HOTUBA YA MAKAMU WA
KWANZA WA RAIS WA ZANZIBAR, MHE. MAALIM SEIF SHARIF HAMAD KWA WAANDISHI WA
HABARI KATIKA UTARATIBU WA VIONGOZI KUKUTANA NA WAANDISHI KILA BAADA YA MIEZI
MITATU KUZUNGUMZIA UTENDAJI SERIKALINI HUKO HOTELI YA GRAND PALACE MALINDI
MJINI ZANZIBAR TAREHE 6 OKTOBA 2012
Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif.hamad
Waheshimiwa Waandishi
wa habari
Kwanza
kabisa sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutuweka katika hali ya
uzima hadi kukutana tena leo kuzungumzia utendaji na majukumu yetu
tuliyokabidhiwa na wananchi wa Zanzibar katika serikali yetu ya awamu ya saba
ya uongozi ambayo imetimiza takriban miaka miwili sasa.
Pili
natoa shukurani zangu za dhati kabisa kwenu nyinyi wanahabari mliotenga muda
wenu kuja kuhudhuria kwa wingi kuitikia wito wetu wa kutusikiliza, na baadaye kupata
fursa ya kuomba ufafanuzi wa masuala mbali mbali yanayohusu maendeleo ya nchi
yetu katika nyanja za kiuchumi, kijamii, kisiasa na mambo yote yanayogusa jamii
ya Wazanzibari kwa jumla.
Waheshimiwa Waandishi
wa habari
Nianze
sasa, kuzungumzia mafanikio kwa jumla tuliyoweza kuyapata na changamoto
tunazokabiliana nazo katika kipindi hichi cha mwaka wa pili wa serikali ya
awamu ya saba. Waheshimiwa katika nchi yetu tunaendelea kujivunia hali ya amani
na utulivu katika nchi yetu ya Zanzibar. Wananchi wote wanapata fursa na uhuru
wa kufanya shughuli zao za kujiletea maendeleo na kuendeleza mshikamano
miongoni mwao. Hali hii hatuna budi kudumisha kwa kuenzi misingi ya maridhiano ya
kisiasa yaliyofikiwa Novemba 5, mwaka 2009 na baadaye kuwa msingi wa kupatikana
serikali hii shirikishi yenye Muundo wa Umoja wa Kitaifa.
Kutokana
na nchi yetu kuendelea kudumu katika hali ya amani, utulivu na maelewano,
wananchi wamekuwa wakiitumia kikamilifu fursa na neema hiyo kushiriki katika
shughuli za kujieletea maendeleo, ambapo pia serikali inaendelea kusimamia
majukumu ya wananchi kikamilifu, ikiwemo kukuza uchumi wake kwa mintaarafu ya
kuwapunguzia wananchi ugumu wa maisha yao.
Katika
mwaka 2011 uchumi wetu ulikuwa kwa asilimia 6.8 huku matarajio katika mwaka huu
wa 2012/2013 yakionesha dalili njema kutokana na tulivyojipanga, ambapo uchumi huo
unatarajiwa kukuwa kwa asilimia 7.5. Vile vile pato la Mzanzibari limekuwa
kutoka T.SHS 782,000 kwa mwaka hadi kufikia TSHS 960,000 ambazo ni sawa na dola
za Marekani 615 kutoka 560 mwaka 2010.
Kwa
vyovyote vile, bila ya kuwepo hali ya amani na utulivu na maelewano miongoni
mwetu tusingeweza kujenga imani kwa wawekezaji vitegauchumi ambao hadi sasa
wanaendelea kujitokeza kwa wingi na kutuunga mkono kwa kuwekeza miradi yao. Bila
shaka hali hiyo inatokana na kuridhishwa kwao na amani na utulivu uliopo.
Hata
hivyo, lazima tukiri kuwa bado tunayo kazi nzito mbele yetu ya kuzidisha bidii kwa
kila mmoja wetu, kuiunga mkono serikali katika kuhakikisha nchi inaendelea
kubaki katika hali ya amani na utulivu na kusaidia kukuza kasi ya kuimarika
uchumi wetu.
Kwa
kufanya hivyo ndipo tutaweza kuyafikia malengo ya Milenia, ambapo nchi zote
zinatakiwa ifikapo mwaka 2015 pato la wananchi wake liwe limefikia T.SHS
884,000. Hata hivyo tunapaswa kuzidi kuwajengea matumaini wananchi wetu, ambao
wanaamini hali ya kukua kwa uchumi wa nchi, haina budi kuambatane na fedha
kuonekana mifukoni na sio kwenye makaratasi.
Sekta
za Kilimo, Biashara na Huduma zimeendelea kupewa msukumo mkubwa na kuendelea
kuchangia kwa kiasi kikubwa uchumi na mapato ya wananchi wetu. Kwa mfano katika
Huduma, utalii umeendelea kutoa mchango wa kipekee katika uchumi wa Zanzibar.
