Habari za Punde

Viongozi Zanzibar acheni kudanganya watu

Salim Said Salim
 
NINAPOPITIA kauli mbalimbali za viongozi waliopita na wa hivi sasa wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar hucheka kwa vile hugundua walichosema ni propaganda za kisiasa au kauli zile zilitolewa kufurahisha umma.
 
Kama nusu ya kauli na ahadi zilizotolewa za miradi iliyosemekana kuwepo zilitekelezwa, Zanzibar ingekuwa imepiga hatua kubwa ya maendeleo.
 
Sasa tunaambiwa patakuwepo na likizo ya uzazi ua siku tano za kazi kwa wafanyakazi wa Serikali ya Zanzibar ili kuwasaidia wake zao baada ya kujifungua.
 
Hili nalo ninaamini litamalizika hewani na hakuna litalofanyika na wahusika wakiulizwa watasema wapo mbioni au bado wanajipanga vema. Ni kudanganyana tu na hakuna ukweli wowote ule.
 
Nasema hivi kwa sababu kama yatafanyika mashindano ya kutoa kauli na ahadi ambazo hazitekelezwi basi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa hali yoyote ile haitakosa medali ya shaba.
 
Hapa naorodhesha baadhi ya kauli ambazo zimemalizikia hewani zilizotolewa katika miaka ya nyuma na karibuni na viongozi wa serikali na kuwaachia wasomaji kuamua:

Rais mstaafu wa Tanzania, Sheikh Ali Hassan Mwinyi alipozuru Pemba mwaka 1993 alisema; “tutaleta wataalamu wa kilimo cha pamba kuangalia uwezekano wa zao hilo kulimwa Micheweni na kuwapunguzia watu umaskini.” Hakuna mtaalamu wa kilimo hicho aliyepelekwa Micheweni hadi leo na haukufanyika utafiti wa uwezekano wa kulima pamba sehemu hio.
 
Rais mstaafu, Dk. Salmin Amour katika mwaka 1993 alisema: “Tutajenga Fumba mji wa kisasa wa biashara utaoitwa Star City na kuwa kituo maarufu cha biashara.” Kilichofanyika ni kutumia mabilioni ya shilingi na mashamba ya watu kuharibiwa. Kampuni iliyopewa mradi huo imetoweka na wahusika hawajulikani walipo.
 
Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, katika mwaka 2003 alisema: “Serikali italifanya soko la karafuu kuwa huru na watu binafsi kuweza kununua karafuu.” Kauli hiyo aliirudia mara kwa mara mpaka alipoondoka madarakani miaka miwili iliyopita na hakuna dalili za serikali kuitekeleza. Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais wa Zanzibar, Mwinyihaji Makame, akiwa katika Baraza la
 
Wawakilishi mwaka 2007 alisema; “Serikali imeanzisha utaratibu kwa watumishi wake kufanya mitihani ya Kiswahili kigumu na chepesi na watakaofaulu watafikiriwa kwanza kupandishwa vyeo.” Hakuna kilichofanyika hadi leo na hakijulikani kinachoendelea.
 
Aliyekuwa Waziri wa Italii na Uwekezaji Zanzibar, Samia Suluhu Hassan katika mwaka 2006 alisema; “Hoteli za kifahari za nyota tano zitajengwa Zanzibar na wawekezaji wakubwa wa utalii duniani. Miongoni mwa makampuni yatakayowekeza ni Ifa Hotel and Resorts, Moving Pick na Nakheel.” Mpaka sasa hakuna mwekezaji mmoja kati ya hawa aliyeonekana Zanzibar na hapajaelezwa kinachoendelea.
 
Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein alipohutubia waandishi wa habari mwaka 2011 alisema; “Nitafuatilia habari za maelfu ya watu kunyimwa vitambulisho vya Mzanzibari na kuhakikisha kila anayestahili kuwa nacho anapatiwa.” Sasa ni zaidi ya mwaka mmoja na maelfu ya watu wanahangaika na kukosa haki yao hii ya kiraia. Hapajatolewa maelezo na Ikulu juu ya suala hili.
 
