Na Abdulla Mohammed
UHUSIANO wa kidugu na wa kihistoria kati ya China na Zanzibar umeimarika zaidi kutokana na watu na serikali za nchi hizo mbili kuwa karibu zaidi na kusaidiana katika nyanja mbali mbali za kimaendeleo.
Hayo yameelezwa na Balozi Mdogo wa China aliyepo Zanzibar, Chen Qiman, katika sherehe ya maadhimisho ya miaka 63 ya kuanzishwa Jamhuri ya Watu wa China, iliyofanyika hoteli ya Zanzibar Beach Resort juzi usiku.
Balozi Qiman alieleza kuwa yeye binafsi amevutiwa na wananchi wa Zanzibar kwa kuwa na utamaduni wa mapenzi miongoni mwao, bila kujali tafauti zao za rangi, dini au kabila, pamoja na ukarimu wao kwa wageni, jambo ambalo linapaswa kuiga na nchi nyengine duniani.
Balozi huyo alisema mbali ya misaada iliyotolewa na China kwa Zanzibar, bado kuna fursa kubwa ya Zanzibar kuweza kufaidika zaidi na misaada ya China kupitia mabilioni ya dola za Marekani zilizotengwa kwa bara la Afrika.
"Bado nina kazi kubwa ya kuhakikisha nikiwa hapa, Zanzibar inapata misaada zaidi kwani imepata kidogo hadi sasa, hivyo tushirikiane kufanikisha lengo hili" alisema Balozi Qiman.
Hata hivyo Balozi Qiman, alisema Zanzibar ikiwa sehemu ya Tanzania itafaidika na fedha zilizotengwa kwa ajili ya Tanzania.
Aliitaja miradi ambayo inaendelea Zanzibar kupitia China kuwa ni ujenzi wa taminali mpya ya uwanja wa ndege wa Zanzibar, Mradi wa e-government, ujenzi wa skuli ya Sekondari ya Mombasa, ukarabati wa kitengo cha ICU cha hospitali kuu ya Mnazimmoja na hospitali mpya kisiwani Pemba.
Aliitaja miradi mingine kuwa ni wa masafa mafupi wa ZBC Redio, taa za barabarani na mafunzo kwa watendaji wa sekta mbali mbali na viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wa kada tafauti.
Akizungumza kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, waziri wa Ardhi, Maji, Makaazi na Nishati Zanzibar, Ramadhan Abdalla Shaaban, alisema Serikali na wananchi wa Zanzibar wanatoa shukurani zao za dhati kwa wananchi wa China, pamoja na Serikali yao kwa kuisiadia Zanzibar katika nyanja mbali mbali.
No comments:
Post a Comment