Habari za Punde

Arsenal yapeleka kilio Spurs

 
LONDON, Uingereza
 
KLABU ya Arsenal,  iliifanyia mauaji makubwa timu ya Tottenham Hotspurs kwa kuichapa mabao 5-2 katika mechi ya ligi kuu ya Uingereza iliyopigwa katika uwanja wa Emirates.
 
  Hata hivyo, Tottenham walikuwa wa kwanza kuziona nyavu za wapinzani wao kwa bao la dakika ya kumi lililofungwa na mchezaji wa zamani wa Arsenal Emmanuel Adebayor baada ya mlinda mlango Szczesny kuutema mpira wa Jermain Defoe na kumkuta mfungaji.


  Muda mfupi baada ya kupachika bao hilo, mwamuzi wa pambano hilo alimfurusha nje kwa kadi nyekundu Adebayor katika dakika ya 17 baada ya kumchezea vibaya Cazorla.
 
Kutolewa kwa Mtogo huyo kulionekana kumchanganya Meneja wa Spurs AVB ambaye alisimama muda mwingi kutoa maelekezo kwa wachezaji wake.
 
Arsenal ilipiga hatua moja mbele baada ya kusawazisha bao hilo katika dakika ya 23 kupitia kwa mchezaji wake Mertesacker aliyeunganisha kwa kichwa mpira wa kona uliopigwa na Theo Walcot.
 
Jitihada za Spurs kutaka kusawazisha bao hilo, zilirejeshwa nyuma baada ya kupachikwa bao la pili mara hii likifungwa na Lucas Podolski katika dakika ya 41 baada ya kuufuma mpira uliomgonga beki wa zamani wa Arsenal William Gallas.
 
Kama hilo halitoshi, nyavu za Spurs zikachanwa tena sekunde chache kabla mapumziko kwa goli la Olivier Giroud aliyeinasa pasi ya Cazorla.
 
Timu hizo zilikianza kipindi cha pili kwa kasi lakini Spurs walionekana kuelemewa zaidi kutokana na pengo la Adebayor, kwani katika dakika ya 58, walimruhusu Cazorla kuandika bao la nne akiunganisha krosi ya Podolski.
 
Washambuliaji wa Spurs walipigana hadi wakafanikiwa kuambulia bao la pili katika dakika ya 69, lililofungwa na Gareth Bale kwa shuti kutoka nje ya eneo la 18.
 
Huku wachezaji wa Spurs wakihaha kusaka mabao zaidi, mbio zao zilikwama baada ya Walcott kuipatia Arsenal goli la tano katika dakika ya 88 kutokana na mpira wa krosi uliomiminwa langoni na Oxlade Chamberlain.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.