Na Rose Chapewa,
Morogoro
WATU 657
wamegundulika kuwa na unene uliokithiri, wakati 14 wakiwa na dalili za saratani
ya matiti mkoani Morogoro,wakati wa zoezi la upimaji afya lililofanywa na Mfuko
wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kwenye uwanja wa Jamhuri Mkoani hapa.
Akizungumza na
gazeti hili, ofisa Mawasiliano Mwandamizi wa (NHIF) Luhende Singu alisema katika zoezi hilo watu 765 walipimwa hali
lishe, ambapo kati ya hao 6 walikuwa na hali duni ya lishe, huku 102 wakiwa na
hali nzuri.
Ofisa Mawasiliano
huyo alisema, watu 78 waligundulika kuwa na shinikizo la juu la damu, na kwamba
watu 251 waliojitokeza kupima saratani ya matiti 14 waligundulika kuwa na dalili za ugonjwa
huo.
Singu alisema,
waliobainika kuwa na dalili za Saratani walipewa rufaa kwenda hospitali ya Mkoa
wa Morogoro kwaajili ya kufanyiwa uchunguzi zaidi, ambapo watakaobainika
kuwanayo wataandikiwa kwenda kupata matibabua katika Hospitali ya Ocean Road
Jijini Dar es salaam.
Kwa Upande wake
Dk. Adolph Kahamba kutoka mfuko wa Bima
ya Afya (NHIF) amewataka wananchi kuzingatia lishe bora, ili kuepuka magonjwa yasiyo ya kuambukizwa, yatokanayo na
ulaji wa vyakula visivyozingatia lishe
ikiwemo kansa, kisukari, shinikizo
la damu na figo.
Alisema ikiwa
wananchi watazingatia matumizi bora ya vyakula, watakuwa na hali lishe nzuri,
pamoja na kuepuka kupatwa na magonjwa yatokanayo na ulaji wa vyakula visivyozingatia lishe.
Aidha alisema, upo umuhimu wa kutoa elimu ya afya kwa jamii nzima ya
Tanzania, kwa kuwa imegundulika
kuwa watu wengi hawana tabia ya kupima afya zao mara kwa
mara, na hivyo kusababisha magonjwa kuwa sugu katika miili yao.
Hata hivyo aliwapongeza wakazi wa mkoa wa Morogoro kwa mwitikio
waliouonesha, na kwamba ni mfano wa kuigwa na mikoa mingine mara zoezi hilo litakapofanyika katika maeneo
yao.
No comments:
Post a Comment