LILONGWE, Malawi
RAIS
wa Malawi, Joyce Banda, ameiondoa nchi yake katika mazungumzo ya mgogoro wa
mpaka wa Ziwa Nyasa na Tanzania, kutokana na kile anachodai kuwa uchokozi,
ubabe na vitisho vinavyofanywa na
serikali ya Tanzania
dhidi ya raia wake.
Rais
Banda alisema Malawi
sasa itaufikisha mgogoro huo katika mahakama ya kimataifa.
Nchi
hizo mbili ziliingia katika mvutano mkubwa wa Ziwa hilo, ambalo linaaminika
kuwa na rasilimali kubwa ya mafuta na gesi.
Rais
Banda alisema amemuagiza Waziri wake wa Mambo ya Nje,kuvunja kabisa mazungumzo
na Tanzania baada ya nchi
hiyo kutangaza rasmi uzinduzi wa ramani mpya katika eneo la Ziwa hilo.
Aidha
alisema nchi yake haitavumilia unyanyasaji unaofanywa na Tanzania dhidi ya raia wake wanaofanya shughuli
za uvuvi katika Ziwa hilo.
Banda
alitoa kauli hiyo wakati alipowasili mjini Lilongwe akitokea mjini New York,
Marekani alikokwenda kuhudhuria mkutano wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa.
“Wakati
naondoka kwenda New York, nilifikiria kuwa mgogoro huu ungemalizwa kwa njia ya
mazungumzo,” alisema.
“Lakini
wakati nipo njiani, Tanzania walizindua ramani mpya, wamewadhalilisha,
kuwatisha na kuwabugudhi wavuvi wetu na
wanatembea na boti zao katika Ziwa letu,” alisema kwa uchungu mama huyo.
“Suala
limekuwa tete sasa na tunalichukua katika hatua nyengine. Tanzania imetishia
kushambulia boti za Malawi zitakazoonekana katika Ziwa Nyasa,” alisema Banda.
Kiongozi
huyo wa Malawi alisema alifanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa UN, Ban Ki-moon na
kumjulisha juu ya nia ya Malawi
ya kulifikisha suala hilo
katika mahakama ya kimataifa ya usuluhisi wa migogoro.
Banda
alisema katika mazungumzo yake na Rais Kikwete walipokutana katika mkutano wa
SADC walikubaliana kumaliza mgogoro huo kwa njia ya mazungumzo.
Hali
katika mpaka wa nchi hizo mbili bado uko swahari, lakini uamuzi huo wa Banda
huenda unaashiria kuwa mgogoro huo umeingia katika sura mpya.
Wakati
huo huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki Moon amepongeza msimamo wa
Tanzania kutafuta majawabu
ya amani na ya kujadiliana kuhusu mzozo wa mpaka kati yake na Malawi kwenye Ziwa Nyasa.
Ki
Moon alisema uamuzi wa Tanzania
ndiyo njia sahihi na inayokubaliwa kimataifa kutafuta na kupata suluhisho la
migogoro ya namna hiyo.
“Majuzi nilikutana na Rais Joyce Banda wa Malawi na akanielezea mzozo wa mpaka kati ya Tanzania na Malawi kwenye Ziwa Nyasa na mazungumzo
ambayo nchi zenu mbili zinafanya ili kupata ufumbuzi wa amani. Hii ndiyo njia
sahihi na Umoja wa Mataifa unaunga mkono njia hiyo,” alisema.
Rais
Kikwete amemweleza Katibu Mkuu huyo wa UN kuwa Tanzania bado inaamini kuwa njia
sahihi na maelewano zaidi ni kutafuta ufumbuzi wa mvutano huo wa mpaka kwa njia
ya mazungumzo.
“Wazo la awali la kutafuta ufumbuzi wa tatizo
hili la miaka mingi sana lilitokana na Rais wa Malawi, marehemu Bingu wa
Mutharika ambaye aliniandikia barua ya kutaka nchi zetu zianze mazungumzo
kuhusu mzozo huo. Nasi tulikubali. Hivyo, ndivyo tulivyoanza kuzungumza,”
alisema
Rais Kikwete.
Alisema
Tanzania
inaongozwa na msingi mkuu wa mipaka inayopita kwenye maeneo ya maji ambako
mipaka hiyo inakuwa katikati.
“Mpaka
kati ya Malawi na Msumbiji kwenye ziwa hilo hilo, umekuwa katikati ya Ziwa
tokea mwaka 1954 wakati nchi hizo zilipokubaliana kusahihisha makosa ya kuuweka
mpaka huo nje ya Ziwa. Mpaka wa Tanzania na Malawi kwenye mto mkubwa zaidi
unaoingiza maji katika Ziwa Nyasa uko katikati ya mto wenyewe,” alisema Kikwete.
“Kila mahali ambako nchi zinatengenishwa na
maji, mpaka unakuwa katikati ya nchi. Sisi tunadhani hata kwenye mpaka wetu wa
Malawi kwenye Ziwa Nyasa ni lazima uwe katikati ya Ziwa,” alisema.
Lakini
alisema katika hali ya sasa wananchi wa Tanzania wanapokunywa maji ya Ziwa
Nyasa wanaambiwa wanakunywa maji ya Malawi, kila wanaposafiri ndani ya Ziwa
kufanya shughuli zao wanaambiwa wanasafiri kwenye maji ya Malawi.
No comments:
Post a Comment