Habari za Punde

Mjini bingwa ‘Mzee Kheir Cup’

 
 
Na Ameir Khalid
 
TIMU ya kombaini ya vijana Wilaya ya Mjini iliyo chini ya miaka ya 16, imefanikiwa kutwaa ubingwa wa michuano ya kumuenzi kocha wa zamani wa KMKM marehemu Mzee Kheir.
 
Mjini ilivaa taji hilo baada ya kuifunga timu ya Wete magoli 3-1, katika mchezo uliopigwa uwanja wa Amaan juzi.
 
Awali, fainali hiyo ilikuwa izikutanishe Wilaya ya Mjini na Magharibi Jumapili iliyopita, lakini Magharibi ikagomea mchezo kwa madai ya waandaaji kupunguza kiwango cha fedha za zawadi kwa washindi.

 
Katika mchezo huo, Wilaya ya Mjini ilijipatia magoli yake katika kila kipindi kupitia kwa wachezaji wake Juma Ali aliyecheka na nyavu mara mbili katika kipindi cha kwanza.
 
Goli la tatu la washindi hao lilifungwa na Is-haka Mibomba, na lile la kufutia machozi kwa vijana wa Wete likawekwa kimiani na Nassir suleiman.
 
Kufuatia ushindi huo, mgeni rasmi mchezaji veterani Salum Bausi aliikabidhi Wilaya ya Mjini kombe na fedha shilingi milioni moja, na laki tatu kwa washindi wa pili, timu ya Wete, zawadi ambazo zilitolewa na kampuni ya Arma Promotions.
 
Mashndano hayo yalizishirikisha timu za kombaini za vijana wenye umri chini ya miaka 16 kutoka Wilya zote kumi za Unguja na Pemba.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.