Habari za Punde

Maendeleo ya elimu miaka 48 yalindwe



Na Hafsa Golo
 
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imepiga hatua katika kutanua  sekta ya elimu mjini na vijijini ambapo jumla ya wanafunzi 361,610 wanapatiwa elimu katika taasisi mbali mbali ili taifa liweze kuwa kuzlisha wataalamu wake katika  fani mbali mbali.

Akizungumza juu ya maendeleo hayo,Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Ali Juma Shamuhuna alisema jukumu hilo limeanza kuonesha dalili ya kufikiwakidogo kidogo kulingana na maendeleo ambayo sekta ya elimu imetapata katika miaka 48 ya elimu bila malipo.

Alisema  taasisi matumaini hayo yamekusanya nyanja nyingi na inaonekana dhahiri kwamba taasisi zinazotoa elimu kwa  wanafunzi hao zimefikia 713, zikiwemo Skuli za Maandalizi 253, skuli za Msingi kamili 194, Skuli za Sekondari kamili 107, Skuli za mchanganyiko, Msingi na sekondari pamoja 149, Vyuo vikuu  vitatu.


Alifahamisha kuwa uandikishaji wa wanafunzi katika ngazi ya elimu ya maandalizi imefikia asilimia 34.4, na ngazi ya msingi asilimia 121.5,ngazi ya sekondari asilimia 67 sambamba na uwiyano kati ya wanafunzi wa kiume na wanafunzi wa kike wamekuwa wakilingana katika ngazi za msingi na sekondari.

Alisema hatua hiyo ya maendeleo imefikiwa kutokana na ushirikiano makubwa yaliopo kati ya wananchi na serikali kwani wananchi wamekuwa wakitoa michango  katika maeneo mbali mbali  hasa kwa ujenzi wa madarasa.


"Pia ninawapongeza kwa juhudi kubwa kuhakikisha watoto wenu wanaandikishwa na wanahudhuria masomo katika skuli zilizokaribu na maeneo munayoishi,ninawaomba tuendelee kushirikiana ili sekta yetu ya elimu iweze kupata maendeleo zaidi."alisema  

 Akizungumzia upande wa elimu ya juu, alisema kuwa hatua ya maendeleo imefikiwa kwani hivi sasa zipo taasisi nne zinazotoa elimu ya Chuo kikuu,akizitaja taasisi hizo alisema Chuo kikuu cha Taifa cha Zanzibar,Chuo Kikuu cha Zanzibar, Chuo Kishirikishi cha Elimu Chukwani na Taasisi ya Fedha iliyopo Chwaka.

Aidha,  alisema pamoja na mafanikio makubwa yaliofikiwa katika sekta ya elimu, bado yapo matatizo mbali mbali yanayoikumba sekta ya elimu yakiwemo uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi, uhaba wa vikalio na vifaa vya maabara.

Shamuhuna alisema azma ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutatua matatizo hayo hatua kwa hatua, ikiwa moja wapo ni kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID) ambapo imeanza kutekeleza mradi wa TZ21 wa kupatiwa kompyuta kwa kuhifadhia kumbukumbu na kutumiwa kwa kufundishia na kujifunzia.

Kutokana na kiwango hicho cha wanafunzi ambao wamekuwa wakipata huduma muhimu ya elimu katika taasisi mbali mbali alisema ni jambo muhimu  kwa taifa  na yataweza kufikiwa  malengo yaliokusudiwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.