Na Abdi Suleiman
LIGI ya soka daraja la kwanza taifa Pemba, imezidi kutimua vumbi huku timu vigogo zikichezea vipigo katika viwanja viwili tafauti mwishoni mwa wiki.
Katika uwanja wa Gombani, timu ya Kizimbani ilipeleka kilio katika kijiji cha Kangani baada ya kuitandika Fufuni SC mabao 2-1, katika mchezo uliokuwa mgumu na kwa timu zote hizo.
Mabao ya Kizimbani katika pambano hilo, yaliwekwa nyavui na mchezaji Ali Othman katika dakika ya 39, pamoja na Salum Nia aliyehitimisha ushindi huo kwenye dakika ya 64.
Goli la kufutia machozi kwa Fufuni FC, lilifungwa na Mohammed Ali dakika moja kabla mchezo kumalizika.
Pambano jengine la ligi hiyo, lilirindima katika uwanja wa Makombeni, timu ya Afrikan Kivumbi ya Mwambe ikaitandika Madungu United magoli 3-0, huku mchezaji wa Madungu Abdulkarim Amour akitolewa nje kwa kadi nyekundu kutokana na mchezo mchafu.
Nao wakongwe wa soka kisiwani Pemba Mwenge, wakairovya Mila mabao 4-0 katika uwanja wa Kinyasini, Coast Boys ikainyuka Small Tiger 1-0 huko Makombeni, na Selemu Rangers ikairamba Maendeleo Manta bao 1-0 katika dimba la Kinyasini.
No comments:
Post a Comment