Habari za Punde

Vyombo vya habari visaidie maendeleo




 
KUSIMAMIWA ipasavyo kwa  majukumu ndani ya sekta ya habari kwa kiasi kikubwa kutaweza kusaidia vyombo vya habari kutekeleza dhamana zake pamoja na kujua wajibu wake ili kuleta maendeleo katika sekta hiyo.

Akizungumza katika mkutano uliojumuisha wamiliki mbali mbali wa vyombo  vya habari, Waziri wa Habari Utamaduni, Utalii na Michezo Zanzibar,  Said Ali Mbarouk alisema wizara yake ina jukumu kubwa la kusimamia sekta ya habari ili kuhakikisha lengo linafikiwa.


Alisema wizara ina kazi kubwa ya kusimamia sera ya habari na utangazaji  kwa kuitekeleza pale ambapo wakiona ina upungufu kwa lengo la kufanya tathmini ili kuirekebisha kwa pamoja.

Waziri huyo alisema ni wakati sasa kwa sekta ya habari kupiga hatua kubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki kutokana na kwamba Zanzibar ina historia pana katika sekta hiyo hali ambayo itasaidia pia kurejesha heshima ya vyombo vya habari.


Alisema nchi inapokosa uhuru wa habari huwa hakuna maendeleo hivyo ni vyema kukabiliana na changamoto zilizopo ili kulinda hadhi  ya habari na upatikanaji wa habari hizo.

Sambamba na hayo ameviomba vyombo vya habari kupanga mikakati ambayo itaratibiwa kati yao na Wizara kwa lengo la kuendeleza sekta hiyo kielimu, kifikra na iweze kutumika katika kuleta mageuzi ya ulimwengu.

 Akichangia mada mmoja  wa washiriki wa kikao hicho Kaimu Mkuu wa Chuo cha habari Zanzibar, Rashid Omar  alisema ni jambo la msingi kufanyiwa mapitio sera na sheria ya utangazaji kutokana na kutumia vibaya lugha ya kiswahili wakati wa uwasilishaji wa kazi zao.

Amevitaka vyombo vya habari  vya binafsi na serikali kufanya utafiti wa kina wakati wa kukidhi mahitaji ya wafanyakazi kwa kuzingatia mazingira na taaluma waliyonayo.

Nae Hafidh Kassim alisema serikali inavipa mzigo mkubwa sana vyombo vya binafsi katika suala la kuajiri pamoja na kutozwa kodi kubwa jambo ambalo linapelekea kuzorotesha mwenendo mzima wa kubadilisha mitambo yake kutoka  katika mfumo wa analogia na kwenda digitali.



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.