Sekta hii inachangia asilimia 80 ya fedha za kigeni na asilimia 70 ya wananchi
wetu wanafaidika katika sekta hii kwa njia moja ama nyengine.
Mwelekeo
wa Serikali yetu ni kuzidi kuiimarisha sekta hii ya Utalii, ili iendelee kutoa
mchango mkubwa zaidi kwa wananchi. Na katika kuhakikisha lengo hilo tunalifikia,
hivi sasa serikali imekuja na mkakati mpya wa “Utalii kwa Wote”. Mkakati huu tayari
umezinduliwa rasmi, na lengo la kuanzishwa kwake ni kuhakikisha kila mwananchi Mzanzibari
popote pale alipo Unguja na Pemba ananufaika na sekta hii ya utalii.
Waheshimiwa Waandishi
wa Habari
Kama
nilivyogusia hapo awali mafanikio ya mikakati na malengo yote hayo
tuliyoyaeleza yatatokana na nchi yetu kuendelea kudumu katika hali ya amani,
utulivu na maelewano miongoni mwa wananchi wake.
Katika
nchi yetu ni ukweli uliowazi kwamba wapo baadhi ya wananchi ama hawajaelewa, au
wameamua kukataa hali hii ya maridhiano na maelewano miongoni mwetu. Watu hao
wakiwemo miongoni mwa baadhi ya watendaji serikalini wamekuwa na mwenendo ambao
matokeo yake yanaweza kuleta mgawanyiko na kuvuruga hali hii ya mshikamano na
amani tunayojivunia.
Serikali
itaendelea kuchukua juhudi kubwa kuwaelimisha juu ya umuhimu wa maridhiano yetu
na kuwafahamisha kwamba wananchi walio wengi hivi sasa hawako tayari kurudi
nyuma tulikotoka kwenye hali ya mifarakano na chuki miongoni mwa jamii.
Waheshimiwa Waandishi
wa Habari
Katika
mkutano kama huu na waandishi wa habari mwaka jana, nilijikita zaidi kuzungumzia
changamoto za kiuchumi ambazo zimesababisha ugumu wa maisha kwa Wazanzibari
walio wengi, zikiwemo mfumuko mkubwa wa bei za bidhaa muhimu kama vile, mchele,
sukari, unga wa ngano na nyenginezo na kueleza mipango tuliyokuwa tumejipangia.
Leo nimepanga nizungumzie zaidi kwa kifupi changamoto za ndani zinazojitokeza
katika utendaji wa kila siku serikalini.
Waheshimiwa
Katika
utendaji wetu serikalini katika kipindi hiki cha miaka miwili, bado
tunakabiliwa na changamoto nyingi. Kati ya hizo ni kudhibiti matumizi holela ya fedha za umma miongoni mwa
watendaji wetu. Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali mwaka
2010/2011 inaonesha bado kuna watendaji ambao wamedhamiria kujinufaisha binafsi
kupitia fedha za serikali. Wanafanya hivyo, licha ya hatua na juhudi kubwa zinazochukuliwa
kuwakataza na kuhimizana kujali misingi ya Utawala Bora.
Pamoja
na marekebisho katika baadhi ya maeneo lakini bado kila zinapotoka ripoti za
Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu, zinaonesha suala la matumizi yasiyofuata taratibu
linaendelea kujitokeza.
Kuna
udhaifu mkubwa wa kukosekana baadhi ya vielelezo muhimu katika ukusanyaji na
matumizi ya mapato. Aidha, kumegundulika kujitokeza udanganyifu katika
utayarishaji wa mafao ya baadhi ya wastaafu.
Mdhibiti
na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ameanza utaratibu wa kukagua miradi
ya maendeleo na kujiridhisha kuwa kazi iliyofanyika inalingana na thamani ya
fedha zilizotumika. Imegundulika katika baadhi ya miradi, fedha zilizolipwa ni
nyingi sana ikilinganishwa na kazi iliyofanyika pamoja na ubora wa kazi wenyewe
kuwa haulingani kabisa na fedha zilizolipwa.
Napenda
kutoa wito maalum kwa watendaji serikalini kuacha tabia ya udokozi wa fedha za
wananchi, na wahakikishe wanafuata taratibu na kanuni za matumizi ya fedha za
umma. Aidha, serikali haitavumilia kuona baadhi ya watendaji wanaendelea
kukiuka sheria zilizopo na kuchukua fedha za wananchi kujinufaisha wao binafsi.
Sote
tunaelewa ni kwa kiasi gani serikali inavyojibana katika matumizi, ili
kuhakikisha mapato hayo kidogo yanayopatikana yanatumika katika shughuli za
maendeleo na za kijamii.