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad mwaka jana alisema; “Serikali inafanya mpango kwa wazee, wanafunzi na watu wenye ulemavu kusafiri visiwani kwa kulipa nusu nukuu ili kuwapunguzia ugumu wa maisha.” Hakuna habari zozote juu ya utekelezaji wa mpango huu kama vile ilikusudiwa kuudanganya umma.
 
Ukiziangalia kauli nyingi za viongozi utaona zinatoa mwanga wa matumaini ya maisha bora, lakini hakuna linalofanyika.
 
Kauli za viongozi za kuwapa wananchi matumaini hewa ni nyingi. Miongoni mwao ni ujenzi wa hoteli ya Magic Island Hotel (dola 7,989,000), Romantic Beach Hotel (dola 672,00), Meridean na Shining Star.
 
 Vile vile palielezewa kuwepo miradi ya Mfuko wa Lebanon, lakini hakuna linaloendelea. Tunaambiwa mstahamilivu hula mbivu, lakini anayestahamili sana kungojea embe iive hula iliyooza.
 
Sina hakika kama Wazanzibari watakula mbivu au iliyooza! Ni vizuri kwa viongozi panapotokea kutowezekana kwa miradi kutekelezwa kutoa maelezo kwani ukimya unajenga dhana kuwa labda baadhi ya wakubwa walitaka ubia au “kitu kidogo” kutoka kwa wawekezaji.
 
Hizi ni zama za ukweli na uwazi na watu hawapendi kupewa ahadi zisizokuwa za kweli. Si vizuri kuwapa wananchi tamaa na baadaye wakahisi wanadanganywa.
 
Pia upo uwezekano wa baadhi ya wanaopewa mamlaka serikalini wakawa kikwazo cha miradi kutekelezwa kutokana na ubinafsi na ufisadi.
 
Vile vile tusishau baadhi ya wawekezaji, kama wa Hoteli ya Nungwi ambayo ingeligharimu dola bilioni moja ni matapeli. Toka mwanzo walionyesha ishara ya kuwa waongo kwa vile walifikia nyumba za kawaida za kulala wageni na kupatana nauli na madereva wa teksi.
 
Wawekezaji wa kweli hawakai katika nyumba za wageni za malipo ya shilingi 30,000 kwa siku na kupatana malipo ya teksi. Baadhi ya matapeli ambao hata anwani walizotoa hazipo inasemekana wametutapeli na kutuzidishia umaskini.
 
Ni vema kwa serikali kufanya uchunguzi wa kitaalamu kujua ni nani hasa mwekezaji wa kweli na nani tapeli.
 
Tutumie ofisi zetu za mabalozi na taasisi za kimataifa kuutafuta ukweli juu ya wanaotaka kuwekeza kwetu.
 
Tuache kutoa ahadi hewa kwani mwisho wake si mzuri na tujifunze kutokana na makosa tuliyoyafanya siku za nyuma.
 
Chanzo: Tanzania Daima

4 comments:

  1. Hahhhahaha, Ndungu Muandishi, Umesahau ahadi ya bandari kuu ambayo utakuwa badanri kubwa katika ukanda wa Afrika mashariki itajegwa Zanzibar.

    ReplyDelete
  2. Pia Da Salma umesahau Mh. Ali Mohammed Shein wakati wa kampeni kupitia msemaji wake aliahidi kuifanya Zanzibar kama Singapore lakini hadi leo hakuna ila umasikini unaozidi siku hadi siku. Mtoto Nairat anahitaji matibabu hadi achangiwe na wananchi serikali haina uwezo wa kumtibu.Ahadi ahadi ahadi za uongo hadi lini? tumechoka

    ReplyDelete
  3. Huyo si Da Salma ila ni mwandishi mkongwe Salim Said Salim ambaye huwa hammumunyi maneno anapoandika.

    ReplyDelete
  4. Naomba radhi kwa kukosea hii ni kutokana na kutosoma vizuri jina la mwandishi badaala ya Salim Said nilisoma Salma said. naomba radhi kwa hili.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.