Habari za Punde

Ban Ki-Moon Amepongeza hatua ya Amani Zanzibar.



Na Mwandishi wetu 
KATIBU Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Ban Ki-moon amepongeza hatua ya amani na utulivu uliofikiwa Zanzibar kufuatia maridhiano na makubaliano ya kisiasa visiwani humo.

Ki-moon alitoa pongezi hizo alipokutana na Rais Jakaya Kikwete, katika makao makuu ya UN mjini New York, Marekani.

Katibu Mkuu huyo alimwambia Rais Kikwete kuwa sasa Tanzania na eneo lote la Afrika Mashariki linanufaika na uamuzi mwingine wa busara wa kisiasa wa kutafuta na kupata maridhiano Zanzibar.


Aidha Ki-moon amesifu na kupongeza uamuzi wa Rais Kikete wa kuridhia mageuzi ya katiba ya Tanzania.

“Nakupongeza sana kwa uamuzi wako sahihi na wa busara wa kisiasa wa kuangalia upya katiba ya sasa ya nchi yako kwa nia ya kutungwa kwa katiba mpya kwa sababu hatua hiyo dhahiri itaendeleza utulivu ambao umedumu Tanzania kwa miongo mingi,” alisema Ki-moon.



Rais Kikwete ambaye yuko New York, Marekani, kwa ziara ya siku mbili amekutana na Ban Ki Moon ikiwa ni shughuli yake ya kwanza rasmi tokea alipowasili mjini humo mchana wa juzi.

Katibu Mkuu huyo wa UN amesifu jitihada zinazofanywa na viongozi wa nchi wa eneo la Maziwa Makuu katika kuleta amani Mashariki mwa Congo (DRC).

“Niliitisha mkutano wa viongozi wa eneo hilo Septemba 27, mwaka huu, walihudhuria viongozi wengi akiwamo Rais Joseph Kabila wa DRC na Rais Paul Kagame wa Rwanda, na kuwaeleza kuwa Umoja wa Mataifa unafuatilia kwa makini matukio ya eneo hilo na kuwajulisha kuwa kama wanahitaji msaada wowote basi sisi tuko tayari,” alisema Ki moon.

Katibu Mkuu huyo pia alimwomba Rais Kikwete kusaidia maendeleo ya kisiasa nchini Zimbabwe kufuatia Rais Kikwete kuchaguliwa Mwenyekiti wa chombo maalum cha Jumuia ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kuhusu siasa, ulinzi na usalama.

“Kwa nafasi yako kama Mwenyekiti wa chombo maalum cha SADC ni dhahiri kuwa unaweza kuchangia sana maendeleo ya kisiasa ya Zimbabwe,” Ki-moon alimwambia Rais Kikwete.

Rais Kikwete alimweleza Katibu Mkuu huyo kuwa uamuzi wa kuunda katiba mpya unalenga kuwa na katiba ambayo itaiongoza Tanzania kwa miaka 50 ijayo.

 “Baada ya kutumia katiba yetu nzuri kwa miaka 50 iliyopita, tukaamua kuwa pengine ni vyema kuunda katiba ambayo itatupeleka kwa miaka mingine 50 ijayo,” alisema.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.