Hivi
sasa serikali inafanya kila linalowezekana kuhakikisha inapata usafiri wa
uhakika wa baharini, kwa azma ya kuwaondolea usumbufu wananchi na wageni
wanaohitaji kusafiri kati ya Unguja na Pemba na Tanzania Bara. Jambo hilo
linahitaji fedha nyingi katika kufanikiwa kwake; fedha ambazo zitatoka katika mfuko wa serikali. Sasa pale
wanapojitokeza watendaji wa serikali kurudisha nyuma juhudi kama hizo kwa
kufanya udanganyifu kwa kweli hilo si jambo zuri na si jambo la kuvumiliwa.
Serikali inachukua bidii kutafuta meli kubwa
ya kisasa au za kisasa kwa kuamini kwamba hatua kama hiyo ndiyo
itakayotuwezesha kuwa na usafiri wa uhakika na kuepuka maafa ya baharini, kama
yaliyotokea mwezi Julai mwaka huu kwa kuzama meli ya MV. Skagit katika eneo la
Chumbe na Septemba mwaka jana, yalipotokea maafa kama hayo ilipozama meli ya
MV. Spice Islander katika eneo la Nungwi.
Changamoto
nyengine ya muda mrefu inayotukabili ni baadhi ya watendaji wetu kulalamikiwa
kuviza kwa makusudi haki za wananchi. Hali hiyo imejitokeza zaidi katika suala
la utoaji wa Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi (ZANID).
Pamoja
na ahadi na kauli mbali mbali za watendaji na viongozi kuahidi kila mwananchi
aliyefikia umri wa miaka 18 na mwenye sifa zote za kupata kitambulisho hicho
kuwa atapatiwa, bado malakamiko ni mengi katika jamii kuwa kuna watu wananyimwa
haki hiyo kwa makusudi kabisa.
Serikali
inajitahidi kutafuta ufumbuzi wa haraka changamoto hii kwa kutambua kuwa vitambulisho
hivyo ndio utambuzi wa Wazanzibari Wakaazi na vinahusika moja kwa moja katika
upatikanaji wa huduma na haki mbali mbali za msingi.
Kuwa
na kitambulisho hicho ni jambo la lazima la kisheria na kwamba kumkosesha mtu
au mtu kushindwa kuwa nacho ni kosa ambalo mhusika anaweza kuhukumiwa kifungo
na faini. Na kwa umuhimu huo huo, napenda kuwanasihi wananchi ambao
vitambulisho vyao viko tayari, lakini bado wamekuwa na ajizi kwenda kuvichukua
wakavichukue haraka.
Kwa
upande mwengine kutokana na umuhimu wa kitambulisho hicho na kwa kuwa kimehusishwa
moja kwa moja katika upatikanaji wa huduma na haki za msingi, kumejitokeza
mahitaji makubwa ya watu kuvitafuta na hata wasiohusika, yaani baadhi ya wageni
wanavitafuta kwa udi na uvumba.
Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduizi Mhe. Dk. Ali Mohammed Shein kwa
kuendelea kuwasisitiza wahusika wanaolalamikiwa kuwanyima wananchi vitambulisho
hivyo kuacha tabia hiyo. Kwa mara ya mwisho Rais Shein alitoa wito wiki
iliyopita kule Pemba wakati wa semina maalum kwa watendaji wa Serikali za
mitaa. Ni imani yangu kwamba watendaji na viongozi wa serikali za Mitaa, Wilaya
na Afisi ya Msajili wa Vitambulisho, watatii agizo hilo la Rais.
Waheshimiwa Waandishi
wa Habari
Nimelazimika
kulizungumza kwa kirefu kidogo suala hili la vitambulisho vya Ukaazi kutokana
na umuhimu wake kwa wananchi. Lakini pia tumeona namna baadhi ya watu na
vikundi wanavyoweza kutumia udhaifu wa utoaji vitambulisho hivyo kuuhusisha na
masuala mengine muhimu ya Kitaifa.
Tumeona
wakati wa zoezi la Sensa ya Kuhesabu watu na Makaazi hivi karibuni, baadhi ya
watu walivyo tumia udhaifu wa utoaji vitambulisho hivyo kukaidi amri ya
kuhesabiwa. Wamefanya hivyo, licha ya kuwa jambo la kuhesabiwa lina umuhimu wa
kipekee katika maendeleo na ustawi wa wananchi. Hivyo basi ni vyema hatua
zichukuliwe kila mwenye haki ya kitambulisho hicho asiwekewe kikwazo chochote,
ili kuziba mianya kama hiyo inayotumiwa na baadhi ya watu kurejesha nyuma
maendeleo na umoja wetu.
