaohitaji tiba hizi inaendelea kuongezeka siku kwa siku. Halikadhalika waganga wa tiba hizi nao wanaongezeka sana. Kwa mfano zamani hapa kwetu shughuli hizi zilionekana kufanywa zaidi na watu wazima, yaani watu wa umri mkubwa , hasa wazee.
Lakini leo mambo yamebadilika. Inaonekana fani hii sasa ni sehemu muhimu ya ajira. Kwa hivyo vijana wengi nao wanajishughulisha na tiba asili.
Hapa nakuombeni tukumbuke ule usemi kwamba, “Unapofungua milango wataingia wanaohitajika na wasiohitajika. Katika muktadha huu wasiohitajika ni wale ambao hawana taaluma yoyote juu ya mambo haya, lakini nao wameamua kuingia katika mkumbo wa kutibu.
Tumekuwa tukisikia baadhi ya Waganga wa Tiba hizi wakijitangaza kutibu maradhi makubwa, hata yale ambayo kwa kawaida yanahitaji vifaa na utaalamu mkubwa, ambao hawanao.
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inatoa umuhimu wa kipekee kwa Tiba Asili, pamoja na kuandaa mazingira ambayo yatawezesha shughuli za utibabu huu ziende vizuri na ziwanufaishe wanaozihitaji, bila ya kuathiri wananchi wetu.
Ndio maana Serikali imeanzisha sera ya Tiba Asili na Tiba Mbadala ya mwaka 2008 kwa madhumuni hayo makuu.
Baadhi ya maeneo yaliyozingatia katika sera hiyo ni;
Kuweka sheria na utaratibu wa kuendesha Taiba Asili.
Kusaidia utoaji na upatikanaji wa Tiba Asili kitaalamu zaidi kwa kutoa umuhimu wa kipekee katika Utafiti pamoja na Kuweka utaratibu unaozingatia mazingira mazuri ya utoaji wa huduma na kujali usalama kwa watumiaji wa Tiba hizi.
Sasa tukirudi kwenye ile kauli mbiu yetu. Kati ya mambo ambayo mimi binafsi naamini sote tunajifunza na yanahitaji kufanyiwa kazi ni kuwepo ushirikiano wa kutosha kati ya Waganga wa Tiba Asili na wale wa Matabibu wa kisasa (Modern Doctors).
Tunachoweza kujifunza hapa ni kuwa iwapo wataalamu wa pande mbili hizi watakapokuwa na ushirikiano, basi kazi zao zitakuwa nzuri na zenye viwango vya hali ya juu zaidi katika kuponya matatizo ya watu wetu.
Lazima tukiri kwamba hadi sasa tuna tatizo kubwa katika suala zima la Utafiti katika fani hii ya Tiba Asili, hali inayosababisha waibuke watu kufanya shughuli hizi bila ya kuwa na taaluma yoyote inayohusiana na shughuli hizi ambazo zinazogusa usalama na uhai wa watu.
Vile vile bado tuna tatizo jengine, wapo waganga wa tiba asili ambao wana taaluma ya kutosha, lakini wanaficha taaluma zao na kuendelea kuwa ni siri mpaka wanakufa, na linalobaki ni jina tu la Mganga lakini taaluma anaondoka nayo.
Lakini pia wapo watafiti wa kisayansi (Research Scientists) ambao hawana taaluma ya tiba asili na miti shamba kwa jumla, lakini wanafanya utafiti bila ya kuwashirikisha wenye taaluma hiyo.
Aidha, tunao waganga wa tiba asili wenye taaluma ya kutosha ya miti shamba, lakini hawana mafunzo ya kisayansi ya kufanya utafiti (Scientific methodology).
Nahisi pande hizi mutakapoamua kushirikiana na kuunganisha nguvu zenu kufanya kazi kwa pamoja mtaweza kuleta mapinduzi makubwa katika Nyanja ya Utibabu sio tu kwa Zanzibar, lakini Barani Afrika na Duniani kote.
Waheshimiwa Viongozi, wataalamu na waalikwa wenzangu
Nimefurahishwa sana kuona ya kuwa kuna mashirikiano makubwa miongoni mwa Waganga wa tiba asili Afrika Mashariki. Sote tumejionea jinsi gani waganga hawa wa nchi za Kenya, Uganda, Tanzania Bara na Zanzibar walivyoweza kufanya maonyesho yao mazuri na ya kuvutia.
Naamini kwamba wamefanya maonesho yale kwa moyo (spirit) ule ule wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Hali hii ni ishara kuwa umoja wenu huu utawawezesha kufanya mambo makubwa sana hasa katika suala zima la utafiti wa dawa zetu za tiba asili.
Ni wazi kuwa kazi ya kutibu ni ya wito na mkiwa kama Waganga, mnahitaji ushirikiano pamoja na mshikamano katika kutoa matibabu. Na katika hilo nakusihini zile itikadi za zamani ya kuwa mimi ndiye mganga mzuri na wengine hawajui zimepitwa na wakati na si maadili ya Mtibabu. Awe wa Tiba ya kisasa au Tiba Asili nyote mnalengo moja ambalo ni kuhudumia wananchi.
Ni vyema Waganga wote kuungana kwa lengo la kutoa huduma zilizo bora kwa wananchi wetu, na kuachana na ubinafsi ambao kwa sasa hauna nafasi.
Pia nimesikia kuwa kuna misuguano isiyokwisha baina ya Waganga wetu hasa wa Tiba Asili, ikiwemo kupitia vyama vyao vilivyosajiliwa. Nakuombeni sana muache tabia hiyo na muwe wamoja. Pia natowa wito kwa Waganga wote kuhakikisha wanasajiliwa na Baraza la Tiba Asili.
Pia ni wajibu wenu kukitumia chombo hichi ambacho kipo kwa mujibu wa sheria katika kuiendeleza fani hii ya utibabu.
Na mwisho kabisa, niwakumbushe kuwa, Ukimwi bado upo na ni tatizo kubwa linaloleta athari kwa mtu mmoja mmoja na kwa taifa kwa jumla. Ukimwi unapunguza nguvu kazi, kuongeza mayatima, ni wajibu wetu sote kuelimishana juu ya athari za maradhi haya, na nyinyi kama waganga, mko karibu sana na watu walio wengi na sauti zenu zinasikika.
Hivyo nyinyi kwa ushirikiano na Madaktari wa kisasa munawajibu wa kutoa elimu ya kujikinga na maradhi ya ukimwi.
Baada ya kusema hayo machache, naomba niwashukuru tena kwa kunipa nafasi hii, na kuweza kunisikiliza kwa makini wakati nilipokuwa nikizungumza.
Ahsanteni.
No comments:
Post a Comment