Habari za Punde

Ngeleja kuvunja makundi CCM

Na Rose Chapewa, Morogoro, Dotto Mgaza,Sengerema
 
MBUNGE wa Viti Maalumu kupitia CCM, Sara Msafiri amesema makundi yanayoendelea ndani ya chama ndiyo yanayokimaliza, na kuwataka wanachama kuhakikisha wanayamaliza.
 
Kauli hiyo aliitoa katika wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro, wakati akifungua mkutano wa uchaguzi wa wagombea mbalimbali wa chama hicho.
 
Aliwataka wanachama kutokukubali kugawanywa kwa makundi na baadhi ya wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi, na kwamba kufanya hivyo ni kukidhoofisha chama.

“Kuna makundi ya muda mrefu hapa Mvomero, kabla hata rais Jakaya Kikwete hajapata urais mpaka anakaribia kumaliza urais yapo, tatizo ni nini, tuna tatizo ndani ya siasa zetu, tuna vikwazo tubadilike,” alisema.
 
Aliwataka wagombea wa nafasi mbalimbali za chama kuacha tabia ya kuwagawa wanachama, na kwamba kushindwa kwao isiwe chanzo cha kuwagawa wanachama. Mbunge huyo aliwataka kutotishika na mabadiliko yaliyopo ndani ya siasa na kwamba mabadiliko hayo yanafanywa na vijana na kwamba chama kina wajibu wa kuendana na mabadiliko hayo kwa kuondokana na siasa za zamani.
 
Aliwataka wanachama kutafuta mbinu mbadala ili kuhakikisha CCM kinakubalika kwa wananchi hasa vijana, kutokana na kundi hilo kukimbilia vyama pinzani. Hata hivyo aliwataka wagombea watakaoshinda, baada ya uchaguzi wahakikishe wanawatafuta vijana watakaojiunga na chama hicho na kwamba chama kinatakiwa kuwa na vijana.
 
MBUNGE wa jimbo la Sengerema,William Ngeleja ameahidi kuyavunja makundi mabaya yaliyomo ndani ya CCM wilayani Sengerema mkoani Mwanza. Ngeleja alisema makundi ndio yanayosababisha chama kutosonga mbele na badala yake kinazidi kudidimia kimaendeleo.
 
Kauli hiyo aliitoa usiku wa kuamkia jana baada ya kutangazwa mshindi katika nafasi ya NEC kupitia wilaya katika uchaguzi mkuu wa chama hicho uliOfanyikia viwanja vya shule ya Sekondari St.Carol.
 
“Ndugu wajumbe nia ya kuwatumikiwa wananchi wa wilaya ya Sengerema ninayo…nakubali kutumwa nikatumika,nawashukuru sana naomba ushirikiano wenu,” alisema Ngeleja. Hata hivyo alisema kwa kushirikiana na wananchi wa wilaya ya Sengerema kupitia CCM atahakikisha anashirikiana nao ili kusongesha mbele gurudumu la maendeleo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.