Waheshimiwa Waandishi
Jambo
jengine ambalo napenda kuwahimiza tena wananchi, ni juu ya umuhimu wa kushiriki
kutoa maoni yao kuhusu mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Tume ya Mabadiliko ya Katiba inayoendelea kufanya shughuli za kuratibu maoni ya
wananchi nchi nzima tayari imefanya kazi hiyo katika mikoa ya Kusini Unguja na
Kusini Pemba kwa hapa Zanzibar. Na katika mikoa hiyo wananchi waliweza
kujitokeza vizuri kutoa maoni yao.
Nawasihi
wananchi wote wa mikoa ya Kaskazini Unguja, Kaskazini Pemba na Mjini Magharibi
wajitokeze kwa wingi kwenda kutoa maoni yao, wakati tume hiyo itakapofika
katika maeneo yao. Hatua hiyo ndiyo itakayotuwezesha kupata Katiba tunayoitaka yenye maslahi kwa
Zanzibar.
Hii
ni fursa adhimu ambayo tumekuwa tukiililia kwa siku nyingi juu ya haja ya
Watanzania kupata fursa ya kutoa maoni yetu, juu ya masuala yote yanayohusiana
na Muungano. Wananchi wawe huru kutoa maoni yao kwa uwazi na pawepo na
uvumilivu. Hata kama mtu hakubaliani na maoni, hoja zinazotolewa na mwengine,
inabidi asikilize kwa uvumilivu. Naye akipata fursa aseme yake kwa uwazi pia.
Na
mwisho wa yote hayo, ni kama ambavyo tunatarajia, maoni ya wengi ndiyo yatakayo
heshimiwe baada ya wale wachache kupewa haki yao ya kusikilizwa kwa kikamilifu.
Na sisi viongozi tunawajibu wa kusimamia hilo.
Waheshimiwa Waandishi
wa Habari
Sasa
naona tugusie masuala ambayo imekabidhiwa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais.
Kama
ambavyo mnafahamu ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais pamoja na mambo mengine,
imekabidhiwa majukumu mazito, majukumu ambayo kwa lugha ya siku hizi yanaitwa
Masuala Mtambuka (Cross Cutting issues), yakiwemo; Masuala yanayohusu Watu
Wenye Ulemavu, Mapambano dhidi ya Madawa ya Kulevya, Uhifadhi wa Mazingira
pamoja na Ugonjwa wa Ukimwi.
Waheshimiwa Waandishi
wa Habari
Katika
suala la mapambano dhidi ya UKIMWI, Wazanzibari tunapaswa sote tufahamu kuwa
ukimwi bado upo na unaendelea kuwaathiri watu wetu. UKIMWI ni tatizo
linalotugusa sote, wanawake, wanaume, vijana na watoto na ni janga ambalo
linasababisha matatizo makubwa katika ngazi za familia hadi serikali.
Serikali
kwa ushirikiano na wadau mbali mbali inachukua hatua kubwa katika kuweka
mazingira mazuri ya kupiga vita janga hili, lakini bado kuna maambukizi mapya
ya UKIMWI yanatokea.
Pia
wale walioathiriwa na maambukizi bado wanakabiliwa na vikwazo vingi, ikiwemo
kunyanyapaliwa na baadhi ya wanajamii. Aidha wanakumbana na hali ya umasikini
na uhaba wa dawa na huduma nyengine wanazozihitaji.
Kiwango
cha maambukizi ya ukimwi miongoni mwa watu wenye umri wa miaka 15 hadi 49 kimeendelea
kusimama kwenye 0.6, ikiwa ni sawa na watu 7,200 wanaokadiriwa kuishi na virusi
vya UKIMWI. Visiwani humu hali ya maambukizi ni mbaya zaidi kwa watu wa makundi
maalum, ambayo inakadiriwa kupita kiwango kilichopo katika jamii nzima.
Kwa
Zanzibar makundi maalum yanajumuisha; Watu wanaojidunga sindano za madawa ya
kulevya, Wanawake wanaouza miili yao, Wanafunzi katika vyuo vya Mafunzo na
Wanaume wanaofanya mapenzi ya jinsia moja.
Hata
hivyo, tafiti mbali mbali ndogo ndogo hivi sasa zinaendelea, ili kujua hali
halisi ya maambukizi ya UKIMWI Zanzibar, pamoja na mwenendo mzima wa maradhi
hayo na kuweza kuandaa mikakati thabiti kwa mujibu wa hali ilivyo katika
kudhibiti maambukizi mapya, na kuwasaidia wale ambao tayari wameambukizwa.
Aidha,
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais imeweza kufuatilia na kutathmini program
mbali mbali za UKIMWI. Mwaka jana jumla ya vikundi 24 vyenye miradi 36 ya
kujiongezea kipato vilifuatiliwa. Jumla ya shilingi milioni 15 kwa mfano walipatiwa
jumuiya ya ZAPHA+ kwa ajili ya kutekeleza shughuli zao mbali mbali zinazolenga
utekelezaji wa Mkakati wa Pili wa Taifa wa UKIMWI Zanzibar.
Waheshimiwa Waandishi
wa Habari
Nadhani
bado mnakumbuka Disemba Mosi mwaka jana tulizindua Mkakati wa Pili wa Taifa wa
UKIMWI wa Zanzibar. Mkakati huo umeandaliwa maalum kuongoza muitikio wa kitaifa
wa mapambano dhidi ya ukimwi kwa mwaka 2011/2016. Lengo kuu ni kuzuia kuenea
maambukizi ya virusi vya UKIMWI miongoni mwa Wazanzibari, kukabiliana na athari
mbaya za kiafya, ustawi na za kiuchumi zinazompata mtu mmoja mmoja , familia zao,
makundi maalum na Taifa kwa jumla.
Aidha,
Sera ya Taifa ya UKIMWI ya 2005 imejenga msingi mzuri wa kufanikisha mapambano
dhidi ya ukimwi. Sera hiyo imeweka mfumo wa utawala wa kisheria kwa ajili ya
mipango na harakati zote zitakazofanywa, ikiwemo kuzuia maambukizi mapya,
kutibu, kutunza na kuwasaidia walioambukizwa pamoja na kuimarisha uwezo wa
taasisi katika kutayarisha na kutekeleza program za ukimwi kwa kuzingatia
jinsia na haki za binaadamu wote.
Katika
kufanikisha mapambano dhidi ya UKIMWI Zanzibar tunaendelea kutoa wito kwa
jamii, wakiwemo wazazi na viongozi wa kidini waendelee kutoa nasaha na
kuwakataza vijana wetu na jamii kwa jumla, kuepuka matendo ambayo yatasababisha
watu kuambukizwa virusi vya UKIMWI.
Vijana
katika umri wao huiona dunia kama mahali pa uwezekano usiomalizika. Vijana
waliopewa miongozo na malezi mazuri ndio wenye mwelekeo mzuri wa kusalimika na
matatizo kama haya. Familia hazina budi kuwapa mawaidha vijana wao wa kike na
kiume tena kwa uwazi mkubwa kabisa juu ya ukimwi, ili wajiepushe.
Waheshimiwa
Waandishi wa Habari
Kuhusu Masuala ya Watu Wenye
Ulemavu, katika jamii ya Wazanzibari kama zilivyo jamii nyengine, miongoni
mwetu kuna Watu Wenye Ulemavu. Aidha, katika harakati za kimaisha za siku hadi
siku kuna sababu tafauti zinazopelekea idadi ya watu wenye ulemavu kuongezeka.
Kutokana na ukweli huo pamoja na wajibu wetu wa kibinaadamu, hatuna budi kuwa
na mipango na mikakati imara ya kuwasaidia watu wenye ulemavu. Kujitolea kwetu
kuwasaidia watu wenye ulemavu ndipo tutawawezesha wenzetu hawa kuishi kwa
furaha na kuondokana na vikwazo vingi vinavyowakabili hivi sasa.
Watu wenye ulemavu wana haki sawa
na watu wengine katika jamii. Wenzetu hawa wana kila haki ya kushirikishwa
katika mipango yote ya kimaendeleo, pamoja na huduma za kijamii. Lakini kwa
bahati mbaya sana hadi sasa watu wenye ulemavu wana kilio kikubwa cha
kutopatiwa haki zao stahiki ipasavyo, pia wana malalamiko mengi ya kunyanyaswa
na kudhalilishwa ikiwemo kijinsia.
Lakini pia katika jamii zetu
tunaona ni namna gani hata mwamko juu ya watu wenye ulemavu ulivyo mdogo. Hadi
leo kuna watu bado wanawaficha watoto na ndugu zao kwa sababu tu wana ulemavu.
Kutokana na hali hiyo ndio maana tukaamua kuanzisha zoezi la makusudi kabisa
kushajiisha jamii kuwafichua na kuwasajili watu wenye ulemavu.
Katika zoezi hilo linaloendelea
ambalo lilitanguliwa na mafunzo kwa Masheha na wakusanyaji taarifa, tumeweza
kusajili jumla ya watu 6,445 wenye ulemavu katika mikoa yote miwili kisiwani
Pemba. Awali zoezi hilo lilifanyika kwa majaribio katika Mkoa wa Kaskazini
Unguja, ambako jumla ya watu wenye ulemavu 3,002 walisajiliwa.
Aidha, katika kukuza na
kuendeleza mwamko juu ya masuala ya watu wenye ulemavu, Ofisi ya Makamu wa
Kwanza wa Rais imefanya kazi kubwa kuhakikisha masuala ya watu wenye ulemavu
yanaingizwa katika mipango ya taasisi za za Serikali. Hadi sasa ofisi imeweza
kusimamia uanzishwaji wa mpango huo na Maafisa Waratibu 16 tayari wapo katika
wizara mbali mbali kwa ajili ya hatua hizo na tayari wamepatiwa mafunzo maalum.
Kwa
upande mwengine, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais imehakikisha inajenga uwezo
kwa Idara ya Watu wenye Ulemavu pamoja na Baraza la Watu Wenye Ulemavu Zanzibar,
kwa kununua vifaa vya ofisini pamoja na vifaa vya utendaji kwa wafanyakazi
wake. Vile vile jumuiya tisa za Watu wenye Ulemavu zimeweza kupatiwa ruzuku
pamoja na visaidizi, yaani viti vyenye magurudumu mawili kwa watu 31 Unguja na
Pemba, ili kuwasaidia katika harakati zao za kimaisha.
Waheshimiwa Waandishi
wa Habari
Wajibu wetu
kwa watu wenye ulemavu ni mkubwa, lakini wakati ukweli ndio huo uwezo na nyenzo
zetu hazitoshi kuweza kuwajengea uwezo kikamilifu kwa mujibu wa mahitaji yao.
Lakini kwa kuthamini maisha na maendeleo yao, haki,
fursa na usawa kwa watu wenye ulemavu, wajibu wetu wa kuwawezesha kukabilina na
umasikini uliokithiri na upatikanaji mdogo wa huduma za afya tumeona kuna haja
kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Watu Wenye Ulemavu.
Mfuko
wa Maendeleo ya Watu wenye Ulemavu Zanzibar umeanzishwa kama Sheria No. 9 ya
mwaka 2006 inavyoagiza. Kama ambavyo waandishi wa habari ni mashihidi, Mfuko
huo tayari umezinduliwa rasmi wiki iliyopita na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar,
Dk. Ali Mohammed na kwakweli naona fahari kusema tumeanza vizuri.
Tunawashukuru
mwananchi mmoja mmoja, mashirika, jumuiya, taasisi za kiserikali na watu
binafsi, kwa namna walivyojitokeza na kuonesha moyo wao wa dhati kuwasaidia
watu wenye ulemavu Zanzibar. Moyo wao huo umewezesha mfuko huo kuanza na kiasi
cha T.SHS milioni 285. Tunaendeela kukuhimizeni wananchi na taasisi mbali mbali
kuendelea kuchangia mfuko huu kwani uchangiaji wa mfuko unaendelea.
Matumaini
yetu Mfuko huu utaweza kutoa mchango mkubwa kusaidia utatuzi wa changamoto
nyingi ambazo baadhi tumesha zianisha.
Waheshimiwa Waandishi
wa Habari
Kwa
upande wa Madawa ya Kulevya, Suala hili pia ni changamoto nyengine kubwa
inayotukabali katika nchi yetu. Na ukweli
ni kwamba tatizo hili sio tu kwa Zanzibar, bali kwa Dunia nzima. Kutokana na
ukubwa wa tatizo la madawa ya kulevya mataifa yanaungana kupambana na wazalishaji,
wafanyabiashara na walanguzi wa madawa haya ambao nao wamejidhatiti vilivyo.
Katika baadhi ya nchi tunashuhudia hata nguvu za kijeshi zikitumika kukabiliana
na tatizo hili.
Athari
za madawa ya kulevya zipo wazi na Zanzibar tunashuhudia hilo. Maisha ya watu
wetu hasa vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa yamekuwa hatarini. Lakini kwa
upande mwengine madawa ya kulevya yamekuwa chanzo kikuu cha maambukizi ya
maradhi ya ukimwi, ambayo nayo yanachukua nafasi kubwa kuteketeza maisha ya
binaadamu na kudhorotesha uchumi wa nchi.
Ofisi
ya Makamu wa Kwanza wa Rais imekuwa ikifanya kazi kubwa ya kuratibu na
kudhibiti utumiaji, biashara na usafirishaji wa madawa hayo. Kazi hizo zimekuwa
zikifanywa kwa karibu na wananchi pamoja na wadau mbali mbali katika mapambano
dhidi ya madawa ya kulevya, vikiwemo vyombo vya ulinzi na usalama, azma yetu
ikiwa ni kuinusuru Zanzibar kuwa kituo cha madawa ya kulevya na wananchi wake
kuathirika na madawa hayo.
Mikakati
yetu juu ya jambo hili imelenga zaidi kuwa na sheria zinazokwenda na wakati
ambazo zinakidhi haja ya kudhibiti madawa ya kulevya kwa wakati uliopo.
Katika
utekelezaji wa hatua hiyo tayari sheria Nam. 9 ya mwaka 2009 ilipitiwa na wadau
mbali mbali na baadaye kuwasilishwa katika kikao cha Baraza la Wawakilishi na kurekebishwa.
Aidha, uandaaji wa Sera ya Madawa ya Kulevya Zanzibar inaendelea na hivi sasa
kazi za kukusanya maoni ya wadau inafanyika.
Waheshimiwa Waandishi
wa Habari
Juhudi
kubwa katika kudhibiti madawa ya kulevya Zanzibar tumezielekeza katika kutoa
taaluma kwa jamii juu ya madhara yake, lakini pia kuwasaidia vijana walioingia
kwenye matumizi ya madawa haya, kwa kuwanasihi waache, pamoja na kuwashauri na
kuwasaidia njia zitakazowawezesha kupata kazi za kujiongezea vipato na
kuondokana na tabia ya kukaa bila ya kazi, tabia ambayo huwapa msongo wa mawazo
na kuwafanya waendelee kutumia madawa hayo.
Ofisi
ya Makamu wa Kwanza wa Rais katika mwaka wa fedha uliomalizika, iliweza kutoa
ushauri nasaha kwa familia 984 za watumiaji wa madawa ya kulevya, wakiwemo wanawake 510 na wanaume 474, ambapo
kati yao, 97 walikuwa watumiaji wa madawa ya kulevya.
Aidha,
ahadi ya kuzisaidia angalau fedha kidogo taasisi zinazotoa huduma za makaazi ya
vijana wanaoacha kutumia madawa ya kulevya (Sober Houses) ilitekelezwa na shilingi
9,900,000 zilitolewa, pamoja na televisheni na redio Unguja na Pemba.
Rasimu
ya muongozo wa nyumba za marekebisho za makaazi ya vijana wanaoacha matumizi ya
madawa hayo imekamilika. Aidha, suala la taaluma kwa jamii juu ya kupiga vita
madawa ya kulevya limeendelea kupewa umuhimu wa kipekee kwa kuandaa vipindi mbali
mbali vilivyoweza kurushwa hewani kupitia televisheni na redio. Vile vile Shehia
mbali mbali zilifanyiwa ziara za uhamasishaji na taaluma juu ya athari za
madawa hayo Unguja na Pemba.
Waheshimiwa
Waandishi wa Habari
Kuhusu suala la Kuyahifadhi na
kuyalinda mazingira yetu, pia hili nalo ni muhimu katika kudumisha Uhai na Ustawi
wa nchi yoyote ile. Hata hivyo changamoto inayojitokeza katika nchi nyingi,
ikiwemo Zanzibar ni uharibifu na uchafuzi mkubwa na wa makusudi wa mazingira
yetu. Kasi tunayoishuhudia ya ukataji ovyo wa misitu na uchimbaji wa mchanga na
mawe, kwa ajili ya kutengeneza matofali ni ya kutisha na iwapo haitadhibitiwa
nchi yetu ya Zanzibar kipindi kifupi kijacho itakabiliwa na janga kubwa la
kimazingira.
Aidha, upoteaji wa bioanuwai za
nchi kavu na baharini kwa jumla, utupaji ovyo wa taka na maji machafu, uvunaji
usioridhisha wa maliasili zisizojirejesha, hali inayosababisha kuachwa kwa
mashimo mengi, pamoja na ile tabia ya kuingizwa kwa wingi nchini vifaa chakavu
vya elektroniki, umeme na mifuko ya plastiki inaongeza ukubwa wa hatari hiyo ya
kimazingira.
Kwa upande mwengine suala la
mabadiliko ya tabianchi limekuwa ni tishio kubwa kwa dunia, na nchi zinazoathirika
zaidi ni zile za visiwa vidogo kama vyetu vya Zanzibar. Hali inayojitokeza
katika baadhi ya maeneo ya visiwa vyetu ambako maji ya bahari yamevamia
mashamba ya kilimo cha mpunga inatosha kuwa onyo kali kwetu na kufanya kila
linalowezekana kuyalinda mazingira.
Ofisi
ya Makamu wa Kwanza wa Rais katika kukabiliana na changamoto hizo za
kimazingira, ikiwemo suala la athari za mabadiliko ya tabianchi bado inaamini
utoaji wa elimu na kuzidi kukumbushana ndio njia muafaka na yenye umuhimu wa
kipekee.
Hata
hivyo hatua za kisheria zimeendelea na zitaendelea kuchukuliwa kwa wananchi au
miradi ya kiuchumi ambayo inaonekana kwa makusudi kupinga au kudharau sheria na
kanuni za uhifadhi wa mazingira.
Waheshimiwa Waandishi
wa Habari
Miongozi
mwa hatua zinazoendelea kuchukuliwa ni kutoa taaluma kwa njia ya semina,
vipindi vya televisheni na redio, pamoja na kuandaa ziara za kimasomo katika
maeneo mbali mbali, ili wananchi, viongozi wa maeneo na wanachama wa jumuiya
zisizokuwa za kiserikali, waweze kujifunza na baadaye kusaidia jamii kukumbusha
na kuhamasisha suala zima la kulinda, kutunza na kuhifadhi mazingira ya nchi
yetu.
