Na Masanja Mabula, Pemba
MAKAMU Mwenyekiti
wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake (UWT), Asha Bakar Makame amewataka wananchi
katika mkoa wa kaskazini Pemba kuacha ushawishi wakati wa kutoa maoni ya katiba
ya Jamhuri ya Muungano bali kila mmoja atoe maoni kwa mujibu anavyoona inafaa.
Akizungumza na
mwandishi wa habari hizi Wete, alisema pamoja na kuwepo na baadhi ya watu
wanopita mitaani kuwashawishi wananchi na kuwafundisha jinsi ya kuzungumza mbele ya tume, lakini wanapaswa kuwapuuza na
kufikiria ni kasoro zipi za muungano zinahitaji marekebisho.
Alisema katiba
itakayopatikana itakuwa na maslahi kwa wananchi wote , hivyo kuchangiwa mawazo
na baadhi ya watu si jambo la busara kwa
vile mawazo yao hayatapata fursa ya
kusikilizwa na wajumbe wa kuratibu maoni ya katiba.
"Wananchi
acheni jazba, na waepukeni wanaowashawishi na kuwafundisha jinsi ya kwenda
kuzungumza mbele ya tume, kwani mtakuwa mmepoteza haki yenu kikatiba na mawazo
mtakayotoa yatakuwa ni faida ya waliowafundisha na sio kwa ajili ya umma,"
alisema.
Aidha Makamu
Mwenyekiti huyo aliwataka wanawake kuwa msitari wa mbele kwenda kutoa maoni yao
na kuwashauri wafike mapema mbele ya tume ya kuratibu maoni ambayo inatarajiwa
kuwasili mkoa wa kaskazini Pemba Jumapili kuendelea na mchakato wa ukusanyaji
wa maoni.
Alifahamisha kuwa
pamoja na katiba ya sasa kuwa na changamoto kadhaa, huu ni wakati wa kuziondoa
changamoto hizo kupitia maoni na si vyenginevyo.
"Zipo
changamoto nyingi ndani ya Muungano ambazo zinahitaji kufanyiwa marekebisho,
hii ni fursa pekee kwa wananchi wa mkoa wa kaskazini Pemba kuitumia na wasiwe
na woga kwani tume imeundwa kisheria na itaheshimu maoni ya kila mmoja,"
alieleza.
Mweyekiti huyo
pia amekanusha taarifa za kwamba yeye ni miongoni wa wanachama wa CCM
wanaopinga Muungano na kusema kuwa hizo ni propanga za kumchafua kisiasa kwani
yeye ni miongoni mwa viongozi walio
katika mstari kuutetea muungano.
"Najua faida
za muungano, unaposema kuwa mimi siutaki nitashindwa kukuelewa, hizo ni njama
za baadhi ya wanachama wa UWT wanaotaka kujipatia umaarufu kisiasa, natambua
kuwepo na ndugu zetu Tanzania Bara, leo iweje niukatae Muungano?" alihoji.
Hata hivyo
alisema bado yeye ana mapenzi makubwa na
CCM na ataendelea na msimamo wa
kukitetea,kukilinda na kuzisimamia sera zake ili ziendelee kuwanufaisha
wanachama na Watanzania kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment