Habari za Punde

Hofu yatanda wazazi CCM. Lowassa apeta NEC



Na Joseph Ngilisho, Mwantanga Ame
WAZIRI Mkuu mstaafu, Edward Lowasa ameshinda katika kinyang’anyiro cha kuwania nafasi ya mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) baada ya kuwabwaga wapinzani wake wawili.

Lowasa alipata kura 709 na kuwashinda wapinzani wake Nanai Konina aliepata kura 44 na Dk. Salash Toure aliepata kura saba.

Kabla ya uchaguzi huo, wapinzani wa Lowasa walidai kufanyiwa mizengwe wakati wa kurejesha fomu kwani katibu hakuwepo ofisini.

Lowasa amefuta aibu iliyompata mtangulizi wake, Frederick Sumaye ambaye aliangushwa na Dk. Mary Nagu katika uchaguzi wa NEC kupitia wilaya ya Hanang.
Akizungumza baada ya ushindi huo,Lowasa aliwapongeza wananchi kwa kuendelea kumuamini na kumuunga mkono.



Alisema ataendelea kuwatumikia wananchi kwa kulinda na kutetea ilani ya chama na kuhakikisha chama kinashinda katika uchaguzi mkuu ujao.

Kuhusu mipango yake ya kugombea urais, alisema bado ni mapema ila atatoa tamko muda utakapofika.


Baada ya kitimtim cha kuanguka kwa baadhi ya vigogo ndani ya chama cha Mapinduzi, hofu imeanza kuhamia kwa wagombea wa Jumuiya za chama hicho wanaoanza kuchaguana leo.

Hofu hiyo, imeanza kujionesha baada ya baadhi ya vigogo hao kubwagwa vibaya katika uchaguzi wa kuwania nafasi sita za wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).

Baadhi ya wanachama wamekuwa wakitabiri kuwa huenda uchaguzi wa Jumuiya hizo ukaja na sura mpya kama ilivyotokea katika nafasi sita za kuwania ujumbe wa NEC.


Jumuiya ambazo zinatarajia kufanya uchaguzi wake leo  nchini kote, ni wa Jumuiya ya wazazi  ngazi ya Mkoa.

Akizungumza na Zanzibar Leo, Katibu Mwenezi wa CCM mkoa wa mjini, Maulid Issa, alisema anatarajia uchaguzi huo utakuwa wenye mvuto zaidi, kutokana na kujitokeza kwa sura nyingi mpya zinazotaka kuwania nafasi ndani ya jumuiya hiyo.

Katibu huyo alisema ni kweli ndani ya mchakato huo zipo sura nyingi mpya ambazo suala la mabadiliko lazima litatokea kutokana na wingi wa wanawake ambao wamejitolea kuwania nafasi hizo.

 Akiwataja watakaowania kinyanganyiro hicho  kwa nafasi ya Mwenyekiti kwa wilaya ya magharibi, alisema wote ni wapya akiwemo Ali Amour Ali, Amina Ali Mohammed, Vuai Ali huku wanaowania nafasi ya baraza kuu wazazi taifa, ni Fatma Abeid Haji, Issa Abdalla Bori na Asha Khamis Bakari.

Watakaowania nafasi ya wajumbe wa baraza kuu mkoa, alisema  ni watu tisa, ambapo kati ya hao ni watatu tu ndio wanaotarajiwa kuchaguliwa katika kinyanganyiro hicho.

Wagombea watakaoingia katika mchakato huo  kuwania nafasi hizo ni pamoja na Abass Hassan Juma, Ali Salim Suleiman, Ameir Sose Ameir, Gharib Addy, Habiba Ali Mohammed, Mjumbe Msuri Mjumbe, Shabaani Seif Mohammed, Msekwa Mohammed Ali na Zamzam Ali Rijal.

Wakati hali hiyo ikianza kuonekana katika uchaguzi wa jumuiya ya wazazi, tayari na katika jumuiya ya wanawake Tanzania, nako kumeanza kujaa hofu kwa wagombea nafasi mbali mbali ndani ya chama hicho.

Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania, Asha Bakari Makame, anautabiri uchaguzi huo kuwa utakuwa wenye mvutano mkubwa kutoka na baadhi ya waliojitokeza kuwania nafasi hizo, kuonekana kuwa na ari ya ushindi.

Alisema suala kubwa ambalo litapaswa kuzingatiwa na wagombea waliojitokeza kuwania nafasi hizo, ni kuzingatia kanuni za uchaguzi bila ya kupitisha vitendo vya rushwa.

Alisema ikiwa kanuni za uchaguzi hazitafuatwa kwa uhuru  na haki, ni  wazi kuwa inaweza kujitokeza mvurugano ambao utachangia kuwepo matatizo  ya kutoaminiana.

Alisema wanachama waliojitokeza  kuwania nafasi ndani ya chama hicho, hivi sasa wametambua umuhimu wa jumuiya za chama kuwa ni sehemu ya kuimarisha chama na ndio sababu wamejitokeza kwa wingi kuwania nafasi hizo.

Alisema jumUiya hiyo ambayo inatarajia kufanya uchaguzi wake kuanzia Oktoba 6, na 7, 2012, itahakikisha uchaguzia  huo unakuwa wenye mvuto mkubwa.

Hata hivyo, Makamu huyo aliwataka wagombea wa chama ambao watashindwa kupata nafasi katika uchaguzi huo kuwa wastaahamilivu na kuyakubali matokeo na sio kuanzisha makundi au kununiana.

Alisema hilo ni moja ya jambo la kuzingatiwa kwa vile CCM kina kazi kubwa katika uchaguzi wa 2015 na ni lazima kipate viongozi wazuri ambao wataweza kukitumikia ipasavyo.

Wakati kukiwa na hali hiyo ndani ya Jumuiya upande wa uchaguzi ngazi ya Wilaya, bado baadhi ya vigogo wameendelea kuanguka.

Wilaya ya Kati walioangushwa yumo aliyekuwa mwakilishi wa jimbo la Uzini ambaye pia aliwahi kushika nafasi ya Naibu Waziri wa Maji, Nishati na Ardhi,Tafana Kassim Mzee, aliekuwa Mbunge wa Mpendae, Issa Kassim Issa aliekuwa Mwakilishi wa Chwaka, Haidar Ali Abdalla na aliyekuwa Mwakilishi wa wanawake, Mosi Amour Kajala.

Hata hivyo sura mpya zilizofanikiwa kuzikwaa nafasi sita kwa wilaya hiyo ni pamoja na Waziri Ramadhan Abdalla Shaaban, Balozi Ali Karume, Khalifa Salum Suleiman, Asha Mshimba, Kombo Hassan Juma na Haji Mkema Haji.

Wilaya ya Kusini waliofshinda nafasi ya Uwenyekiti ni Abdul-azizi Hamad Ibrahim (40), aliepata kura 203, Idrissa Makame Haji (64) aliepata kura 87  na Mjaka Haji Mjaka (67) aliepata  kura 85.

Walioshinda nafasi sita NEC kwa Wilaya hiyo ni Dk. Mwita Haji Ali (62), aliepata kura 164, Haji Ameir Timbe, kura 159, Jafar Sanya Jussa (kura 301), Haji Ameir Haji (kura 199), Mussa Makame Pandu  (Dere) kura 233 na Ramadhan Nyonje Pandu aliepata kura 159.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.