Hatua
hizo zinajumuisha mafunzo juu ya
mabadiliko ya Tabianchi na mwelekeo wa Zanzibar katika kusimamia jambo
hilo, yalitolewa kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi. Aidha wafanyakazi 12
kutoka Idara ya Mazingira, Baraza la Manispaa Zanzibar, Halmashauri za Wilaya
ya Magharibi na Mabaraza ya Miji ya Chake Chake, Mkoani na Wete na baadhi ya
wawakilishi wa Jumuiya zisizokuwa za kiserikali waliwezeshwa kufanya ziara za
kujifunza huko Moshi na Arusha, ili waweze kupata uzoefu juu ya usimamizi wa
taka.
Ziara
za kujifunza za aina hii, pia ziliwahusisha viongozi 10 wa Kamati za Machimbo
ya Uwandani waliokwenda Mjini Mombasa Kenya kujifunza njia bora za shughuli za
uchimbaji na urejeshwaji wa maeneo yaliyochimbwa na kuepusha athari za
kimazingira.
Hatua
hizo zilichukuliwa kwa makusudi, ili kudhibiti kasi ya uchafuzi wa maeneo na
kuyaweka katika hali ya usafi, pamoja na kudhibiti athari za uchimbaji mawe kwa
ajili ya kazi za uchongaji matofali, maeneo ambayo yanahatarisha sana hali ya
mazingira hapa Zanzibar.
Eneo
jengine ambalo linaonekana ni sugu katika uharibifu wa mazingira yetu ni kwenye
fukwe na miradi ya hoteli za kitalii. Katika siku za hivi karibuni miradi 110
ya kitalii ilifanyiwa ufuatiliaji kuona inavyozingatia masuala ya kimazingira.
Taarifa ya ufuatiliaji huo si ya kufurahisha kwa sababu kati ya miradi mingi
ambayo ilionekana kukiuka kanuni ya kudhibiti matumizi ya ardhi kwa ajili ya
uwekezaji ya mwaka 2006.
Miradi
hiyo ilitakiwa kubomoa sehemu zilizojengwa kinyume na kanuni, lakini ni mradi
mmoja tu wa hoteli ya Zanzibar Ocean View ambao umetii amri hiyo.
Ofisi
ya Makamu wa Kwanza wa Rais ilichukua hatua ya kuwasilisha majina ya miradi
hiyo iliyoshindwa kufuata agizo hilo, Idara ya Mipango Miji na Vijiji kwa ajili
ya hatua za kisheria kwa mujibu wa kanuni.
Hata hivyo, lazima tukiri kwamba ipo haja
kubwa ya kuimarishwa Sheria na kanuni zetu za Mazingira, ili ziweze kukidhi
haja kwa mujibu wa wakati.
Kuhusu
usimamizi wa marufuku ya mifuko ya plastiki, baada ya Kanuni kufanyiwa
marekebisho, mafanikio makubwa yameweza kupatikana ambapo hadi unakamilika
mwaka wa fedha uliopita, watu 192 walikamatwa na kushitakiwa mahakamani na
jumla ya shilingi 7,650,000 zilizotokana na faini ziliingia katika mfuko wa
serikali.
Ni dhahiri changamoto ya
kimazingira ni kubwa, hivyo ni jukumu la
kila mmoja wetu kutekeleza wajibu wake wa kulinda na kuyahifadhi
Mazingira yetu ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa kizazi
cha sasa na kijacho.
Waheshimiwa
Waandishi wa Habari
Baada
ya kusema hayo natanguliza shukurani zangu nyingi, kwa viongozi na watendaji wa
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, akiwemo Waziri wangu wa Nchi mchapakazi na
muadilifu, Mheshimiwa Fatma Abdulhabib Fereji.
Vile vile shukurani hizo ziende
kwa Katibu Mkuu makini mwenye uzoefu na ujuzi wa taratibu za serikali ambaye
ndiye anayenishauri mimi na Waziri wa Nchi kuhusu masuala ya kitaalamu, mbali
kuwa Mtendaji Mkuu wa shughuli zote zilizochini ya ofisi hii. Huyo ni Dk. Omar
Shajak akisaidiwa na Naibu Katibu Mkuu, Dk. Islam Seif Salum, pamoja na
Wakurugenzi na Watendaji Wakuu wa Kamisheni zilizo chini ya ofisi hii. Wote hao
nawashukuru kwa msaada mkubwa wanaoendelea kunipa kwa muda wote huu.
Ahsanteni
sana.
No comments:
Post a Comment