Habari za Punde

Maalim Seif: GNU imepata mafanikio. Imewakomboa wengi na umasikini. Ahimiza uhuru, uwazi kuchangia katiba. Akemea rushwa, kufuja mali za umma


Na Juma Khamis
 
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kutoa maoni yao katika mchakato wa katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Maalim Seif aliyasema hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika hoteli ya Grand Palace mjini Zanzibar.

Maalim Seif amesema suala la maoni ya katiba mpya aliwataka wananchi kushiriki kutoa maoni kwa uhuru, uwazi na kuzingatia uvumilivu.

“Hata kama mtu hakubaliani na maoni au hoja zinazotolewa na mwengine, inabidi asikilize kwa uvumilivu. Naye akipata fursa aseme yake kwa uwazi pia,” alifafanua.

Alisema maoni ya wengi ndio yatakayoheshimiwa baada ya wale wachache kupewa haki yao ya kusikilizwa kikamilifu.

Katika hilo Maalim Seif alisema kila kiongozi  wa kisiasa ana haki ya kuwaelimisha  wafuasi wake kwa kuzingatia misingi na sera ya chama chake
, muhimu tu yatumiwe majukwaa ya kisiasa.

Aidha Maalim Seif amewataka watendaji serikalini kuacha tabia ya udokozi wa fedha za wananchi kwa lengo la kujinufaisha wao binafsi, huku akisisitiza kuwa serikali haitavumilia tena.

Alisema kumekuwa na matumizi holela ya fedha za wananchi kunakofanywa na watendaji hao, licha ya juhudi zinazochukuliwa na serikali  kuwakataza na kuwahimiza kujali misingi ya utawala bora.

Alisema pamoja na marekebisho katika baadhi ya maeneo lakini bado kila zinapotoka ripoti za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu, kunaonekana matumizi ya fedha za umma yasiyofuata taratibu.

Alisema katika baadhi ya miradi, fedha zilizolipwa ni nyingi ikilinganishwa na kazi iliyofanyika pamoja na ubora wa kazi yenyewe.

Maalim Seif alisema tayari serikali imeshawasimamisha kazi baadhi ya watendaji ambao wamebainika kuhusika na ubadhirifu wa fedha za umma na wanaendelea kuchunguzwa.

“Iwapo watabainika kuhusika, watachukuliwa hatua nyengine za kisheria,” alisema Maalim Seif.

Akizungumzia suala la watendaji kulalamikiwa  kuviza haki za wananchi, Maalim Seif alisema suala hilo limejitokeza zaidi katika utoaji wa vitambulisho vya Mzanzibari Mkazi.

Alisema pamoja na ahadi na kauli zinazotolewa na watendaji na viongozi kuwa kila mwananchi mwenye sifa apatiwe kitambulisho hicho, bado malalamiko ni mengi kuwa kuna watu wananyimwa haki hiyo kwa makusudi.

Hata hivyo, alisema serikali inajitahidi kutafuta ufumbuzi wa haraka wa changamoto hiyo kwa kutambua kuwa vitambulisho ndio utambuzi wa Wazanzibari wakaazi na vinahusika moja kwa moja katika upatikanaji wa huduma na haki za msingi.

Alisema kuwa na kitambulisho ni jambo la lazima na kwamba kumkosesha mtu au mtu kushindwa kuwa nacho ni kosa ambalo muhusika anaweza kuhukumiwa kifungo jela.

Aliwanasihi wananchi ambao vitambulisho vyao viko tayari, lakini bado wamekuwa na ajizi kwenda kuvichukua, wakavichuke haraka.

Akizungumzia serikali ya umoja wa kitaifa, maalim Seif alisema imepata mafanikio makubwa kutokana na juhudi za kuleta mabadiliko na maendeleo kwa wananchi wa Zanzibar.

Alitaja baadhi ya mafanikio hayo kuwa ni kuimarika kwa huduma za afya, elimu, pamoja na wananchi wengi zaidi kunufaika na utalii.

Aidha alilitaja suala la miundombinu kuwa nalo limepiga hatua kwa kiasi kikubwa, pamoja na kuinua maisha ya wakulima wa karafuu kwa kuongeza bei na kusukuma hatua za maendeleo ya kilimo kwa kutoa pembejeo kwa bei rahisi ikiwemo mbolea na trekta, ambapo mzigo mkubwa unabebwa na Serikali.

Kuhusu maridhiano, alisema wako baadhi ya wananchi ama hawajaelewa, au wameamua kukataa maridhiano na maelewano miongoni mwa Wazanzibari.

Alisema watu hao miongoni mwao wakiwemo watendaji serikalini wamekuwa na mwenendo ambao  matokeo yake yanaweza kuleta mgawanyiko na kuvuruga hali ya amani na mshikamano uliopo.

Hata hivyo, alisema serikali haitachoka kuchukua juhudi ya kuwaelimisha juu ya umuhimu wa maridhiano na kwamba wananchi hawako tayari kurudi nyuma walikotoka katika hali ya mifarakano na chuki.

Aliwahimiza wananchi kuendelea kulinda amani na utulivu uliopo, kwani amani ikivunjika hakuna mtu atakaenusurika.

Alisema bado serikali ya awamu ya saba ni vumilivu na sikivu na haijataka kuchukua hatua za mabavu dhidi ya watu wanaovuruga amani, lakini akawanasihi wananchi watumie vizuri uhuru waliopewa  na wasipindukie mipaka.

Maalim Seif aliwakumbusha wananchi kujikinga na ugonjwa wa Ukimwi na kuacha tabia ya kuwanyanyapaa wale walioambukizwa ugonjwa huo.

Alisema hali ya ukimwi Unguja na Pemba ni mbaya zaidi kwa watu wa makundi maalum, ambayo inakadiriwa kupita kiwango kilichopo katika jamii cha asilimia 0.6.

Kwa upande wa watu wenye ulemavu, Makamu wa Kwanza wa Rais, aliwahimiza wananchi kuendelea kuwasaidia watu wenye ulemavu na kuisihi jamii kutowaficha watoto wenye matatizo hayo akisisitiza kuwa walemavu wana haki sawa na wengine.

Kuhusu dawa za kulevya, Maalim Seif alikiri kwamba bado ni changamoto kubwa inayoikabili Zanzibar na kusema athari za dawa hizo zipo wazi miongoni mwa vijana.

Kuhusu kujiuzulu kwa Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Ismail Jussa Ladhu, alisema chama kimemkosa mtu muhimu, mchapakazi, lakini akasema ameonesha mfano mzuri.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.