NA MAELEZO ZANZIBAR
Naibu Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar Issa Haji Usi (Gavu) amewataka washiriki wa Semina ya Usimamizi Salama wa Abiria na Vyombo vya Baharini kuhakikisha mafunzo wanayoyapata katika Semina hiyo yanaleta tija ili kuiwezesha Sekta ya usfiri wa baharini nchini kupiga hatua ya kimaendeleo.
Gavu ameyasema hayo leo alipokuwa akifungua Semina ya siku tano inayohusu Usimamizi Salama wa Abiria na Vyombo vya Baharini katika ukumbi wa Hoteli ya Ocean View iliyopo Kilimani mjini Zanzibar.
Amesema Semina hiyo imekuja wakati muafaka ambapo sekta ya Usafirishaji inakabaliwa na changamoto nyingi ikiwemo ya usimamizi ambapo wadau wa Semina hiyo watajifunza namna bora ya kuimarisha Sekta hiyo.
Ameongeza kuwa mafunzo watakayoyapata wanasemina hao yatakuwa kwa ajili ya taifa katika kuimarisha kiwango cha usalama wa abiria wanaotumia usafiri wa baharini ili kuweza kunusuru ajali ambazo zinaweza kuepukika.
Amefahamisha kuwa Jukumu la Serikali ni kupanga sheria na taratibu zinazoongoza sekta ya baharini kama ilivyo kwa sekta nyingine na kwamba watekelezaji wa Sheria hiyo ni wadau hao wa semina kwa kushirikiana na wananchi husika.
Aidha amewataka wadau hao kutoa mashirikiano kwa wakufunzi wa Semina hiyo na kuchangia mawazo yao kikamilifu katika mijadala ili lengo la Semina hiyo liweze kutimia.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Usafirishaji Baharini Zanzibar (ZMA) Ahmed Sheikh Abrahman amelishukuru Shirika la kimataifa la Usafirishaji wa Baharini IMO kwa kuweza kukubali kushirikiana na ZMA nakufanikisha Semina hiyo kufanyika Zanzibar.
Amesema ili malengo ya semina hiyo yaweze kutimia ushirikiano na umakini unahitajika ambapo pia aliwataka Washiriki wa Semina hiyo kutoa michango yao bila ya uoga ikiwemo kukosoa ili kupata suluhu la kueleweka.
Kwa upande wake Mkufunzi wa Semina hiyo kutoka nchini Senegal Babakar Diop amesema lengo kuu la Semina hiyo ni kuiongezea uimara Mamalaka ya Ushafirishaji Baharini Zanzibar ili kuweza kufanya kazi zake kwa ufanisi ikiwa ni pamoja na kukabiliana na majanga.
Ameongeza kuwa atatumia uwezo wake wote kuwaelewesha washiriki wa Semina hiyo njia za kuimarisha usafirishaji salama na uwezo wa kukabiliana na majanga na kwamba anachohitaji ni mashirikiano kutoka kwao.
Semina hiyo ya siku tano ya Usimamizi Salama wa Abiria na Vyombo vya Baharini imeandaliwa na Mamlaka ya Usafirishaji Baharini Zanzibar (ZMA) kwa kushirikiana na IMO ambapo lengo lake ni kuijengea uwezo ZMA kufanya kazi kwa ufanisi na kukabilina na majanga
No comments:
Post a Comment