Habari za Punde

Dewji aishangaa Yanga

Aitaka ijitambue, isilumbane na mdhamini
 
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
 
WAKATI klabu za Yanga na African Lyon zikiendelea kusuguana na mdhamini wa ligi kuu Tanzania Bara, Vodacom, klabu hizo zimetakiwa kujitambua na kuacha malumbano yasiyo na faida.
 
Aliyekuwa mfadhili wa Simba Azim Dewji, amezishauri klabu za ligi kuu Bara, zianze kujitambua ili ziweze kunufaika kwa mambo mengi zaidi, badala ya kutumia muda mrefu kulumbana kwa mambo madogo.
 
Dewji alitolea mfano wa nembo ya Vodacom katika jezi za klabu, ambayo imeifanya Yanga igomee kutumia jezi zilizotolewa na wadhamini kwa vile zina alama yenye rangi nyekundu, ambayo ni ya watani wao Simba.
 
Mfanyabiashara huyo alisema kuwa, kama klabu za Tanzania zingekuwa zinajitambua, kamwe zisingepoteza muda kwa malumbano ya nembo, bali zingeangalia maslahi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Dewji alisema klabu kubwa kama Simba na Yanga, zinapaswa kujenga hoja nzito kwa wadhamini, ili ziweze kunufaika zaidi kwa kuwa zina thamani kubwa kutokana na ukongwe wao na utajiri wa wafuasi ndani na nje ya Tanzania.
 
“Sawa wana haki, lakini klabu zetu ifike mahali zijitambue. Wavuke hapo, mfano Simba na Yanga zijenge hoja za kupata fedha zaidi kwa wadhamini, kwamba ili zivae jezi na nembo, zilipwe vizuri kulingana nahadhi halisi ya klabu hizi”, alieleza.
 
“Haiingii akilini kuona zimeshindwa kujenga ushawishi hata baada ya kuwekwa kundi moja na timu ambazo hazina wanachama wala ofisi, lakini kwa mujibu wa mkataba zote zinalipwa shilingi milioni saba kwa mwezi”, aliongeza Dewji.
 
Alihoji ni vipi Yanga yenye utitiri wa wanachama na wafuasi, utajiri wa majengo, likiwemo la klabu lenye thamani ya shilingi bilioni mbili, ilipwe sawa na African Lyon ambayo haina wanachama wala ofisi. “Si kama naidharau Lyon, la hasha, bali ndio uhalisia kwa sababu kama ni kunufaika, Vodacom itanufaika zaidi kwa Yanga kutokana na wafuasi wake wengi kuliko Lyon, kwa nini wasitumie mwanya huo kujenga hoja?”, alihoji.
 
Alisema kutokana na hadhi ya klabu za Simba na Yanga, angalau kila moja iambulie shilingi milioni 250 kwa mwaka, na jezi za hadhi ya juu zitakazolingana na klabu hizo.
 
Klabu ya Yanga imeingia katika mgogoro juu ya kutovaa jezi zenye nembo ya Vodacom ambayo ina rangi nyekundu, huku Lyon ikitaka iruhusiwe kuvaa jezi za mdhamini wake binafsi, kampuni nyengine ya simu, Zantel.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.