Habari za Punde

Balozi Seif ataka wazazi wasimamie malezi ya watoto



Othman Khamis Ame

 MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Balozi Seif Ali Iddi amesema sifa sahihi watakayoendelea kupewa  wazazi popote walipo  itapatikana endapo jukumu la kuwalea watoto wao watalipa kipaumbele kinachostahiki.

Balozi Seif ambaye pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba mfumo wa utandawazi wa dunia  uliopo hivi sasa umechangia kuathiri malezi bora ya vijana   ndani ya jamii licha ya kwamba upande mmoja unaelimisha.

Akiufungua mkutano mkuu wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Kaskazini Unguja katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya CCM jimbo la Kitope, Balozi Seif alisema  jumuiya hiyo hivi sasa ina kazi nzito ya malezi ya vijana kutokana na mfumo  wa utandawazi.


Balozi Seif alionya kwamba baadhi ya wazazi nchini wanahusika katika janga la upotofu wa maadili kwa vijana kutokana na kuwaridhia watoto wao kupindukia na matokeo yake watoto hao kukosa heshima kwa kiwango cha kutisha.

“Utandawazi kwa kiasi kikubwa umeharibu mfumo wa malezi na kupelekea baadhi ya watoto kuwaita baba zao madingi wakati mama wakiwaita mom. Sasa  tunakwenaa wapi,?” alihoji Balozi Seif .

“U dot. com wao walioubeba vijana hivi sasa unawaharibia maadili yao. Sasa watoto wetu heshima zao zimepungua kutokana na utandawazi uliotuharibia mfumo wetu wa malezi,”alieleza.

Alisema wanajumuiya hiyo lazima wawadhihirishie wananchi, CCM na vijana wote kwamba jumuiya hiyo ina nguvu kwa vile inabeba watu wa rika zote katika jamii inayowazunguuka.

Balozi Seif aliwashauri viongozi wapya watakaochaguliwa katika mkutano huo kukubali kubeba dhamana ya kuwa waaminifu, waadilifu na upendo ili kuisaidia serikali kuu kwa wao ndio walezi katika kutoa elimu kwa watoto.

Akizungumzia suala la amani Balozi Seif aliitaka jamii kupiga vita dalili zote zinazoashiria kuvurugika kwa amani ambayo ikitoweka hakutakuwa na wakati wa kujenga uchumi wa taifa.

Aliwakumbusha viongozi wa jumuiya hiyo na wanaCCM    kuendelea kuisimamia amani iliyopo nchini kama ilani ya chama hicho ilivyoelekeza.

Aliwakumbusha wanaCCM wote kuendelea kutetea sera na ilani za chama chao bila ya kificho kwa vile wanaziamini na walishiriki katika kuzitengeneza.

Mapema  Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Kaskazini Unguja ambae pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi Tanzania upande wa Zanzibar, Mussa Ame Silima alisema jumuiya hiyo inaendelea kufanya chaguzi zake katika ngazi mbali mbali sambamba na jumuiya nyengine kutokana na mabadiliko ya ngazi za juu ya CCM.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.