Na Mwandishi maalum
UKOMBOZI
mkubwa zaidi wa wakulima wa Tanzania utafikiwa mwishoni mwa mwaka ujao wakati serikali
inapopanga kuzindua soko la mazao (Commodity Exchange) ambalo kazi yake kuu
itakuwa ni kuwahakikishia soko la uhakika zaidi na bei za uhakika zaidi
wakulima.
Dk.
Eleni Z. Gabre Madhin ambaye anashauri kuhusu uanzishwaji kwa soko la mazao
katika Tanzania amemwambia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya
Mrisho Kikwete kuwa soko hilo linaweza kuanzishwa mwishoni mwa mwaka ujao ili
mradi tu mchakato wa kuanzishwa kwake uanze Disemba, mwaka huu.
Rais
Kikwete na Dk. Eleni Madhin wamekutana kwenye hoteli ya Ngurdoto mjini Arusha
ambako wote wawili wanahudhuria mkutano wa pili wa Taasisi ya Mapinduzi ya
Kijani katika Afrika (AGRA).
Dk.
Eleni Madhin ambaye ni Mwanzilishi na Mtendaji Mkuu wa Soko la Mazao la
Ethiopia ameshauri kuwa kikosi kazi cha kuanzishwa kwa soko hilo kianzishwe
haraka iwezekanavyo ili kuwezesha mchakato wa kuanzishwa kwa soko hilo uweze
kuanza Disemba, mwaka huu.
“Kama
tukianza mchakato Disemba, mwaka huu, na tukiweza kuunda kikosi kazi katika
wiki chache zijazo, basi naweza kukuhakikishia kuwa utaweza kuwa na soko la mazao
linalofanya kazi mwishoni mwa mwaka 2013,”
alisema Dk. Eleni Madhin na
kuongeza:“Ushauri wangu ni kwamba Rais ukubali kuanzisha kikosi kazi cha taifa kikishirikisha
maofisa kutoka taasisi mbali mbali zikiwamo Wizara ya Kilimo, Wizara ya Fedha,
Wizara ya Biashara na Viwanda, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA), Mamlaka ya Soko la Mitaji na taasisi nyingine ambazo unaona
zinafaa ili kazi hii ianze mapema iwezekanavyo.”
Rais
Kikwete pia amekutana na kufanya mazungumzo na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya
Mbolea ya Yara, Jorgen Ole Haslestad.
Viongozi
hao wawili walizungumzia uwekezaji wa Yara katika sekta ya kilimo nchini Tanzania.
Aidha,
Rais Kikwete amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Shirika la Kimataifa ya
Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Dk. Konaye Mwanze.
Dk.
Mwanze amemwambia Rais Kikwete kuwa Tanzania inatarajiwa kupata msaada
wa kati ya dola za Marekani milioni 75 na milioni 80 katika muhula wa kati ya
mwaka 2014 na 2017.
No comments:
Post a Comment