Habari za Punde

Askofu Mokiwa alitaka kanisa kukataa fedha chafu




Joseph Ngilisho,Arusha
 
ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Anglikana nchini,Dk.  Valentino  Mokiwa amelitaka kanisa hilo kukataa fedha chafu zinazotolewa kama sadaka na mafisadi wanaotumia mgongo wa makanisa kujisafisha.

Askofu Mokiwa aliyasema hayo katika ibada maalumu ya shukrani iliyofanyika kanisa la Anglican dayosisi ya Mount Kilimanjaro.
Ibada hiyo imefanyika baada ya kumalizika  mgogoro wa muda mrefu uliolikumba kanisa hilo na kusababisha Askofu wa kanisa hilo mkoa wa Arusha,Stanley Hotay  kupingwa mahakamani.


Dk.Mokiwa alisema kumeibuka tabia zisizofaa kwa baadhi ya viongozi wa dini kuogopa kuwakemea mafisadi wa makanisa baada ya kukubali kupokea fedha zao huku wakijua kabisa wanakiuka sheria za kanisa.

Alisema iwapo mafisadi hao wataachwa watambe makanisani ni wazi kanisa litagawanyika kutokana na wao kutaka kuliendesha watakavyo.


Alilitaka kanisa hilo kuacha tabia ya kuwa omba omba badala yake lijijengee uwezo wa kujitegemea kwa kubuni miradi mbalimbali ikiwemo kuanzisha shule na hospitali hatua ambayo itasaidai kuondoa fedha chafu zinazopenyezwa na mafisadi kanisani.

Katika hatua nyingine askofu Mokiwa aliwataka waumini wa dini hiyo kuacha kuyashabikia baadhi ya magazeti ambayo yanaandika vibaya habari zake.

Naye askofu wa Kanisa hilo Dayosisi ya Mount Kilimanjaro,Stanley Hotay aliliomba kanisa hilo kuendelea kudumisha amani na kushirikiana kwa pamoja na kusahau yote yaliyopita.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.