Na Masanja
Mabula, Pemba
WAPAMBE wa wagombea
wa nafasi ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vija ya CCM (UVCCM) mkoa wa kaskazini
Pemba nusura wazichape hadharani baada ya taarifa za matokeo ya uchaguzi kuvuja
kuwa wagombea wao wamepitana kwa kura tatu, huku pia kukiwa na taarifa ya
kuwepo ongezeko la kura tatu zaidi ya mahudhurio ya wajumbe.
Kuvuja kwa
matokeo hayo kulisababisha hali ya sintofahamu kwa wagombea na wapambe wao nje
ya ukumbi wa Jamhuri hall ambapo wapambe wa mmoja wa mgombea walionekana
kutokubaliana na matokeo hayo wakidai kura zimechakachuliwa.
Baadhi ya wapambe
hao pamoja na wajumbe waliokuwa wakimuunga mkono mgombea wao walipanda jazba na
kutaka kumtembezea kipigo kijana mmoja anayedaiwa kupiga kura licha ya kutokuwa
mjumbe halali wa jumuiya hiyo.
Fujo hizo
zilimlazimisha Katibu wa UVCCM mkoa huo, Mussa Said Kisinja kuingilia kati na
kumnusuru kijana huyo ambaye alikuwa amezongwa na wapambe wa mmoja wa mgombea,
ambapo Katibu huyo alitumia hekima na busara na
hivyo kufanikiwa kuwatuliza wapambe
na mgombea wao.
"Kama kuna
udanganyifu umefanyika, basi tumieni utaratibu kikatiba ya nini kufanya fujo,
kanuni zipo na sheria zipo, kuweni na moyo wa kustahamili ikiwa kuna
uchakachuaji lazima sheria za uchaguzi zifuatwe," Kisinja alisema.
Hata hivyo, hali
ilibadilika mara ya baada ya matokeo kutangazwa kwani wagombea hao walikuwa
wamepitana kwa zaidi ya kura 30 jambo ambalo hata mgombea na wapambe waliokuwa
na jazba walitulia na kukubali matokeo.
Msimamizi wa
uchaguzi huo Katibu wa CCM mkoa wa
kaskazini Pemba, Hassan Ali Shaali ndiye alizima hali hiyo ya sintofahamu baada
ya kumtangaza Fadhila Nassor Abdi kuwa mshindi baada ya kupata kura 86 huku
Yahya Khamis Ali akipata kura 33 na Khamis Hamad alipata kura 16.
Nafsi ya ujumbe
wa mkutano mkuu wa vijana taifa waliochaguliwa ni Omar Juma 69, Asila Ali Salim
68, Time Bakar 62 na Viwe Khamis ambaye pia ni mjumbe wa baraza la wawakilishi
kupitia vijana mkoa huo aliyepata kura 53.
Aidha msimamizi
huyo wa uchaguzi alikiri kuwepo na ongezeko la kura za ziada 3 na kuwaomba wagombea kuridhika na matokeo
yaliyotangazwa kwa kuwa aliyepata na aliyekosa wote wana lengo moja na kuijenga
jumuiya hiyo na CCM kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment