Habari za Punde

Kamati ‘Mapinduzi Cup’ yaanza kazi

Precission Air, ZATI, Z’bar Ocean zachangia 15 m/-
 
Na Ameir Khalid
 
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, juzi usiku alitoa baraka kwa Kamati ya Kombe la Mapinduzi kuanza kazi rasmi, katika hafla iliyofanyika ukumbi wa Bahari, hoteli ya Zanzibar Ocean View.
Akizungumza na wajumbe wa kamati hiyo, Balozi Seif alieleza imani yake kuwa itafanya kazi nzuri kama kawaida yake, na hivyo kufanikisha mashindano ya kuwania Kombe la Mapindizi mwaka ujao, ili yawe mazuri zaidi.
Aliisifu kamati hiyo ya watu kumi, kutokana na jitihada zake za kufufua vuguvugu la mpira wa miguu nchini, ambalo kwa miaka ya karibuni, limeonekana kufifia.
“Mara mbili nimepata bahati ya kuzindua kamati hii na kwa kweli imefanya kazi nzuri kwa kualika timu bora kushirki mashindano, na hivyo kurejesha haiba ya soka nchini, hasa kutokana na kuongozwa na watu makini na wenye kuaminika”, alisema.
Alieleza matarajio yake kuwa, baada ya kumalizika mashindano ya mwakani ambapo sherehe za Mapinduzi zitatimiza miaka 49, ile ya mwaka 1914 itakuwa mama wa mashindano yote kutokana na kuadhimisha nusu karne ya Mapinduzi hayo.
Aliahidi kuwa Serikali itakuwa bega kwa bega na kamati hiyo kwa kuipa ushirikiano ili kufanikisha mashindano ya mwaka.
Mapema, akimkaribisha Makamu wa Pili wa Rais, Mwenyekiti wa kamati hiyo Mohammedraza Dharamsi, alisema ni dhamira yao kuona soka la Zanzibar lnarejesha hadhi yake, pamoja na kutaka sherehe za Mapinduzi zipambwe pia na michezo mingine.
Kamati hiyo iliyopewa baraka za kuendelea na kazi zake, inaundwa na Mohammedraza Dharamsi (Mwenyekiti), Sharifa Khamis Salim (Makamu Mwenyekiti), Amani Ibrahim Makungu Mshika Fedha) na Khamis Said Abdallah (Katibu).
Wajumbe ni Ali Khalil Mirza, Ali Saleh Mwinyikai, Nassor Salim Ali, Abubakar Bakhresa, Issa Mlingoti na Farouk Kareem.
Katika hatua nyengine, Kampuni ya Usafiri wa Anga ya Pressicion Air, Kampuni ya Huduma za Ndege (ZAT) na hoteli ya Zanzibar Ocean View, kila moja imechangia shilingi milioni tano ili kufanikisha mashindano hayo.
 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.