Habari za Punde

Zanzibar yavuta wawekezaji sekta ya kilimo


Joseph Ngilisho, Arusha
 
ZANZIBAR zimewakaribisha  wahisani katika sekta ya kilimo, kusaidia wakulima wadogo kuboresha kilimo chao ili taifa liweze  kuwa na uhakika wa chakula na kukabiliana na umasikini.

Akizungumza katika mkutano wa mapinduzi ya kilimo mjini Arusha, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi alisema wakulima wa Zanzibar kama walivyo wakulima wengine wadogo wanakabiliwa na tatizo la matumizi ya zana duni za kilimo, na ukosefu wa  mbegu za kisasa.


Alisema ingawa serikali ya Zanzibar imekuwa na programu mbali mbali za kusaidia sekta ya kilimo lakini inakabiliwa pia na tatizo la ardhi hasa kutokana na ongezeko la watu.
 
Hata hivyo, alisema licha ya uchache wa ardhi lakini hiyo iliyopo kama itatumiwa vizuri hasa kwa zao za karafuu, Zanzibar itakuwa na mafanikio makubwa.


Hivyo,  alisema Zanzibar inafungua milango kwa wawekezaji wa ndani na wa kigeni kuwekeza katika sekta ya kilimo.

Balozi Seif alisema wakuliwa wadogo wakiwezeshwa wanaweza kuzalisha kwa kiwango kikubwa na kuipunguzia serikali kuagiza chakula kutoka nje.

Kwa upande wake  Makamu wa Pili wa Rais wa Burundi,  Gabriel Ntisezerana, alisema Burundi  imefanikiwa kuwa na ardhi bora yenye rutuba lakini bado haijatumika ipasavyo katika kusaidia sekta ya kilimo.

“Bado wakulima wetu wadogo wanakabiliwa na matatizo ya kutokuwa na zana bora za kilimo na matumizi mazuri ya pembejeo,"alisema Ntisezerana.

Mkutano huo, ulioandaliwa na taasisi ya mapinduzi ya kijani(AGRA) unaendelea katika hoteli ya Ngurdoto mjini Arusha na unashirikisha wataalam wa sekta ya kilimo na wadau wengine zaidi ya 1200 toka bara la Afrika na nje ya Afrika.

Wakati huo huo Mwanzilishi wa Taasisi ya Mapinduzi ya Kijani barani Afrika(AGRA),ambaye pia ni mke wa tajiri mkubwa duniani, Bill Gates, Melinda Gates,  ameimwagia sifa Tanzania,kutokana na kuwa na mikakati madhubuti ya kuimarisha  sekta ya kilimo.

Akizungumza katika mkutano wa pili wa mapinduzi ya kijani barani Afrika,katika hoteli ya Ngurdoto  Melinda Gates alisema,Tanzania ni moja ya mataifa ambayo yanatarajiwa kuwa na maendeleo makubwa katika sekta ya kilimo.

Alisema alitembelea bara la Afrika kwa mara ya kwanza miaka 19 iliyopita na alifika Tanzania na tangu wakati huo, kilio kikubwa cha wananchi hasa akina mama ni umasikini ambao unachangiwa na kilimo duni.
 
Alisema taasisi yake, imekuwa ikisaidia katika kilimo na sekta ya afya kwa kutambua umuhimu wa sekta hizo katika kusaidia vita dhidi ya umasikini barani Afrika.

Melinda alisema ni wajibu wa serikali za Afrika kuwasaidia wakulima, kulima mazao ambayo yahawezi kuathiriwa na mabadiliko ya tabia nchi na hilo litawezekana kama kukifanyika tafiti za kutosha katika sekta ya kilimo.
 
Hata hivyo, alisema ni vyema wakulima wadogo wapewe uhuru wa kuchagua kulima mazao ambayo wao wanayamudu na rahisi kwao kama kilimo cha mihogo.

Alisema msaada ni muhimu kwa wakulima wadogo, kwani wengi ambao wanajihusisha na kilimo vijijini ni akina mama, ambao malengo yao makubwa yamekuwa ni kupata fedha za kusomesha watoto wao na pia kuwahudumia kiafya.

Hata hivyo, alieleza kuridhishwa na watendaji wa AGRA kutokana na kuwa na program mbali mbali za kusaidia sekta ya kilimo barani Afrika na sasa wamefikiwa zaidi ya wakulima wadogo  milioni moja.


Awali Rais wa AGRA, Jane Karuku akizungumza katika mkutano huo,alisema taasisi hiyo kwa kushirikiana na serikali kadhaa barani Afrika na taasisi binafsi imeweza kusaidia sekta ya kilimo, hasa katika upatikanaji mbegu bora na masoko.

Alisema bara la Afrika bado linahitaji uwekezaji mkubwa katika sekta ya kilimo, ili kuwa na uhakika wa chakula la lishe na hilo litawezekana kama wakulima wadogo hasa wa vijijini wakisaidiwa katika kupata pembejeo,miundombinu bora ya kuwafikia na masoko.

Rais huyo, alisema taasisi hiyo, itaendelea kusaidia miradi kadhaa ya kilimo nchini Tanzania na maeneo mengine, ikiwepo pia kusaidia taasisi za utafiti na mbegu ili kuweza kuwasaidia wakulima hasa wa vijijini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.