Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MKUTANO wa uchaguzi mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ambao ulipangwa kufanyika mwezi ujao, sasa umesogezwa mbele hadi Februari 16 na 17 mwakani.
Hatua hiyo inafuatia Kamati Tendaji ya TFF kuafiki mapendekezo ya marekebisho ya katiba katika kikao chake cha Novemba 3, mwaka huu.
Taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya TFF, Wakili Alex Mgongolwa, imesema baada ya kutafakari mapendekezo hayo, kamati hiyo imeamua kuifanyia marekebisho katiba ya shirikisho hilo kama iliyopendekezwa.
“Kwa vile mapendekezo mawili kati ya matatu ya marekebisho ya katiba yana uhusiano na uchaguzi mkuu wa TFF, ipo haja ya marekebisho hayo kufanyika kabla ya kutangazwa kwa mkutano mkuu wa TFF na kuanza kwa mchakato wa uchaguzi mkuu”, imesema taarifa ya Mgongolwa.
Aidha, Mgongolwa amesema kwa vile TFF haina uwezo wa kuitisha mikutano mikuu miwili – mkutano mkuu maalum kwa ajili ya marekebisho ya katiba ya TFF; na ule wa uchaguzi katika kipindi kifupi kijacho, marekebisho ya katiba yafanywe kwa njia ya waraka (‘Circular Resolution’).
Waraka huo ulipaswa uwe umeshatayarishwa na sekretariati ikishirikiana na Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria ifikapo tarehe 15 Novemba 2012, na kukabidhiwa kwa wajumbe wa Kamati Tendaji wanaowakilisha kanda za TFF ambao watahakikisha kuwa kila mjumbe wa mkutano mkuu wa kanda husika anapata fursa ya kutoa ridhaa yake.
Aidha, wakili huyo ameagiza zoezi la kupata ridhaa ya wajumbe wa mkutano mkuu liwe limemalizika katika kipindi cha siku 21 na kwamba kikao kinachofuata cha Kamati Tendaji Disemba 15, mwaka huu kiwe kwa madhumuni ya kupokea taarifa ya zoezi hilo na kufanya matayarisho ya mkutano mkuu.
No comments:
Post a Comment